Dar es Salaam. Wale wapandisha maudhui yenye picha na kichwa cha habari (Thumbnail) kisichoendana na video husika katika mtandao wa YouTube sasa kubanwa kila kona baada ya mtandao huo kuja na mfumo wa kuziondoa habari hizo.
Mchakato wa uondoaji ambao utaanzia nchini India kisha kusambaa katika nchi nyingine mapema mwakani. YouTube itakuwa inaangalia picha na kichwa cha habari kilichoandikwa kama kinaendana na video iliyopo endapo ikiwa ni uongo basi video hiyo itaondolewa na inawezekana mhusika akafungiwa akaunti.
Mfano wa habari za namna hiyo ni zile zilizoandikwa misemo yenye kuvutia wasomaji na kuwashawishi wafungue kutazama video ilhali ni uongo, “Tazama hutaamini alichokifanya mtu huyu maarufu bila aibu.’ ‘Rais ajiuzulu’ wakati video haielezi hivyo.
Hivyo katika kukabiliana na hilo mtandao wa YouTube umeanza kampeni ya kuondoa picha na habari za uongo zisizoendana na uhalisia wa video iliyotumwa hatua iliyotajwa kuondoa taharuki katika jamii.
YouTube inasema itapambana na uongo huo ambao inapotosha watazamaji, ikilenga hasa video zinazohusiana na habari muhimu za kisiasa au matukio makubwa ya dharua yanayotokea.
Tovuti ya Financial Express inasema vichwa na picha zinazopotosha zimekuwa tatizo kubwa mara nyingi zikilaghai watazamaji na kupotosha maudhui wanayotarajia kuona.
Mbinu hizi za udanganyifu, ambapo vichwa vya habari au picha zinatoa ahadi za kuvutia au zisizohusiana na maudhui halisi, zinaweza kusababisha watazamaji kukosa imani kisha kufadhaika.
Hatua hii inalenga kuwalinda watazamaji kutokana na kuhisi kudanganywa au kufadhaika wanapotafuta taarifa za wakati husika katika mtandao huo.
Hata hivyo ili kusaidia waandishi wa maudhui, YouTube awali itaondoa maudhui yanayokiuka miongozo mipya bila kutoa adhabu.
Kampuni hiyo pia itazingatia utekelezaji kwenye video mpya zilizowekwa, ikilenga kuzuia upakiaji wa maudhui yanayopotosha badala ya kutoa adhabu kwa video za zamani.
Kama sehemu ya utekelezaji huo, YouTube itaendelea kuwaelimisha waandishi wa maudhui kuhusu umuhimu wa kuweka video zenye ukweli na uhalisia wa kile kilichoandikwa.
Ikifafanua zaidi, tovuti ya New York Magazine imesema mfumo wa YouTube, mtandao wa video za mtandaoni kwa karibu miongo miwili kuwashawishi watazamaji kubofya wa Clickbait hutokea wakati kichwa cha video au picha ya thumbnail inakua na madai ambayo hayapo kwenye video husika.
Katika blogi ya Google imesema dhumuni ni kuhakikisha watazamaji hawapotoshwi kuhusu kile wanachotazama kwenye YouTube.
“Ili kuhakikisha kuwa watayarishi wanapata muda wa kuzoea masasisho haya ya utekelezaji, tutaanza kwa kuondoa maudhui ambayo yanakiuka sera hii bila kutoa onyo.
Akizungumzia hilo alipotafutwa na Mwananchi, Mwanamaudhui wa Youtube nchini, Rashid Mansa amesema ni hatua nzuri kwakuwa inaonesha inajali na inalinda watazamaji.
“Vilevile itaweza kuwa mbaya kwani nafikiri inatumia Akili Mnemba na sidhani kama inauwezo wa kujaji kwa asilimia 100. Pia sisi tunatumia hizi Thumbnail kwa masirahi ya kibishara katika mtandao huo waliojiajiri watu.
“Hili ni janga kwa wanamaudhui wadogo wanaoanza kwakweli. Kilichokuwa kinachofanyika ni mbinu ya kuvutia watu waje ili waone kisha wavutiwe na video nyingine za akaunti yako,” amesema Mansa.
Mmoja ya watumiaji wa mtandao wa YouTube, Amani Joseph amesema hatua hiyo ni nzuri kwani itaondoa uongo uliopo.
“Kuna watu wanafanya hivyo ili wapate watazamaji tu kumbe wanadanganya kilichopo na kilichoandikwa, ni heri wabanwe, itatusaidia hata siye” amesema.
Kwa upande wake, Krantz Mwantepele Mkurungezi Mtendaji wa Koncept Group, amesema kumekuwa na watu wengi waliokuwa wakingia YouTube wanakuta mkanganyiko unaotokana na kila walichokiona awali na wanachokutana nacho.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza uaminifu wa chombo husika cha habari. Pili amesema kwakuwa YouTube watakuwa wameshaweka kwenye sera zao basi mwanamaudhui akienda tofauti atapata adhabu.
“Jambo la tatu itaboresha brand ya media husika kwani ikiwa kinyume na hivyo italeta taswira isiyo nzuri mtu atavutiwa na thumbnail inayoendana na maudhui atayoyapata,” amesema Mwantepele alipotafutwa na Mwananchi.