NYOTA wa Mashujaa Kigoma, Crispin Ngushi, amefunguka jinsi ushindani wa namba aliokumbana nao Yanga ulivyomjenga na kuwa alivyo sasa kwa Wana Mapigo na Mwendo.
Ngushi, ambaye sasa ni mmoja wa wachezaji muhimu wa Mashujaa akiwa na mabao mawili katika ligi, amesema kuwa miaka aliyokuwa akicheza Yanga ilimfundisha kuwa kila nafasi katika timu kubwa inahitaji juhudi na kujiweka tayari, huku ushindani wa namba ukilazimisha kila mchezaji kujiendeleza zaidi ili kuwa na nafasi.
Akiwa na Yanga, Ngushi alikubaliana na ukweli kwamba kushindana na wachezaji wa kiwango cha juu ilikuwa changamoto na kukubali kutolewa kwa mkopo Coastal Union kabla ya kusajiliwa Mashujaa anayoitumikia sasa.
“Katika klabu kubwa kama Yanga, ushindani wa namba ni mkubwa. Hata unapokuwa na uwezo, bado inabidi ujitume zaidi kila wakati ili kuepuka kuwa nje ya kikosi cha kwanza,” alisema Ngushi na kuongeza;
“Nilijua kuwa nilihitaji kuwa na programu ya binafsi, kujiwekea malengo na kujifua zaidi ili niweze kuboresha kiwango changu. Nilijua kuwa ili niweze kufika mbali, ilibidi niwe na mpango maalum wa mazoezi, chakula bora na kuwa na umakini katika kila jambo. Hii ilinisaidia na nakumbuka kuna wakati nilianza kupata nafasi kabla ya kuondoka.”
Hata hivyo, Ngushi alisema kuwa maisha yake Mashujaa ni tofauti na Yanga, na anajivunia hatua aliyofikia. “Sasa niko Mashujaa, na ninajiona kuwa ni mchezaji mwenye hatua mpya katika maisha yangu ya soka. Hapa nimepata nafasi ya kuonyesha kile nilichojifunza, na timu inategemea mchango wangu.”
“Ninajivunia kuwa sehemu ya Mashujaa na najiona kuwa ni hatua nyingine muhimu katika safari yangu ya soka,” alisema Ngushi.