Janga la wazazi, walezi kuwaamini bodaboda

Dar/Dodoma. Wakati likiripotiwa tukio la mtoto Graison Kanyenye (6), mkazi wa jijini Dodoma kuuawa akiwa ameachwa kwenye uangalizi wa dereva wa pikipiki maarufu bodaboda, angalizo limetolewa kwa familia kuhusu baadhi ya wazazi na walezi kuwa na imani kubwa kwa watoa huduma hao wa usafirishaji.

Mwananchi imebaini familia nyingi hususani mijini zimekuwa zikiwaamini bodaboda na kuwakabidhi jukumu la kuwasafirisha watoto kwenda na kurudi shuleni na hata kufanya shughuli zingine zinazowaweka karibu na familia zao.

Kwa mfano, Mwananchi limebaini bodaboda wamekuwa wakitumika kusafirisha mizigo, fedha na wakati mwingine kufanya ununuzi wa mahitaji mbalimbali ya nyumbani kwa niaba ya familia.

Imani ya wazazi kwa bodaboda

Mkazi wa Tabata, Mathias Masai amesema licha ya kuwa bado hajaanzisha familia lakini humtumia bodaboda kwa shughuli zake nyingi.

“Naishi mwenyewe ila nina mtoto, hatuko vizuri na mama yake, hivyo nikitaka kumuona namuagiza bodaboda anamleta mtoto na bahati nzuri hata huyo mama anamfahamu vizuri, hivyo hatuna wasiwasi. Ukiachana na hayo bodaboda wangu amekuwa kama ‘mshikaji’ (rafiki) vitu vyangu vingi anavijua na sijawahi kuchezwa na machale kumhusu yeye,” amesema.

Mkazi mwingine wa Tabata Mawezi ambaye hakutaka jina litajwe, amesema:“Mimi nina bodaboda wangu ambaye hata akienda nyumbani na kuwaambia awape chochote kwa madai kwamba nimemuagiza, hawatasita kufanya hivyo wala kujiuliza mara mbili watampa kwa sababu ni mtu aliyezoeleka na anaaminika ndani ya familia.’’

Maoni hayo hayatofautiani na yaliyotolewa na Eldiana Masanja, mkazi wa Mtoni Kijichi anayesema,  hakuwahi kufikiria mara mbili kuhusu imani ambayo familia yake imeijenga kwa bodaboda wanayemtumia.

“Sijawahi kuwaza kwamba kuna kitu chochote kibaya kinaweza kutokea kumhusisha bodaboda, ndiyo maana jukumu la kuwapeleka watoto shuleni na kuwarudisha nyumbani nimelikabidhi kwake kwa sababu namuamini,” amesema.

Anaongeza: “Hata nisipokuwapo yeye anakwenda nyumbani kuwachukua watoto na kuwarudisha, kwa sababu hiyo hata msichana wangu wa kazi ndiye anawasiliana naye ikitokea anahitaji msaada wowote wa nyumbani kwa haraka anamuita yeye anakwenda kumsaidia.’’

Wakati baadhi ya wanajamii wakijenga imani hiyo kwa bodaboda, tahadhari imetolewa kwamba inaweza kuleta madhara endapo bodaboda hao wataamua kuitumia vibaya.

Mwanasaikolojia Jacob Kilima amesema familia nyingi zinajenga imani kwa bodaboda ikiwa ni matokeo ya wanafamilia, hususani wazazi kutoa kipaumbele kwa shughuli za kiuchumi, hivyo kuhitaji msaada wa watu nje kusaidia familia zao ikiwemo watoa huduma hao wa usafiri.

“Changamoto iliyopo hapa wazazi hawana muda na watoto wao, ndiyo maana inakuwa rahisi kuwaacha kwa watu wengine wakiwemo bodaboda. Hawa mara nyingi tumekuwa tukiwatumia kwa ajili ya usafiri, hivyo kuna namna anajenga ukaribu na mtoto.

“Mzazi utaona kwamba wameshazoeana hivyo hakuna lolote baya linaweza kutokea, bila kujua huenda lisitokee baya la kumdhuru ila upo uwezekano mtoto akajenga ukaribu na imani zaidi na huyo na akakutoa kichwani mwake wewe mzazi wake,” amesema.

