Rupia ajichomoa vita ya kiatu Ligi Kuu Bara

MSHAMBULIAJI wa Singida Black Stars, Elvis Rupia amesema licha ya kuongoza katika mbio za ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa na mabao manane, lakini lengo lake ni kuhakikisha kikosi hicho kinafanya vizuri zaidi.

Nyota huyo amefikisha mabao hayo baada ya juzi kuifungia timu hiyo bao moja katika ushindi wa 2-1 dhidi ya KenGold na kumfanya kuongoza akifuatiwa na kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua aliyefunga mabao saba.

“Kama itatokea nikawa mfungaji bora nitafurahi sana kwa sababu ndio malengo ya mshambuliaji yeyote, ingawa jambo ambalo naliangalia zaidi ni kuona kwanza timu inafanya vizuri na kutimiza tulichokikusudia cha kumaliza nafasi nne za juu,” alisema.

Rupia aliongeza jambo kubwa analojivunia ndani ya kikosi ni ushirikiano anaoupata kutoka kwa wenzake akiamini mwenendo huo ni chachu ya wachezaji, benchi la ufundi na viongozi kufikia malengo.

Kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Ramadhan Nswanzurimo alisema anajivunia uwepo wa mshambuliaji huyo ingawa amemtaka kuongeza umakini wa kutumia nafasi zinazopatikana.

Rupia alijiunga na kikosi hicho msimu wa 2023-2024 akitokea Police FC ya Kenya ambako alifunga mabao 27 na kuivunja rekodi iliyochukua miaka 47 katika Ligi Kuu Kenya ya Moris Aloo Sonyi aliyefunga 26, mwaka 1976 akiwa na Gor Mahia. Katika msimu wake wa kwanza, Rupia alichezea timu mbili tofauti akianza na Singida Fountain Gate kisha dirisha dogo akatua Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars.

Related Posts