MSHAMBULIAJI wa Coastal Union, Maabad Maabad ameziingiza vitani Tabora United na klabu anayoichezea sasa aliyomaliza nayo mkataba, baada ya kila upande kutaka kupata huduma yake, Wagosi wakitaka kumbakisha na Tabora kumbeba ili kwenda kuboresha safu ya ushambuliji ya kikosi hicho cha Nyuki wa Tabora.
Maabad anaitumikia Coastal kwa msimu wa tatu sasa katika Ligi Kuu kuanzia 2022 hadi sasa mkataba alionao ukidaiwa kumalizika, akifunga jumla ya mabao 11 katika misimu hiyo, wa kwanza akitupia manne sawa na msimu huu, huku msimu uliopita akifunga matatu tu.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezinasa ni kwamba, Maabad yuko kwenye hatua za mwisho kumalizana na Tabora Utd, japo Coastal inapambana ili kumuongeza mkataba mpya kabla ya dirisha dogo kufungwa katikati ya mwezi ujao.
“Wachezaji wengi wanaoichezea Coastal wanaamini, wakitoka hapo watapata timu kama Simba, Yanga na Azam ila ligi sasa imekuwa ngumu, lolote linaweza kutokea. Muda wowote Maabad anaweza kutua Tabora United kwani hana mkataba, alikuwa amebakiza miezi sita tu na ndio imemalizika mzunguko wa kwanza,” kilisema chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Coastal.
Kwa sasa Tabora iko katika hali nzuri katika ligi kulinganisha na Coastal kwani rekodi zinaonyesha inashikilia nafasi ya tano wakati Wagosi wakiwa ni wa 10 kila moja ikicheza mechi 15 hadi sasa.
Awali, Mwanaspoti liliwajulisha kwamba kocha wa timu hiyo, Juma Mwambusi amezungumza na mabosi wa klabu hiyo mapema na kuwapa mipango yake kabla ya mzunguko wa pili haujaanza.
Ilielezwa kocha huyo aliweka wazi anahitaji mshambuliaji mmoja, viungo watatu, beki na kipa ili kuongeza nguvu zaidi katika kikosi hicho.
“Katika ripoti ya kocha anataka mashine mpya sita, mshambuliaji, beki na kipa sambamba na viungo watatu, ili kuiongezea nguvu kwa ajili ya mechi za duru la pili ambalo ni la lalasalama kila moja ikipambana kumaliza vyema,” chanzo hicho kilisisitiza ripoti ya Mwambusi.