KIWANGO cha JKT Tanzania katika kujilinda kinaweza kuwa mtihani mwingine wakati leo itakapokuwa mgeni wa Azam FC inayonolewa na kocha Rachid Taoussi ambaye alipata nafasi ya kuwaona maafande hao siku chache zilizopita wakila sahani moja na Simba katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara.
Azam inakutana na JKT Tanzania ikiwa na kumbukumbu ya kutoka suluhu katika mchezo wa duru la kwanza msimu huu uliokula kichwa cha aliyekuwa kocha wa Wanalambalamba, Youssouph Dabo aliyempisha Taoussi.
JKT imeonyesha kuwa timu ngumu kufungika katika michezo mitano iliyopita ya Ligi ambapo wameruhusu bao moja tu dhidi ya Simba tena kwa mkwaju wa penalti ya jioni iliyozua mjdala mtandaoni, jambo linalomfanya Taoussi kuingia uwanjani na mpango mbadala kuhakikisha anaifungua ngome hiyo kama inahitaji ushindi leo.
Timu hizo zinakutana kila moja ikiwa na rekodi tofauti kwa msimu huu japo zote zinabebwa na nyota wenye vipaji na uwezo mkubwa uwanjani, huku rekodi baina yao katika mechi tisa zilizopita za ligi tangu mwaka 2018 zinaibeba zaidi Azam, ikiwa imeshinda mara sita, huku tatu zikiisha kwa sare na JKT haijawahi kushinda.
Licha ya Azam kubebwa na rekodi, lakini kocha Taoussi aliyepata nafasi ya kuwaona maafande hao katika mchezo dhidi ya Simba kuna vitu amegundua na atatumia kama njia ya kuikabili JKT kwa hesabu kali.
“Nimeona uwezo wa JKT katika mchezo uliopita, ni timu yenye ngome imara, lakini Azam tunahitaji ushindi katika mchezo huu ili kuendelea kupigania malengo tuliyonayo. Tutatumia mbinu mbalimbali kuhakikisha tunapata matokeo mazuri,” alisema Taoussi, huku kocha wa JKT, Ahmed Ally akisema; “Azam ni timu kubwa na tunawaheshimu, lakini sisi tumejiandaa na tuna lengo la kupata matokeo mazuri. Haturuhusu makosa katika mchezo huu. Tumefanya maandalizi mazuri.”