Israel yashambulia uwanja wa ndege Yemen, bosi WHO anusurika

Jeshi la Israel linadaiwa kutelekeza mashambulizi ya anga katika uwanja wa ndege wa Sana’a na Bandari ya Ras Issa, eneo la Hodeidah nchini Yemen, yaliyoua watu watatu papo hapo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, watu wawili kati ya hao waliuawa katika mashambulizi hayo, kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sana’a nchini humo na mwingine aliuawa kwa kombora lilipopiga kwenye bandari ya Ras Issa iliyopo eneo la Hodeidah nchini humo.

Mashambulizi hayo ya Israel, pia, yalijeruhu watu 11 katika maeneo hayo.

Miongoni mwa walionusurika kuathiriwa na mashambulizi hayo ya Israel yaliyolenga uwanja wa ndege wa Sana’a ni pamoja na Kiongozi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tedros Adhanom Ghebreyesus ambaye alikuwa nchini Yemen wakati mashambulizi hayo ya anga.

Dakika chache baada ya mashambulizi hayo, Tedros aliandika kwenye ukurasa wa akaunti yake ya X (zamani Twitter): “Wakati tukisubiria kuingia kwenye ndege yetu kutokea Sana’a, saa kama mbili zilizopolita, ghafla uwanja ulikuwa chini ya milipuko ya makombora kutokea angani.

“Mmoja wa wahudumu wa ndege yetu walijeruhiwa na wawili tulielezwa kwamba wamefariki. Eneo la kuongozea ndege limeharibiwa vibaya na eneo la kusubiria ndege pia bila kusahau njia ya kurukia,”

Alisema wasafiri wenzake wakiwemo kutoka Umoja wa Mataifa na Shirika la Afya wako salama, na kwamba watahitajika kusubiria kwa muda ili kupata namna ya kuondoka nchini humo.

Aliongeza: “Tunatoa pole kwa familia ambazo zimeguswa kwa kuondokewa na wapendwa wao ama ndugu zao kujeruhiwa kutokana na mashambulizi hayo.”

Saa kadhaa baadaye, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alijitokeza hadharani na kudai kwamba jeshi la taifa hilo (IDF) litaendeleza mashambulizi yake nchini Yemen hadi pale lengo lao litakapotimia.

Katika kipande cha video alichokipakia kwenye akaunti yake ya YouTube na Telegram, Netanyahu alisema: Tuko makini kuhakikisha tunatokomeza tawi lingine la ugaidi linaloungwa mkono na Iran. Tutaendelea hadi tutakapokamilisha kazi yetu,”

Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu huyo, Netanyahu alikuwa akifuatilia mwenendo wa mashambulizi hayo, kutokea kilipo kituo cha anga cha kijeshi Jijini Tel Aviv akiwa na Waziri wake wa Ulinzi, Israel Katz, na Mkuu wa IDF, Luteni Generali, Herzi Halevi na Meja Generali, Tomer Bar.

Tayari leo asubuhi kundi la Wahouthi wa Yemen wamedai kutekeleza mashambulizi ya kulipa kisasi nchini Israel na mashambulizi hayo yamethibitishwa na msemaji wa wanamgambo wa Kihouthi, Yahya Saree.

Saree amesema makombora yao yamepenya na kupiga maeneo mbaalimbali ya Jiji la Tel Aviv nchini Israel, saa chache baada ya milipuko kusikika katikati ya jiji hilo.

Amesema mashambulizi yao, pia, yalilenga kupiga eneo la kijeshi lililoko karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Ben Gurion, jijini humo.

“Makombora yetu yamefanikiwa kufika tulipolenga, tunaendelea kufuatilia mwenendo wa madhara yaliyosababishwa na makombora yetu nchini mwao,” amesema Saree.

Wakati huo, Israel haijatoa kauli yoyote kuhusiana na madhara yaliyosababishwa na mashambulizi hayo ya Wahouthi wa Yemen.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaaani mashambulizi ya Israel nchini Yemen na kudai ni kuhatarisha usalama na amani ya dunia.

kupitia taarifa yake kwa Umma Iran imesema: “ Haya matendo ni wazi kwamba yanakiuka na kuvunja amani na utulivu wa kimataifa na ni uhalifu usiopingika, hatutakoma kuendelea kuwaunga mkono watu wasio na hatia wanaoonewa eneo la Palestina na Yemen,” amesema Msemaji wa Wizara hiyo, Esmail Baghaei.

Katika hatua nyingine, kundi la wanamgambo wa Hamas nchini Gaza, wamelaani mashambulizi hayo ya Israel katika maeneo yanayokaliwa na Wahouthi nchini Yemen.

Taarifa yao kwa Umma iliyonukuliwa na Reuters inasomeka: “Hamas inalaani vikali ugaidi unaotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya ndugu zetu wa Yemen ikiwemo kulenga uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sana’a na bandari ya Hodeidah,”

Tangu kuanza kwa uvamizi wake katika mataifa ya magharibi husuan ni Gaza Palestina Oktoba 7, 2023, Jeshi la Israel limesababisha vifo zaidi ya 48,000 huku zaidi ya 120,000 wakijeruhiwa.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika

Related Posts