Wakati mashabiki wa ndondi wakihesabu saa kushuhudia wababe wa Knock Out ya Mama, mabondia watano wa Tanzania watapanda ulingoni kuwania mikanda ya ubingwa.
Pambano hilo litawakutanisha mabondia 34 wa ndani na nje ya Tanzania kwenye Ukumbi wa Super Dome, Masaki usiku wa leo Desemba 26, 2024.
Tayari amshaamsha za pambano zinaendelea ukumbini hapo, huku Watanzania wanaowania mikanda ya ubingwa wakiwekewa bonusi ya Sh10 milioni kila mmoja iwapo atashinda kwa Knock Out (KO).
Watanzania hao ni Kalolo Amir anayezichapa na Shile Jelwana wa Afrika Kusini kuwania ubingwa wa Pugilistic Syndicate of Tanzania (PST).
Mwingine ni Salmin Kassim anayechuana na Adrian Lerassan wa Ufilipino kuwania ubingwa wa Mabara wa World Boxing Federation (WBF)
Said Chino atakuwa na shughuli dhidi ya Michael Klassen wa Afrika Kusini kuwania ubingwa wa Mabara wa International Boxing Association (IBA)
Ibrahim Mafia atazichapa na bondia wa nne kwa ubora nchini Afrika Kusini, Lusizo Manzana kuwania mkanda wa ubingwa World Boxing Champion (WBC) Africa.
Wakati Yohana Mchanja akizichapa na Miel Farjado wa wa Ufilipino kuwania ubingwa wa World Boxing Organisation Global Championship.
Kama watashinda kwa KO, mabondia hao wataondoka na bonasi ya Sh10 milioni kwenye pambano hilo.
Kama itatokea bondia atashinda kwa pointi ataondoka na kitita cha Sh5 milioni huku mabondia wengine wa Tanzania watakaozichapa na mabondia wa nje watakaoshinda wataondoka na kitita cha Sh1 milioni kila mmoja ambayo ni zawadi ya Boxing Day.
Endelea kufuatilia Mwananchi kutoka The Super Dome wakikuletea moja kwa moja mapambano hayo.