Boni Yai ashikiliwa na polisi kwa saa 4, aachiwa kwa dhamana

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kanda ya Pwani, Boniface Jacob ‘Boni Yai’ ameshikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, kwa saa nne na kuachiwa kwa dhamana.

Wakili wake Hekima Mwasipu, ameliambia Mwananchi leo Ijumaa Desemba 27, 2024 kuwa Jacob ameshikiliwa kwa tuhuma za kuzuia upelelezi, baada ya kuhuisha laini zake za simu zinazoshikiliwa na jeshi hilo.

Alipotafutwa kuthibitisha hilo, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kipolisi Kinondoni (RCO), Davis Msangi hakuwa tayari kuzungumza akisema hana mamlaka ya kufanya hivyo.

“Mtafute Msemaji wa Jeshi la Polisi ndiye mwenye mamlaka ya kuzungumza kwa niaba ya Polisi, mimi si msemaji,” amesema.

Hata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Mtatiro Kitinkwi hakuwa tayari kuzungumzia.

Mwasipu amesema mteja wake huyo, leo alikwenda kuripoti katika Kituo cha Polisi cha Oystebay, baada ya jana Alhamisi kupelekewa wito uliomtaka afike hapo Ijumaa Desemba 27, 2024.

Mwananchi imefanikiwa kuona nakala ya wito huo uliosainiwa na Msangi, ukimtaka ‘Boni Yai’ kufika katika ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Kinondoni Desemba 27, kuanzia saa mbili kamili asubuhi.

“Alipofika kituoni aliambiwa ana tuhuma za kuvuruga upelelezi wa kesi yake kwa kuhuisha laini zake za simu, ambazo zilikamatwa awali na polisi. Simu zake zinashikiliwa na polisi, sasa yeye amekwenda kuhuisha laini na hivyo kudaiwa amezuia upelelezi,” amesema Mwasipu.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Related Posts