Mtoto wa mfanyabiashara maarufu Dodoma auawa na watu wasiojulikana

Dodoma. Mtoto wa mfanyabiashara maarufu jijini Dodoma anayejulikana kwa jina la Jojo, Graison Kanyenye (6), anadaiwa kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani wakati mama yake akiwa matembezini usiku wa kuamkia jana.

Mbali na hilo, Jeshi la Polisi limesema mwili wa mtoto huyo ulikutwa ndani ya nyumba ukiwa na majeraha shingoni.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi amesema jana, Desemba 25, 2024 kuwa tukio litokea saa 1.00 asubuhi katika Mtaa wa Bwawani, Ilazo Extension jijini Dodoma, nyumbani kwa Ofisa Uvuvi wa Mtera, Hamis Mohamed.

Amesema Hamis (anatajwa kuwa mpenzi wa mfanyabiashara huyo) na mama yake walitoka kwenda matembezini na kumwacha mtoto huyo chini ya usimamizi wa dereva bodaboda wa Ilazo Extension, Kelvin Gilbert.

Bodaboda huyo anayetajwa kuwa walimfahamu kupitia huduma ya usafiri wanayoitoa kwa familia, aliachiwa mtoto ili amwangalie kipindi ambacho watakuwa kwenye matembezi wawili hao (Hamis na mfanyabiashara huyo).

“Kelvin Gilbert aliachiwa mtoto huyo amwangalie, wakati Hamis na mama yake walipoondoka kwenda matembezini, lakini waliporudi saa 1.00 asubuhi walikuta mtoto Graison Kanyenye Mabuya (6) amepigwa kichwani na kitu kizito kwenye paji la uso, huku akiwa na majeraha shingoni,” amesema.

Mtoto Grayson Kanyenye (6) akiwa na mama yake enzi za uhai wake.

Amesema mtoto huyo alikutwa amefariki dunia na dereva bodaboda hakuwepo ndani ya nyumba, walipomtafuta walimkuta nje ya nyumba hiyo.

Kamanda Katabazi, amesema wanaendelea kumshikilia Kelvin kujua kilichotokea hadi mtoto huyo kuuawa.

Alipoulizwa chanzo cha mauaji hayo, Kamanda Katabazi amesema bado polisi wanaendelea na uchunguzi.

Amesema katika mahojiano ya awali kati ya polisi na dereva huyo wa bodaboda, amekana kuhusika na tukio hilo.

Aidha, Kamanda Katabazi amewataka wakazi wa Dodoma kuhakikisha wanawaacha watoto chini ya uangalizi wa watu wanaowaamini, ili kuwalinda na vitendo vya kikatili.

Mmoja wa majirani wa Jojo ambako msiba wa mtoto huo upo, Munira Hassan amesema amepata taarifa za kuuawa kwa mtoto huyo saa 6.00 mchana jana baada ya kuona ujumbe (post) katika ukurasa wa instagram wa Jojo.

 “Chanzo cha mauaji hayo hakijajulikana, ila tunaliomba Jeshi la Polisi kuchunguza kwa haraka ili kuwapata wanaohusika na kuwachukulia hatua za kisheria. Yule mtoto mdogo hana hatia, watu wengi tungetaka kufahamu nini kilichotokea,”amesema.

Habari za kuuawa kwa mtoto huyo zilianza kusikika jijini Dodoma jana asubuhi, huku wengi wakipata taarifa kupitia ukurasa wa mtandao wa kijamii wa mfanyabiashara huyo unaojulikana kama jojoladiespoint alipoandika ‘Pumzika kwa amani baba angu mzuri’ na alama za kopa chini ya picha ya mtoto wake.

Mwananchi lilipokwenda nyumbani kwa mfanyabiashara huyo Majengo Mapya ambako ndiko msiba ulipo, lilielezwa Jojo na Hamis bado wanahojiwa na Polisi. 

Related Posts