“Sasa sijui kama huwa tunapata muda wa kujiuliza tunawafahamu kwa kina hawa tunaowaachia watoto wetu, huwa wanazungumza nao nini, wanawajaza nini kwenye vichwa vyao. Siku hizi tatizo la afya ya akili ni kubwa unakuwa na uhakika gani kwamba bodaboda unayemuachia mtoto hana mambo yanayomsonga kichwani?” amehoji.

Kilimba amesema upo uwezekano wa bodaboda hao kutumiwa na watu wasio na nia njema, hivyo kuleta madhara kwa familia husika.

“Inawezekana ukawa na uadui na mtu, kwa bahati mbaya akajua kuhusu uwepo wa bodaboda ambaye anaaminika na familia yako, ni rahisi kwake kumtumia huyo kufanya kitu ambacho kinaweza kuleta madhara. Anaweza asimdhuru mtoto lakini kama anaweza kuja nyumbani kwake na akaaminika basi kama atarubuniwa kwa fedha, upo uwezekano wa kufanya chochote,” amesema.

Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Watoto, Sebastian Kitiku amesema ulinzi na usalama wa watoto ni jukumu linalopaswa kusimamiwa na wazazi na si mtu mwingine ambaye hana uhusiano na mtoto husika.

“Tunaendelea kusisitiza kwamba mzazi ndiye mtu wa kwanza wa kuhakikisha ulinzi na usalama wa mtoto wake, hata ikitokea amemuacha mtoto kwa mtu mwingine ni lazima ufanye hivyo baada ya kumchunguza na kujiaminisha kwamba ni salama.

“Katika utafiti tuliowahi kufanya tulibaini asilimia 60 ya matukio ya ukatili dhidi ya watoto yanatokea nyumbani na yanafanywa na watu wanaoaminika ndani ya familia, ikiwemo hao bodaboda, hivyo ni lazima tuwe makini na watu tunaowaweka karibu na watoto wetu,” amesema.

Kuhusu waendesha bodaboda kuachiwa jukumu la malezi na uangalizi wa watoto, Kitiku amesema changamoto hiyo inafahamika na Wizara yake yenye dhamana na watoto inaipiga vita.

“Kwanza si ruhusa kwa mtoto kupanda bodaboda, haya mambo ya kuzitumia kama usafiri wa kuwasafirishia hatukubaliani nalo na hili linasimamiwa pia na Jeshi la Polisi. Hata hivyo, hatuwezi kufanikiwa kama wazazi hawatatoa ushirikiano na kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha usalama wa mtoto.

“Kwenye suala la malezi kuna mambo matatu ambayo mzazi anapaswa kuzingatia, kwanza kumpatia mtoto mahitaji muhimu, ulinzi na usalama na pia kutenga muda wa kukaa naye na kumsimamia. Watoto wanahitaji uangalizi wa karibu wa mzazi au wazazi siyo mtu yeyote yule,” amesema.

Alivyoishi mtoto aliyeuawa

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wazazi au walezi kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto na kukumbuka kuwa, tafiti zinaonyesha ndugu jamaa wa karibu ndiyo wanaoongoza kuwafanyia watoto ukatili ikiwa ni pamoja na ubakaji, ulawiti na hata mauaji.

“Nina imani vyombo vya kusimamia sheria vinafuatilia jambo hilo kwa kadiri iwezekanavyo ili wahusika waweze kubainika na haki ya mtoto iweze kupatikana na kuwa funzo kwa wengine wanaofanya ukatili kwa watoto.

Mwalimu wa Kwaya ya Shekina iliyoko chini ya Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Area D jijini Dodoma, Amani Bale amesimulia jinsi mtoto Grason Kanyenye  aliyeuawa, alivyoshiriki uimbaji.

Graison, mtoto wa mfanyabiashara Zainab Shaban, alifariki dunia usiku wa kuamkia Desemba 25, 2024 nyumbani kwa rafiki yake ambaye ni Ofisa Uvuvi Mtera, Hamis Mpeta, mkazi wa Ilazo Extension jijini Dodoma.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi alisema Desemba 25, 2025 saa 1:00 asubuhi, Mpeta akiwa na mama wa mtoto, Zainab waliporejea kutoka matembezini walibaini ameuawa.

“Walikuta mtoto akiwa ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na shingoni amekatwa na kitu chenye nja kali. Katika tukio hilo, mama alimwacha mtoto huyo chini ya dereva bodaboda anayejulikana kwa jina la Kelvin Gilbert,” alisema.

