Musoma. Benki ya CRDB imefungua matawi mawili mapya mkoani Mara, Mugango (Musoma Vijijini) na Sirari (Tarime), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kusogeza huduma karibu na wananchi kwa kaulimbiu ya ‘ulipo, tupo’.
Ofisa Mkuu wa Biashara wa CRDB, Boma Raballa amesema matawi hayo yameanzishwa kutokana na mahitaji makubwa ya huduma za kifedha katika shughuli za uchumi kama madini, kilimo, uvuvi na biashara ya mpakani.
Raballa amesema kabla ya ufunguzi huo, wananchi walitegemea mawakala wa benki walioko maeneo mbalimbali nchini.
“CRDB ina mawakala zaidi ya 600 mkoani Mara, wakiwemo 195 Tarime na 35 Musoma vijijini. Utafiti uliofanywa na benki umeonyesha umuhimu wa kuwa na matawi kamili ili kuboresha huduma kwa wananchi,” amesema.
Akizindua tawi la Sirari, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele leo Alhamisi, Desemba 26, 2024 amesisitiza umuhimu wa huduma za benki kwa maendeleo ya mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.
Amewahimiza wananchi kujitokeza kulitumia tawi hilo kwa kuwekaakiba, kupata mikopo na kubuni miradi yenye tija.
Pia, amehamasisha uwekezaji katika Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond, aliyosema inalipa faida ya asilimia 12 kila mwaka kwa miaka mitano na inaweza kutumika kama dhamana ya mkopo.
Katika uzinduzi wa tawi la Mugango, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya amewataka vijana na wanawake kutumia fursa ya programu ya Imbeju ya CRDB kupata mitaji na ushauri wa kitaalamu kwa ajili ya kuimarisha biashara zao.
Wakati huohuo, benki hiyo imetoa msaada wa madawati 50 yenye thamani ya Sh5 milioni kwa shule za msingi na sekondari wilayani Tarime.
Akipokea madawati hayo, Mkuu wa Wilaya, Gowele amesema yatasaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Ufunguzi wa matawi hayo mawili unaashiria dhamira ya CRDB katika kukuza ushirikishwaji wa kifedha na kuchangia maendeleo ya jamii na uchumi wa Taifa kwa ujumla.