Mjadala wa chimbuko la shikamoo, umuhimu wake

Maamkizi ya “shikamoo” ni sehemu muhimu ya tamaduni za Kiswahili na yanadhihirisha heshima na unyenyekevu, hasa kwa wazee au wale waliotutangulia kijamii.

Katika jamii za Kiafrika, heshima kwa wakubwa ni msingi wa maadili, na shikamoo hutoa nafasi ya kudumisha uhusiano wa heshima na mshikamano wa kijamii.

Hata hivyo, swali la iwapo ni lazima shikamoo ibaki kama maamkizi rasmi, linategemea mabadiliko ya kijamii na mapokeo ya vizazi vipya.

Wakati baadhi ya watu wanapendelea salamu hiyo kwa sababu ya mizizi yake ya heshima, wengine, hasa vijana wanachukulia shikamoo kuwa ya kizamani au isiyohitajika.

Badala yake, wanapendelea maamkizi yasiyo rasmi kama “mambo” au salamu za kidini kama “Assalaam aleykum” au “Tumsifu Yesu Kristo.”

Asili, maana ya maamkizi shikamoo

Salamu ya shikamoo ni miongoni mwa maamkizi yanayobeba uzito wa heshima kubwa katika jamii zinazotumia Kiswahili.

Neno shikamoo lina maana ya “nashika mguu wako,” ikionyesha unyenyekevu na heshima kwa yule anayesalimiwa.

Asili ya salamu hii inahusishwa na enzi za utumwa, ambapo watwana walikuwa wakiwasalimu mabwana zao kwa heshima ya kiwango cha juu, ikimaanisha kuwa “niko chini ya miguu yako.”

Kwa muktadha wa kisasa, shikamoo imepata maana pana zaidi. Hutumika kama ishara ya heshima kwa mtu aliyekuzidi umri, cheo, au hata mali. Ni sehemu ya utamaduni wa Kiswahili inayothamini heshima na maadili katika mawasiliano ya kila siku.

Ni katika muktadha huu, usishangae kumkuta mtu mzima wa miaka 50 akimpa shikamoo kijana wa miaka 40.

Mapokeo tofauti ya salamu ya shikamoo

Ingawa shikamoo inaheshimiwa kama salamu rasmi, mtazamo wake hutofautiana kati ya watu na makundi tofauti.

Wapo wazee wanaopendelea kusalimiwa shikamoo, lakini kuna wengine  hawapendezwi na salamu hii, wakiona ni ya kizamani au yenye kuashiria utegemezi.

Badala yake, wanapendelea salamu zisizo rasmi kama “mambo” au “heshima yako mwalimu au heshima yako baba.”

Aidha, baadhi ya watu wanaunganisha shikamoo na salamu za kidini au za kijamii. Kwa mfano, baadhi ya familia hutumia salamu mbili, moja ya kidini kama “Assalaam aleykum” kwa Waislamu au “Tumsifu Yesu Kristo” kwa Wakristo, na nyingine ya kijamii kutokana na lugha zao za asili.

Pia, kuna wanaochanganya salamu hizo kwa kuanza na “Assalaam aleykum” na kumalizia na shikamoo, hasa katika mazingira ya heshima ya kijamii.

Matumizi ya salamu tofauti katika jamii

Mbali na shikamoo, kuna aina nyingine nyingi za salamu zinazotumiwa kulingana na muktadha wa mazungumzo, muda na uhusiano kati ya watu.

Salamu hizi ni pamoja na “habari za asubuhi,” “habari za mchana,” “mambo,” “niaje,” na “vipi mishe.”

Hata hivyo, shikamoo bado inachukuliwa kuwa salamu rasmi na yenye uzito mkubwa wa heshima.

Mtazamo wa kamusi na wataalamu wa Kiswahili

Kamusi mbalimbali zimefafanua shikamoo kama salamu ya heshima. Kwa mujibu wa Kamusi ya TUKI (2014), shikamoo ni salamu inayotolewa kwa mtu aliyekuzidi umri.

Vilevile, Kamusi ya Bakita (2015) inatafsiri shikamoo kama tamko la heshima linalotumiwa kumwambia mtu mwenye umri mkubwa, huku ikibainisha kuwa asili ya neno hili ni Kiarabu.

Kwa upande mwingine, Kamusi ya Bakiza (2010) inaeleza kuwa salamu hii ni ishara ya heshima ya mtu mwenye umri mdogo kwa mtu mwenye umri mkubwa.

Kutokana na fasili hizi, ni wazi kuwa msingi wa salamu ya shikamoo ni heshima inayotolewa kwa kuzingatia umri.

Hata hivyo, kama shikamoo ni maamkizi ya mdogo kumsalimu mkubwa, je, watwana wote waliokuwa wakilitumia neno hilo utumwani, walikuwa  na umri mdogo kwa mabwana zao?

Mwandishi Jillo Said katika ukurasa wake wa Facebook anaandika: “Kila mtumwa alipaswa kujua na kutambua salamu hii. Na mtumwa alipaswa kutoa salamu hii hata mara 100 kwa siku moja. Lengo la salamu hii ilikuwa ni kutenganisha kati ya mtumwa na bwana wake.”

Anaendelea kuandika: “Kuanzia miaka ya 600-1700, salamu hii ilikuwa ikitumika maeneo ya Pwani tu. Na kuanzia miaka ya 1700 mwishoni na 1800 mwanzoni Waarabu walianza kuingia maeneo ya ndani ya Afrika Mashariki na kila walipofika salamu hii waliitumia na baadhi ya machifu walipenda sana salamu hii.”

Baadhi ya jamii, shikamoo huambatana na vitendo vingine kama kushikana mikono, kushika kichwa cha anayesalimiwa, au hata kubusiana kwenye viganja vya mikono.

Vitendo hivi vinaimarisha ujumbe wa heshima unaokusudiwa kupitia salamu hiyo.

Hata hivyo, swali linabaki, je salamu hii inapaswa kuendelea kutumika kwa wakati wa sasa na ujao?

Related Posts