Alisema walimwacha mtoto na Gilbert saa 6:00 usiku nyumbani kwa Mpeta na waliporejea walikuta ameuawa na dereva hakuwepo.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Desemba 27, 2024, Bale amesema Grayson alipendwa na waumini, walimu na wenzake katika kanisa hilo.

Amesema upendo ulitokana na utulivu wake na hata alipochokozwa na wenzake, alikwenda kutoa malalamiko kwa walimu.

“Mwalimu ananichokoza, mwalimu yule anachezea kinanda (wakati si muda wa kupiga kinanda kwa watoto). Alikuwa mtoto mzuri na kwa umri aliokuwa nao, angekuwa mwimbaji mzuri baadaye,” amesema.

Bale amesema alikuwa na uwezo mkubwa wa kushika kile anachofundishwa.

Amesema Jumamosi ya mwisho (Desemba 21, 2024) alifika kanisani kufanya mazoezi kwa ajili ya kuimba kwenye ibada ya Jumapili kanisani hapo.

Anasema alimruhusu kushika kipaza sauti kati ya watoto takribani 150 waliopo kwenye kwaya hiyo na alifanya hivyo baada ya kuona ameshika vizuri aliyomfundisha.

Amesema katika wimbo walikuwa wakipishana kuimba na kuitikia, kati ya wavulana wawili na wasichana wawili.

“Kila nikikumbuka machozi yananilenga, hasa nikikumbuka kuwa alipofika Jumapili kanisani, alijua ataimba, hivyo badala ya kusubiri apewe kipaza sauti alienda mwenyewe kukitafuta, kisha kushuka upande wa kushoto wa madhabahu,” amesema.

Bale amewashauri wazazi kuwapeleka watoto kanisani wanapotakiwa kufanya hivyo, ili wajifunze maadili yanayompendeza Mungu, ili waweze kumcha Mungu katika maisha yao.

“Jitihada za kuwapeleka shule za kawaida zimekuwa ni kubwa kuliko wanavyowaleta kwa Mungu, kuwafundisha jinsi ya kuomba, kuwasaidia wengine na kuwaambia wengine habari za Mungu. Wakijisahau hapo watoto watakuwa tofauti na matarajio yao kwa sababu kila kitu huandaliwa,” amesema.

Amesema hakumbuki ni lini Graison alijiunga na kwaya hiyo, bali alianza kuwafundisha yeye na wenzake zaidi ya 150 tangu mwaka jana.

Bale amesema Graison alikuwa akipelekwa kanisani na dereva bodaboda kwa ajili ya mazoezi Jumamosi ambayo hufanyika kuanzia saa 3:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana na pia kwenye ibada kila Jumapili.

“Bado tuna machungu, tutamkumbuka kwa muda mrefu. Najaribu kutafakari kesho (Jumamosi Desemba 28, 2024) kama tutaweza kufanya mazoezi, nahisi tutaaanza kulia tu tukimkumbuka Graison,” amesema.

Rehema Pangasi, mke wa mchungaji wa Kanisa TAG la Area D, amesema mtoto huyo alikuwa mshirika wa kanisa lao na alikuwa mwimbaji wa kwaya ya Shekina.

“Hata Jumamosi hii (Desemba 21, 2024) alikuwa kanisani kwa ajili ya mazoezi ya kwaya. Jumapili alikuwa kanisani anaimba, nilimchukua video kidogo wakati anaimba hata sikujua kwa nini niliichukua Mungu anajua yote,” amesema.

Amesema Jumamosi iliyopita, alipokwenda mazoezi ya kwaya, alimuuliza Graison iwapo amrudishe nyumbani kwao, akakataa akieleza mama yake atamtumia bodaboda imfuate.

Amesema Desemba 25, 2024 wakati wanasherekea sikukuu ya Krisimasi kanisani, walimtafuta mtoto huyo bila mafanikio na baada ya ibada walipata taarifa kuwa ameuawa.

Tayari Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, linawashikilia Gilbert na mtu mwingine ambaye jina lake halijatajwa kwa sababu za kiuchunguzi.

Mtoto huyo alizikwa jana Desemba 26, 2024, katika makaburi ya Kilimo Kwanza jijini Dodoma.

Related Posts