Wakati zikisalia siku kufunga mwaka 2024, yapo mengi ya kufahamu kuhusu ulivyokuwa mwaka, miongoni mwake ni magari yaliyobamba katika kipindi hicho, yaani ni yapi yalinunuliwa zaidi.
Tanzania ina viwanda vichache vya kuunda/kuunganisha magari na sehemu kubwa ya magari yanayotumiwa nchini yameagizwa kutoka nje ya nchini, hususan Japan na Afrika Kusini na yaliyo mengi ni yaliyokwisha tumika (used).
Kwa mujibu wa Ripoti ya mwenendo wa Uchumi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hadi Oktoba, 2024 Tanzania ilitumia Sh832.79 bilioni kuagiza magari kwa ajili ya matumizi binafsi, sawa na wastani wa Sh83.27 bilioni kwa mwezi.
Kwa kawaida ununuzi wa magari Tanzania umetawaliwa na magari madogo ya abiria kwa matumizi binafsi, yaani magari yenye siti tano hadi saba, hayo ndiyo mengi mtaani, unaweza kuyaona kirahisi.
Magari ni mtindo kama ilivyo kwa bidhaa nyingine za anasa, japo kulingana na mazingira na hali, lakini kwa baadhi ya maeneo ni hitaji la msingi na kila gari linanunulia kwa sababu, iwe ni ya kiuchumi au kimazingira.
Katika miaka ya hivi karibuni gari aina ya Toyota IST na Toyota Harrier na Subaru Forester yameendelea kuwa miongoni mwa magari yanayonunuliwa zaidi na Watanzania.
Kwa mujibu wa mtandao maarufu wa uagizaji wa magari nje ya nchi Befoward, ambao hutumiwa na wengi hapa nchini, gari inayoongoza katika orodha ya magari yanayonunuliwa zaidi sasa ni Subaru Forester, ambayo imewahi kujishindia tuzo tofauti kati ya mwaka 2008 na 2009.
Gari hiyo yenye ukubwa wa kati (SUV) mbali na kutajwa na Befoward kama chaguo namba moja kwa Watanzania, pia inatajwa kwa namba hiyo hiyo katika mtandao mwingine maarufu wa uagizaji wa magari nchini (SBT Japan).
Uzao wa kwanza wa Forester ulianza mwaka 1998, uzao wa pili mwaka 2003, uzao wa tatu mwaka 2008, uzao wa nne mwaka 2014 na sasa ipo katika uzao wa tano, ambao ulianza mwaka 2018. Injini zake ni za 2.0L hadi 2.5 (cc2000 hadi 2500) na bei yake ya sasa Sh22 milioni na kuendelea.
Gari inayofuatia kwa kununulia zaidi Tanzania ni Toyota Harrier, ambayo imeanza kuzalishwa karibu miongo mitatu iliyopita, uzao wake wa kwanza ukitoka mwaka 1997, mpaka sasa ipo katika uzao wa nne ambao ulianza mwaka 2020 na unaendelea mpaka sasa.
Toyota ilizalisha gari hiyo yenye injini ya 2.2L hadi 2.0L kwa ajili ya kushinda na masoko ya SUV zinazozalishwa na kampuni ya Mercedes Benz uzao wa ML-Class na BMW X5 ambazo, mpaka sasa zipo Harrier zinazotumia Petroli, Dizeli na Chotara (Hybrid).
Harrier ambayo imepata sifa nzuri katika eneo la usalama inashika nafasi ya pili katika mitandao wa Befoward na SBT Japan, lakini hata mtaani pia unaweza kuziona kwa wingi.
Gari nyingine ambayo imebamba sana mwaka huu ni Mazda CX5, hii haikuwa kwenye orodha ya magari yaliyonunuliwa kwa wingi miaka ya nyuma, lakini kwenye orodha ya Befoward imeshika nafasi ya tatu mwaka huu, huku ikishika nafasi ya sita katika mtandao wa SBT Japan.
Gari hiyo iliyoanza kutengenezwa mwaka 2012 ipo katika matoleo tofauti na matumizi yake ya mafuta yapo kwa petroli. Kwa Tanzania zinapendelewa zaidi zenye injini ya dizeli, licha ya kuwa wapo wachache wanaopendelea za petroli.
Gari hiyo ni kielelezo cha teknolojia mpya ya Mazda iitwayo Skyactiv na sifa kubwa ya gari hiyo ni unywaji wa mafuta mzuri ikilinganishwa na gari nyingine zenye sifa na ukubwa kama wa kwake, katika soko la Bongo gari hiyo bado inabamba sana.
Injini zake za Skyactiv zipo katika cc kuanzia 2.0L hadi 2.5L, mbali na unywaji mzuri wa mafuta wengi wanazipendea muundo wake wa kisasa na zina soko kubwa katika mataifa ya Japani, Malaysia, Russia, China, Ulaya na Amerika ya Kaskazini.
“Mimi nimenunua CX5 kwa sababu inakunywa mafuta vizuri, karibu nusu ya magari mengine inayolingana nayo, dizeli ya Sh10,000 inanipeleka kazini na kurudi wakati kwa harrier nilikuwa natumia Sh20,000 na ina nafasi kubwa ndani,” alisema Allex John, mmiliki wa CX5 mkazi wa Dar es Salaam.
Mazda CX5 inauzwa kwa gharama ya kuanzia Sh30 milioni na kuendelea.
Hii imekuwa kwenye Top 5 ya orodha ya magari yanayonunuliwa zaidi Tanzania kwa muda sasa, pengine ni kutokana na gharama zake ndogo za uendeshaji, ikiwemo unywaji mzuri wa mafuta na upatikanaji wa vipuri kiurahisi.
IST ilianza kuzalishwa mwaka 2002, awali ililenga soko la Japan pekee, lakini ikijikuta ikivutia masoko mengine, ukubwa wa injini yake ni 1.3L hadi 1.5L na vipuri vingi vya gari hiyo ambayo ina mfumo wa 2WD na 4WD vinaingiliana na Toyota Vitz.
Pamoja na utulivu barabarani, safa yake kubwa huko ulimwenguni ni kuwa ina eneo dogo la maegesho, ikimaanisha kuwa inaweza kuegeshwa hata katika nafasi finyu. Kwa Tanzania inapatika kwa bei ya kuanzia Sh17 milioni na kuendelea.
“Hata kama nitanunua magari mangapi lazima nitakuwa na IST hata moja, hii gari haina roho mbaya, haisumbui, hainywi mafuta na vipuri vyake ni rahisi kwa bei na upatikanaji wake,” alisema Oscar Mbundu, mmiliki wa IST.
Hii katika mtandao wa Befoward ilishika nafasi ya tano, lakini katika mtandao wa SBT Japani inatajwa kuwa ilishika nafasi ya tatu kwa kununuliwa zaidi, uzao wake wa kwanza ulianza 2002 na injini zake zina ukubwa wa 2.4 hadi 3.5.
Alphard ambayo ina uwezo wa kupakia watu ambao wamekaa kwa starehe kabisa uzao wake wa pili ulianza mwaka 2008, uzao wake wa tatu ulianza mwaka 2015 na uzao wa nne ulianza mwaka 2023 na unaendelea mpaka sasa. Awali ililenga soko la bara la Asia lakini ikajikuta imevutia duniani nzima.