Baada ya kupoteza mechi iliyopita kwa mabao 4-0 dhidi ya Yanga, Tanzania Prisons imemalizia hasira zao kwa Pamba Jiji kufuatia ushindi wa bao 1-0.
Ushindi huo unakuwa wa kwanza katika mechi mbili kwa kocha Shaban Mtupa aliyekabidhiwa majukumu kwa muda wakati aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Mbwana Makata akisubiri hatma yake na mabosi.
Katika mechi hiyo iliyopigwa leo Desemba 26, 2024 Uwanja wa Sokoine jijini hapa, kipindi cha kwanza Prisons ilicheza kwa utulivu na nidhamu na kufanikiwa kupata bao dakika ya 31 kupitia Tariq Simba.
Hata hivyo, Wajelajela hao walipata pigo baada ya kipa wao, Sebusebu Samson kushindwa kumaliza dakika 45 za kwanza kufuatia kuumia baada ya kugongana na Habibu Kyombo na kuwahishwa hospitali, huku nafasi yake ikichukuliwa na Edward Mwakyusa.
Pamba Jiji chini ya Kocha wake Fred Felix ‘Minziro’ aliwaanzisha baadhi ya nyota wake wapya Habibu Kyombo, Zabona Hamis na Deus Kaseke ambao walikubali kuzidiwa kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili Pamba Jiji ilirejea kwa kasi ikitengeneza nafasi kadhaa, lakini Kipa Mwakyusa alikuwa imara akisaidiwa na mabeki wake kuokoa hatari zote.
Dakika ya 90 Pamba ilijikuta pungufu kufuatia nyota wake Erick Okutu kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Abubakar Mturo kutoka Dar es Salaam baada ya kumchezea rafu Ismail Ally.
Kabla ya mechi hiyo, Pamba Jiji ilitoka ugenini kupoteza alama tatu dhidi ya KMC kwa kufungwa bao 1-0, huku Prisons ikilala 4-0 dhidi ya Yanga.
Mara ya mwisho Pamba Jiji kupata ushindi katika ligi ni Novemba 5 mwaka huu ilipoikanda Fountain Gate mabao 1-3 ugenini, huku Prisons nao kabla ya ushindi wa leo iliwachapa KenGold bao 1-0, Novemba 3 mwaka huu.
Matokeo hayo yanaifanya Prisons kuchumpa kutoka nafasi ya 15 hadi 13 ikifikisha pointi 14 na kuishusha Pamba Jiji yenye alama 12 baada ya michezo 16 kila moja.