Dodoma. Mwalimu wa Kwaya ya Shekina iliyoko chini ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Area D jijini Dodoma, Amani Bale amesimulia jinsi mtoto Grayson Kanyenye (6) aliyeuawa, alivyoshiriki uimbaji.
Grayson, mtoto wa mfanyabiashara Zainab Shaban, alifariki dunia usiku wa kuamkia Desemba 25, 2024 nyumbani kwa rafiki yake ambaye ni Ofisa Uvuvi Mtera, Hamis Mpeta, mkazi wa Ilazo Extension jijini Dodoma.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi alisema Desemba 25, 2025 saa 1:00 asubuhi, Mpeta akiwa na mama wa mtoto, Zainab waliporejea kutoka matembezini walibaini ameuawa.
“Walikuta mtoto akiwa ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na shingoni amekatwa na kitu chenye nja kali. Katika tukio hilo, mama alimwacha mtoto huyo chini ya dereva bodaboda anayejulikana kwa jina la Kelvin Gilbert,” alisema.
Alisema walimwacha mtoto na Gilbert saa 6:00 usiku nyumbani kwa Mpeta na waliporejea walikuta ameuawa na dereva hakuwepo.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Desemba 27, 2024, Bale amesema Grayson alipendwa na waumini, walimu na wenzake katika kanisa hilo.
Amesema upendo ulitokana na utulivu wake na hata alipochokozwa na wenzake, alikwenda kutoa malalamiko kwa walimu.
“Mwalimu ananichokoza, mwalimu yule anachezea kinanda (wakati si muda wa kupiga kinanda kwa watoto). Alikuwa mtoto mzuri na kwa umri aliokuwa nao, angekuwa mwimbaji mzuri baadaye,” amesema.
Bale amesema alikuwa na uwezo mkubwa wa kushika kile anachofundishwa.
Amesema Jumamosi ya mwisho (Desemba 21, 2024) alifika kanisani kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimba kwenye ibada ya Jumapili kanisani hapo.
Anasema alimruhusu kushika kipaza sauti kati ya watoto takribani 150 waliopo kwenye kwaya hiyo na alifanya hivyo baada ya kuona ameshika vizuri aliyomfundisha.
Amesema katika wimbo walikuwa wakipishana kuimba na kuitikia, kati ya wavulana wawili na wasichana wawili.
“Kila nikikumbuka machozi yananilenga, hasa nikikumbuka kuwa alipofika Jumapili kanisani, alijua ataimba, hivyo badala ya kusubiri apewe kipaza sauti alienda mwenyewe kukitafuta, kisha kushuka upande wa kushoto wa madhabahu,” amesema.
Bale amewashauri wazazi kuwapeleka watoto kanisani wanapotakiwa kufanya hivyo, ili wajifunze maadili yanayompendeza Mungu, ili waweze kumcha Mungu katika maisha yao.
“Jitihada za kuwapeleka shule za kawaida zimekuwa ni kubwa kuliko wanavyowaleta kwa Mungu, kuwafundisha jinsi ya kuomba, kuwasaidia wengine na kuwaambia wengine habari za Mungu. Wakijisahau hapo watoto watakuwa tofauti na matarajio yao kwa sababu kila kitu huandaliwa,” amesema.
Amesema hakumbuki ni lini Grayson alijiunga na kwaya hiyo, bali alianza kuwafundisha yeye na wenzake zaidi ya 150 tangu mwaka jana.
Bale amesema Grayson alikuwa akipelekwa kanisani na dereva bodaboda kwa ajili ya mazoezi Jumamosi ambayo hufanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana na pia kwenye ibada kila Jumapili.
“Bado tuna machungu, tutamkumbuka kwa muda mrefu. Najaribu kutafakari kesho (Jumamosi Desemba 28, 2024) kama tutaweza kufanya mazoezi, nahisi tutaaanza kulia tu tukimkumbuka Grayson,” amesema.
Rehema Pangasi, mke wa mchungaji wa Kanisa TAG la Area D, amesema mtoto huyo alikuwa mshirika wa kanisa lao na alikuwa mwimbaji wa kwaya ya Shekina.
“Hata Jumamosi hii (Desemba 21, 2024) alikuwa kanisani kwa ajili ya mazoezi ya kwaya. Jumapili alikuwa kanisani anaimba, nilimchukua video kidogo wakati anaimba hata sikujua kwa nini niliichukua Mungu anajua yote,” amesema.
Amesema Jumamosi iliyopita, alipokwenda mazoezi ya kwaya, alimuuliza Grayson iwapo amrudishe nyumbani kwao, akakataa akieleza mama yake atamtumia bodaboda imfuate.
Amesema Desemba 25, 2024 wakati wanasherekea sikukuu ya Krisimasi kanisani, walimtafuta mtoto huyo bila mafanikio na baada ya ibada walipata taarifa kuwa ameuawa.