Mashine mpya zasaidia kupunguza gharama ya dialisisi

Dar es Salaam. Ili kukabiliana na gharama kubwa ya huduma ya dialisisi kwa wagonjwa wa figo, Serikali imeingiza nchini mashine mpya aina ya SWS 6000 ambazo zimewezesha zishuke kutoka Sh250,000 mpaka Sh150,000.

Mashine hizo moja ina thamani ya Sh31.76 milioni ambazo tayari zimefungwa katika hospitali za rufaa za mikoa. Zina uwezo wa kutoa huduma zaidi ya moja mgonjwa anapokua kwenye mashine na kutobagua vitendanishi.

Akizungumzia utendaji kazi wa mashine hizo leo Ijumaa, Desemba 27, 2024, muuguzi kiongozi wa kitengo cha kusafisha damu kwa wagonjwa wa figo katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Temeke, Abubakari Ali amesema mashine hizo zimeboresha huduma.

Amesema awali mgonjwa angeweza kupata changamoto kwenye mashine na ili kuitatua wangelazimika kusitisha huduma kwanza, lakini sasa utoaji huduma umeimarika.

“Mgonjwa akipata changamoto kama kushuka kwa presha, kupanda au sukari kushuka akiwa kwenye mashine ni rahisi kumhudumia, sifa ya kwanza ina ‘double pump’ inasaidia unapompa huduma unaendelea kutatua changamoto yake.

“Mashine za mwanzo zilibagua, baadhi ya vitendanishi ilikuwa kwenye kuiandaa inaleta changamoto, hizi hazibagui vitendanishi na katika kuiandaa mashine kwa ajili ya mgonjwa mwingine, unaiandaa kwa muda mfupi tofauti na za mwanzo,” amesema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani katika hospitali hiyo, Emmanuel Lazaro amesema mapokezi na ufanisi wa mashine hizo kwa kipindi cha miezi sita umesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza msongamano kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Amesema hospitali hiyo iliyoanza kutoa huduma Juni 14, 2024, ilipatiwa mashine kutoka Bohari ya Dawa (MSD) na tangu wameanza kuzitumia hazijawahi kuwa na hitilafu.

“Kuna mashine ambazo mgonjwa akiwa anazitumia zinaweza kuleta hitilafu zikasimama ghafla, lakini hii unaanza mwanzo mpaka mwisho bila kuzimika. Uzuri ni kwamba, zinatumia vitendanishi vya aina yoyote, hivyo imesaidia kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa.

“Tuna uhuru wa kuchukua vitendanishi popote na mashine zinaweza kufanya kazi, hivyo tunaweza kuchukua vile vya gharama ya chini kabisa na huduma ikawa bado bora. Hii imesaidia kutupunguzia gharama za uendeshaji na kupunguza mizunguko kwa wagonjwa, hivyo tunafanya kwa gharama ya chini ukilinganisha na sehemu zingine,” amesema.

Lazaro amesema kwa sasa wana uwezo wa kuhudumia mpaka wagonjwa 36 kwa siku na kuhudumia wagonjwa 10 kwa mzunguko mmoja ukilinganisha na awali walitumia siku nzima kuhudumia wagonjwa 10 pekee.

Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Joseph Kimaro ameishukuru Serikali kwa maboresho ya sekta ya afya hususani eneo la huduma, dawa na vifaatiba.

Amesema kutokana na urahisi wa matumizi ya mashine hizo, kitengo kimeingiza Sh60 milioni licha ya kwamba wapo ambao hawalipii huduma bali hospitali inachukua jukumu hilo.

“Mfumo wa mashine hizi uko huru, MSD akishatuuzia hatubani wapi tutapata vifaa vyote vya kuhudumia mgonjwa tunapata kwa washitiri, MSD wenyewe na nyakati zingine wasambazaji wengine kwa kuendesha mashine kutoka kwa washitiri ambao bei zao ni rahisi,” amesema.

Amesema mfumo huo ni rahisi kuendesha na hauna changamoto za kulumbana na msambazaji, kwani mpaka sasa wameshatoa jumla ya mizunguko 247 kwa wagonjwa ambao ilibidi wapange foleni kusubiri huduma hiyo Muhimbili.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema wamejipanga kuhudumia mahitaji ya mashine saidizi na vitendanishi vya mashine za dialisisi kwa wagonjwa wa figo yatakayowasilishwa na vituo vya kutolea huduma za afya.

Ametoa rai kwa vituo vya kutolea huduma kukamilisha maandalizi ya eneo la dialisisi ili kuanza kupokea mashine hizo zinazoendelea kuleta ahueni katika gharama za tiba ukozi.

“Tuna mkakati wa muda mfupi tayari kuna mashine tutasambaza kwenye hospitali saba za mikoa na UDOM (Chuo Kikuu cha Dodoma) tayari wapo kwenye mpango wetu, wana mashine lakini tunakwenda kuweka hizi mpya kuondoa zile za zamani.

“Baada ya hapo tutaangalia walio tayari kwa kuwekewa mashine mpya kwa sababu dialisisi ni huduma muhimu inayohitaji uangalizi kwa kukidhi vigezo maalumu kuanzia chumba chenyewe kiweje, mfumo wa maji, umeme, vitanda vinavyotumika kufanya hiyo huduma,” amesema.

Amesema katika mwaka wa fedha 2024/2025 mashine 113 zimeshapokewa MSD na  72 zimesambazwa kwa hospitali 14 nchini ikiwa ni nyongeza ya mashine 137 zilizosambazwa awali. Gharama ya mashine moja ni Sh31.76 milioni.

Related Posts