Kwa nini uepuke vyakula vya wanga

Vyakula vya wanga ni rafiki kwa jamii nyingi za Kitanzania zenye maisha ya chini na kati, ni mara chache kuvikosa katika akiba ya chakula majumbani mwao.

Kwa tafiti ya kuona tu, walio wengi asubuhi, mchana na jioni milo mikuu yao huwa haikosi vyakula vya wanga.

Mfano wa vyakula vya wanga katika jamii yetu ni pamoja na unga wa mahindi (sembe au dona), mchele, ngano, viazi mbatata, wengi hutumia kwa chipsi na vitamu, ndizi, magimbi na mtama.

Sukari ya mezani ya kiwandani hutumika kama nyongeza katika vyakula na vinywaji.

Katika uainishaji wa vyakula vya wanga, kuna wanga rahisi kama vile matunda, maziwa na bidhaa za viwandani kama soda na juisi, wakati wanga tata ni viazi, unga wa mahindi na ngano.

Wanga rahisi hufyonzwa kwa haraka zaidi na kupandisha haraka kiwango cha sukari, ukilinganisha wanga tata ambayo huchukua muda mrefu kusagwa mpaka kupandisha sukari.

Vyakula hivi vinapoliwa mwili huvichakata na kuwa sukari ijulikanayo kitabibu kama glucose, ndiyo inayotumika na seli kama chanzo cha nishati ya mwili kwa ajili ya kazi mbalimbali.

Matokeo ya ulaji holela wa vyakula hutofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Chakula unachokula kitakuwa salama kwako kama tu utakitumia kwa kiwango sahihi, kwa kuzingatia kanuni za afya.

Mwili unahitaji vyakula vya wanga kwa ajili ya kupata virutubisho na nyuzinyuzi ambavyo ndivyo huwezesha mwili kupata mambo kadhaa, ikiwamo nguvu na joto.

Wanaotakiwa kuwa na tahadhari na ulaji holela wa vyakula vya wanga ni wenye umri zaidi ya miaka 40, wanene au wenye uzito uliokithiri na wasiofanya kazi ngumu au kazi za maofisini za kukaa.

Mfumo wa usagaji chakula huvunjavunja vyakula vya wanga na zao lake huwa ni sukari ambayo ndiyo inakwenda katika damu, kisha kuathiri kiwango chake.

Lakini mwili hutumia nishati yake kwa ajili ya matumizi hayo kuendana na hitaji la mwili wako, kama kitabaki na kurundikana huweza kuhifadhiwa kwa kubadilisha kuwa mafuta kwa ajili ya baadaye.

Kuna tofauti kati ya mahitaji ya mwili ya vyakula kati ya mtu anayefanya kazi za ofisini na yule ambaye anafanya kazi ngumu, ikiwamo kuli, askari mpiganaji wa nchi kavu, mwanamichezo na mtembeza bidhaa.

Katika makundi hayo kuna tofauti kubwa katika matumizi ya nishati ya mwili. Wanaofanya kazi zinazoushughulisha mwili zaidi wanatumia kiasi kikubwa mpaka ile akiba ya nishati.

Wa ofisini anapaswa kutumia kiasi kidogo na pengine kila kiasi kilichorundikana kinaendelea kuwepo bila kutumiwa.

Kwa mifano hii, kila unachokula kiendane na mahitaji ya mwili, vinginevyo kinaweza kuwa hatari kiafya.

Inahitajika kuepuka ulaji holela wa wanga. Inashauriwa mlo mkuu sahani ya mduara iwe na robo ya wanga ikibidi iwe ile isiyokobolewa kama dona, mikate ya ata au mchele wa kahawia.

Epuka kutumia kiholela sukari rahisi zote, ikiwamo vinywaji na vyakula vyenye nyongeza za sukari ya mezani.

Shughulisha mwili kwa kazi ngumu na fanya mazoezi mepesi angalau dakika 30 hadi 60 kwa siku katika siku 5 za wiki. Waone wataalamu lishe kwa ushauri zaidi.

Related Posts