Kilio cha maji, ZRA yajitosa kutatua changamoto

Unguja. Wakati wananchi wakieleza changamoto wanazopitia kutokana na kukosa huduma ya majisafi na salama, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imesema itahakikisha inaendelea kufikisha huduma zote muhimu, hususani maeneo ya pembezoni mwa nchi.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya Salum amesema hayo leo Desemba 27, 2024 alipokabidhi kisima kilichojengwa na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Donge Kiungani na vitimwendo kwa watoto wenye mahitaji maalumu wa Kijiji cha Donge Pwani, Mkoa wa Kaskazini Unguja na watoto wenye mahitaji maalumu wa Kijiji cha Paje, Mkoa wa Kusini Unguja.

Dk Saada amewataka wananchi kulipa kodi na kudai risiti za kielektroniki,  ili kuiwezesha Serikali kukusanya kodi nyingi kwa ajili ya maendeleo.

“Maendeleo yote ambayo yanafanyika hivi sasa yanatokana na kodi zinazotokana na wananchi wenyewe,” amesema.

Amewasisitiza kuhakikisha wanashirikiana na Serikali kudai risiti za kielektroniki na kuiwezesha Serikali kufanya mambo makubwa zaidi.

Amesema fedhan hizo zinasaidia kuleta maendeleo kwa nchi kwani barabara, maji, umeme na miundombinu mingine inayoonekana ni kodi ya mwananchi aliyolipa anapofanya ununuzi.

Waziri amesema Serikali inafanya jitihada za usambazaji wa majisafi na salama, lakini yapo maeneo ya kilimo hayafikiwi na miundombinu hiyo, hivyo wameona ipo haja ya kurejesha jambo hilo kwa wananchi wa kijiji hicho.

Ameahidi ZRA itaangalia namna ya kuendelea kusaidia maeneo mengine ambayo yanahitaji miundombinu hiyo.

Saada amewasisitiza wafanyabiashara kuwapa risiti wananchi ili kuwa waaminifu na kuona kodi hiyo inafika serikalini.

Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, akiwemo Ashura Khamis Makame licha ya kushukuru kwa hatua hizo, ameomba huduma ziendelee kusogezwa karibu zaidi.

“Alhamdulilah si haba tutapunguza mwendo kutembea kutafuta maji, lakini tunaomba visima viwe vingi ili kutupunguzia adha hii ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo katika vijiji vingine,” amesema.

Khamis Abdul Nadir, mkazi wa eneo hilo amesema bado wanakabiliwa na changamoto za huduma hasusani za maji, hivyo wanaomba kusogozewa zaidi kutoka kwenye Mamlaka ya Maji Zanzibar (Zawa).

Mwenyekiti wa Bodi ya ZRA, Profesa Hamed Rashid Hikmany, amewasisitiza wananchi kuendelea kuisaidia Serikali kupata mapato ili kuiwezesha kufanya maendeleo kupitia kodi zinazokusanywa.

Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohammed amesema mamlaka hiyo imepewa jukumu la kumsaidia Rais kukusanya mapato ambayo yanatoka kwa wananchi.

Amesema kodi hiyo inakwenda moja kwa moja katika maendeleo ya Taifa, hivyo ni vyema kudai risiti za kielektroniki ili nchi iendelee kupiga hatua za kimaendeleo.

Akizungumzia mwezi wa shukran na furaha kwa walipakodi, amesema ZRA imejipanga kila Desemba kutoa shukran kwa walipakodi, ikiwemo kufikisha elimu kwa wananchi na kurudisha kidogo kwao.

Amesema wameamua katika kijiji hicho njia bora ya kurejesha shukran, ni kuweka kisima ambacho kitatumika na wanakijiji.

Amebainisha kuwa, hayo yote ni kurejesha shukran kwao kama walipakodi, hivyo amewaomba kuendelea kushirikiana na kumuunga mkono Rais ili aendelee kuleta maendeleo kwa Wazanzibari.

“Haipendezi kusherehekea tu bali ni kumsaidia kudai risiti za kielektroniki kupata mapato mengi ili aweze kufanya makubwa zaidi, hasa mnapokwenda kufanya ununuzi,” amesema.

Mwakilishi wa Jimbo la Donge, Dk Khalid Salum Mohammed amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali kupeleka maendeleo kwa wananchi.

Amesema Donge imepata shule ya msingi ya ghorofa, kumefanyika ukarabati wa kituo cha afya, kumewekwa minara ya mawasiliano na ujenzi wa barabara.

Amesema hayo yamefanywa na Serikali katika kipindi cha miaka minne.

Amesema wananchi wafahamu kilomita moja ya barabara ya lami inagharimu Sh1.5 bilioni lakini Rais Dk Hussein Mwinyi ameamua kuondoa usumbufu wa wananchi katika maeneo, hasa vijijini kwa kujenga barabara nyingi za lami.

“Serikali inapojenga barabara siyo fedha za wafadhili bali ni fedha zinazokusanywa na Serikali kupitia kwa wananchi pale wanapofanya ununuzi kwa kudai risiti za kielektroniki,” amesema.

Amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanadai risiti za kielektroniki wanapofanya ununuzi na kukataa risiti za mkono, ili kuiwezesha Serikali kuendelea kuleta maendeleo.

Kuhusu kisima amesema bado kijiji hicho kina changamoto ya upatikanaji wa maji, hivyo kama fursa ipo basi waendelee kuwasaidia.

Ameipongeza ZRA akiahidi kuweka bomba na pampu ili kisima hicho kiwanufaishe watu wengi zaidi.

Related Posts