Duwasa yapunguza makali mgawo wa maji Dodoma

Dodoma. Takribani wakazi 800 wa Mtaa wa Mwangaza jijini Dodoma, waliokuwa wakilazimika kununua ndoo moja ya maji kwa Sh500, sasa wameondokana na changamoto hiyo baada ya Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (Duwasa) kukamilisha mradi wa maji katika eneo hilo.

Akizungumza leo Desemba 27, 2024, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mwangaza, John Ndawanya amesema mgawo wa maji ulitakiwa kuwa wa siku mbili kwa wiki lakini walikuwa hawayapati kabisa na hivyo kuwalazimu kuyanunua.

“Tulikuwa tunanua maji kwa Sh500 kwa ndoo, lakini mara baada ya kumalizika kwa mradi huu, sasa siku zote za mgawo tunapata maji kama kawaida,” amesema.

Mkazi wa Kisasa, Mwanne Othman amesema kutokana na ratiba ya mgawo wa maji kutofikiwa mara nyingi walikuwa wakilazimika kwenda maeneo mengine kufanyia baadhi ya shughuli za usafi.

Amesema kuchimbwa kwa kisima hicho kumepunguza changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa kwa kuwa hivi sasa wanapata maji kwa siku mbili kwa wiki.

“Mimi hapa na familia ya watu sita ili maji yatoshe kwa matumizi ya siku moja hayapungui ndoo 10, tena hapo umejibana sana. Tunashukuru sasa wakisema mgawo wetu ni Jumapili basi tunapata, tofauti na zamani hata wiki inapita bila kupata huyuma hiyo,” amesema Mwanne.

Akitembelea miradi ya maji ya Nzuguni, Kisasa, Nala kiwanda cha Aquaplast, Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew amesema Serikali inatambua changamoto ya maji katika Jiji la Dodoma lakini wameendelea na jitihada za kuzitatua.

Amesema wamevumbua eneo jingine la Kisasa ambalo wamechimba kisima ambacho kitawezesha kuzalisha lita milioni 2.48 kwa siku na kuondoa mgawo mkali kwenye maeneo ya nyumba 300 na baadhi ya maeneo ya Kisasa.

“Itaondoa mgawo mkali ambao siku tatu hadi nne zilikuwa zikipita bila kupata maji sasa changamoto hiyo imekwisha na mradi sasa uko asilimia 98,” amesema.

Amesema changamoto ya maji inasababishwa na uzalishaji wa maji kutoendana na mahitaji na hivyo Serikali imekuja na mikakati ya muda mfupi, wa kati na mrefu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Duwasa, Aron Joseph amesema lengo ni kuongeza uzalishaji wa maji kufikia lita milioni 90 kwa siku ili kupunguza adha ya mgawo wa maji katika jiji la Dodoma.

“Mradi wa Nzuguni na Kisasa tumefikia asilimia 98, Nala tumefikia asilimia 72 na tunategemea hadi Januari mwakani tutakuwa tumeikamilisha kwa asilimia 100,” amesema.

Kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, Jiji la Dodoma lina wakazi takribani 765,000 na kaya 214,000.

Mahitaji ya maji ya jiji hilo ni zaidi lita milioni 149 kwa siku lakini uzalishaji ni lita milioni 79 sawa na asilimia 52.

Related Posts

en English sw Swahili