Dar es Salaam. Komanya Erick Kitwala, Luhaga Mpina na Dk Yahya Nawanda ni miongoni mwa majina ya watu maarufu walioingia katika kumbukumbu za Mahakama kwa mwaka 2024, kutokana na kesi zilizowahusisha au kuamuiwa mwaka huu.
Hizi ni kesi zilizowahusisha wadaawa (kwa zile za madai) au washtakiwa (kesi za jinai ambao ni watu maarufu katika jamii wakiwemo wanasiasa, maofisa au watumishi wa umma au Serikali, wafanyabiashara.
Uamuzi wa Rais kumstaafisha DC aliyemtengua
Huu ni uamuzi wa Mahakama katika shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama lililofunguliwa na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya, Komanya Erick Kitwala akipinga uamuzi wa Rais kumstaafisha utumishi wa umma kwa madai ya maslahi ya umma.
Kitwala aliteuliwa na aliyekuwa Rais wa awamu ya tano, hayati John Magufuli, kuwa Mkuu wa Wilaya ya Tabora Mjini Julai 27, 2018. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa akifanya kazi PSSSF.
Juni 19, 2021 Rais Samia alitengua uteuzi wake huo, na baada ya kutenguliwa alimwandikia barua Katibu Mkuu Utumishi, akiomba amrejeshe katika ajira yake ya awali, PSSF.
Hata hivyo, alipokea barua ya Katibu Mkuu Kiongozi ya Agosti 15, 2022, iliyomfahamisha kuwa Rais amemstaafisha kwa maslahi ya umma.
Kitwala hakukubaliana na uamuzi, hivyo alifungua shauri la maombi ya mapitio ya Mahakama kupinga uamuzi huo wa Rais, akidai kuwa amekwenda nje ya mamlaka yake kisheria dhidi ya kanuni ya haki asili.
Aliiomba imuamuru Katibu Mkuu Utumishi na bodi ya wadhamini wa PSSSF wamrejeshe katika ajira yake ya awali, kulipwa madeni ya mishahara yake na mafao mengine kuanzia Juni 28, 2021 mpaka tarehe ya kurejeshwa katika ajira yake.
Februari 8, Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Elizabeth Mkwizu, ilitengua uamuzo huo wa Rais baada ya kukubaliana na hoja za Kitwala kuwa Rais hakutoa sababu hizo za kumstaafisha kwa maslahi ya umma.
Jaji Mkwizu alisema kuwa uamuzi huo wa Rais si sahihi kwani mtu hawezi kustaafishwa utumishi wa umma kwa maneno tu kuwa ni kwa maslahi ya umma, bila kueleza sababu kwa kuwa maslahi ya umma ni suala pana.
Hivyo Jaji Mkwizu alimwelekeza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kumrejeshea katika utumishi wake na kumlipa stahiki zake
Kesi za mbunge Mpina dhidi ya Spika na dhidi ya mawaziri
Luhaga Mpina ni mbunge machachari wa jimbo la Kisesa jijini Mwanza, ambaye amekuwa akiibua hoja nzito zaidi bungeni na hata nje ya bunge, ambazo zimekuwa zikionekana kuwa mwiba mkali kwa watumishi na viongozi wa Serikali hususan mawaziri.
Mwaka 2024 Mpina ambaye amewahi kuwa Naibu na kisha Waziri katika Serikali ya awamu ya tano ameingia katika kumbukumbu za Mahakama baada ya kufungua kesi mbili za kikatiba.
Kesi moja alifungua dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania, Waziri wa Kilimo na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Katika kesi hiyo alikuwa akipinga adhabu ya Bunge kumsimamisha kuhudhuria vikao 15 vya Bunge kwa tuhuma za kusema uongo dhidi ya Waziri wa Kilimo na kudharau mamlaka ya Bunge.
Juni 4, 2024, Mpina alimtuhumu Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kulidanganya Bunge kuhusu utoaji wa vibali uagizaji sukari nje ya nchi.
Spika Dk Tulia Ackson alimtaka awasilishe ushahidi na akaipa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka jukumu la kupitia ushahidi huo na shtaka la Mpina kudharau mamlaka ya Bunge kwa kupeleka ushahidi huo kwenye vyombo vya habari.
