Ulishajiuliza kabla ya ujio wa saa, mababu zetu walijuaje nyakati?
James Mfikwa, mhifadhi kijiji cha Makumbusho anaeleza kwa undani njia walizotumia wahenga katika kujua muda na kufanya shughuli zao.
Kikubwa anasema walitumia jua na kivuli kufahamu majira ya asubuhi, mchana, alasiri na jioni.
“Kwa mfano, mtu akisimama sehemu ambapo hakuna msongamano wa miti au jengo, alikuwa anaangalia kivuli chake. Kama kivuli kimeangukia upande wa magharibi na kirefu kwa kiasi fulani, atakuambia saa hizi ni asubuhi,”anasema.
Anasema kivuli hicho kikiendelea kupungua urefu hadi kufika hatua ya kumzunguka kwenye miguu, majira hayo kwao yalikuwa ndio mchana.
Anasema kwa muda huu kama walikuwa shambani, wataambizana ni muda wa chakula, huku mume akimwambia mama akaandae chakula.
Anasema kwa jioni, kivuli hubadilisha mwelekeo, kwani jua linavyozidi kwenda Magharibi kuzama, kivuli nacho kinakuwa kirefu zaidi kwenda Mashariki.
“Kwa hiyo hapo mtu anaweza kukuambia saa hizi ni alasiri. Na anajua hilo kwa kwa kuangalia jua na kivuli.Hapo sasa hata kama watu walikuwa shamba wanaacha na kurudi nyumbani, kwani hata jua linakuwa dhaifu na kama kuna mifugo ya kulisha jioni, huo ndio ulikuwa muda wa kufanya hivyo,’’ anaeleza.
Kwa majira ya usiku, anasema wahenga walikuwa wakitumia mwezi kujua muda.Mfikwa anasema kitaalamu mwezi huwa unatembea na kitu pekee kilichosimama ni jua.
“Hivyo mwezi unapozunguka jua na yale mabadiliko yanayotokea wakati wa kuzunguka kwake, ndio ilikuwa ikiwafanya wajue ni muda kwa usiku.
‘’ Kwa mfano, mwezi ukiwa mkamilifu, ikiwa saa moja jioni mwezi unakuwa mwekundu, kesho unakuta hauchomozi saa moja, bali saa mbili,”anasema mhifadhi huyo.
Anasema ikifika usiku wa manane, mwezi hubadilika mahala ulipo, huku alfajiri mwezi ukielekea upande wa Magharibi. Kwa hiyo anasema hapo walijua kuwa sasa kunaelekea kukucha.
Hata hivyo, anasema makadirio hayo ya muda yalikuwa yakitofatiana kulingana na jiografia ya watu walipo.
“Kwa mfano, kwa wanaovua walikuwa wakitumia sana mwezi na mpaka sasa baadhi hufanya hivyo licha ya kuwepo kwa teknolojia nyingine. Ili wasipotee walitumia mwelekeo wa mwezi au nyota.
“Mfano nyota huwa zinakusanyika sehemu moja inapofika usiku, na kwa mwelekeo wake walijua namna ya kuzifuata ili kuwasaidia kurudi, hivyo walikuwa hawapotei,’’ anaeleza.
Kuhusu majira ya mwaka, Mfikwa anasema walikuwa wanaangalia kiwango cha joto kilichowaonyesha wapo katika kipindi gani.
Anasema joto likiwa kali sana hadi kuleta fukuto, wazee walikuwa wakianza kuandaa mashamba na baada ya mwezi mmoja mvua kweli inanyesha.
“Kihistoria hata Wamisri tunaambiwa walitumia mwezi kujua vipindi vya mvua ili kuweza kuandaa mabwawa ya kujaza maji kutokana na nchi ile kuwa jangwa,”anasema.
Anasema kuelekea msimu wa kiangazi, hali inabadilika kutoka kwenye joto, kwenda kwenye ubaridi, ambapo hali hiyo ilikuwa ikianza Juni hadi Septemba.
Hata hivyo, anasema kwa sasa utabiri wa hali hii ni mgumu kutokana na uwepo wa mabadiliko ya tabianchi.
Kuhusu kujua siku, Mfikwa anasema kwao maisha yao hayakuwa na majina ya siku kama ilivyo sasa.