Kamati hiyo iliwasilisha ripoti yake Juni 24, 2024, ikieleza kuwa tuhuma hizo hazikuwa na ukweli, ndipo Bunge chini ya Spika Tulia likampa adhabu hiyo.
Baadaye Mpina akafungua kesi hiyo ya kikatiba Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, akipinga utaratibu uliotumika kumpa adhabu hiyo, akidai kuwa hakupewa haki ya kusikilizwa.
Pamoja na nafuu nyingine, Mpina alikuwa anaiomba Mahakama hiyo itengue uamuzi huo na iamuru alipwe stahiki zake kwa kipindi chote atakachokuwa nje ya Bunge.
Mahakama katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Awamu Mbagwa Oktoba 24, ilibariki uamuzi wa Bunge, baada ya kukubaliana na hoja ya pingamizi lililowekwa na Serikali, kuwa kuwa haina mamlaka ya kuingilia uamuzi wa Bunge.
Jaji Mbagwa alikubaliana na hoja za Serikali kuwa Bunge chini ya kanuni zake za kudumu lina mamlaka ya kumsimamisha mbunge, hivyo lilifanya kile kilicho ndani ya mamlaka yake.
Kesi ya ubakaji dhidi ya aliyekuwa RC Simiyu
Juni 11, 2024, Mwananchi liliripoti taarifa za Mkuu wa Mkoa mmojawapo wa Kanda ya Ziwa kutuhimiwa kumlawiti mwanafunzi wa kike wa chuo kikuu kimojawapo jijini Mwanza.
Siku hiyo hiyo Rais Samia Suluhi Hassan alitengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dk Yahya Nawanda na Juni 13, Dk Nawanda alitiwa mbaroni na Jeshi la Polisi na kumhoji kuhusiana na tuhuma hizo.
Baada ya hapo mambo yalikuwa kimya hali iliyoibua mjadala katika mitandao ya kijamii, huku wachangiaji wakitaka mtuhumiwa huyo achukukiwe hatua za kisheria.
Julai 5 binti huyo Tusiime Ngemela (21) mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Augustine (SAUT) Mwanza, mwenyewe aliyevunja ukimya na kuzungumzia na vyombo vya habari kuhusu tukio hilo lilivyotokea.
Alikiri kuwa walikuwa na uhusiano, lakini siku hiyo mtuhumiwa alimlazimisha kumwingilia kinyume na maumbile, na akamuomba Rais Samia aingilie kati.
Julai 9, Dk Nawanda alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, akikabiliwa kesi ya jinai namba 1883/2024.
Alisomewa shtaka moja na kumwingilia kinyume na maumbile binti huyo, akidaiwa kutenda kosa hilo Juni 2, 2024.
Hata hivyo Novemba 29, 2024, mahakama hiyo katika hukumu yake iliyotolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi, Erick Marley ilimwachia huru Dk Nawanda, baada ya kumuona hana hatia.
Hakimu Marley alisema upande wa mashtaka hakuweza kuthibitisha shtaka hilo bila kuacha mashaka, kutokana na kukinzana kwa ushahidi, ukiwemo ushahidi wa mwathirika (binti huyo) na wa mama yake mzazi.
Alibainisha kuwa wakati mwathirika akisema kuwa mshtakiwa alimpatia mama yake fedha ili asimfungulie kesi, mama wa mwathirika mwenyewe alikana kuwa hakuwahi kupokea fedha kutoka kwa mshtakiwa ili asifungue kesi hiyo.
Alisema kuwa ingawa daktari aliyemfanyia uchunguzi alidai kuwa alibaini michubuko sehemu ya njia ya haja kubwa hali iliyoonesha kuwa alikuwa ameingiliwa na kitu butu lakini alikiri kuwa hakujua kuwa aliingiliwa na nini.
Hakimu Marley alisema kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuwasilisha ushahidi wa kisayansi hususan vinasaba (DNA) kwenye sampuli zilizochukuliwa sehemu ya haja kubwa ya mwathirika huyo.
Hivyo alisema kuwa ushahidi na vielelezo vilivyowasilishwa havikujitosheleza kumtia hatiani mshtakiwa na akamuachilia huru.