Sababu watoto wachanga kupata manjano

Geita. Manjano ni zao litokanalo na kuvunjwavunjwa kwa seli nyekundu za damu ambazo hutoa zao la mwisho ambalo ni bilrubin inayotengeneza rangi ya njano mwilini.

Kazi mojawapo ya bilrubin ni kuhifadhiwa kwenye kifuko cha nyongo na kutengeneza nyongo ambayo kazi yake ni kusharabu aina mbalimbali za vyakula kama vile vya mafuta na vitamin mbalimbali kwenye sehemu ya mmeng’enyo wa chakula pamoja na kukipa choo rangi yake.

Katika nchi zinazoendelea inakadiriwa asilimia 51 ya watoto wanaozaliwa wanapata manjano na vifo vinakadiriwa kuwa 100,000 kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, huku watoto zaidi ya 63,000 wakipata madhara ya kudumu ya mfumo wa fahamu.

Kwenye jamii ni jambo la kawaida kwa mtoto mchanga kupata ugonjwa wa manjano, siku chache baada ya kuzaliwa na wazazi wengi hawajui nini sababu za watoto wao kupata tatizo hilo.

Daktari bingwa wa watoto kutoka Hospitali ya Mkoa wa Geita, Shaban Massawe anasema hali hiyo hutokana na kuzidishwa kwa bilrubin ambayo ni rangi inayoundwa wakati wa kuvunjwavunjwa kwa seli nyekundu za damu.

Kwa mujibu wa Dk Massawe, zipo aina mbalimbali za manjano, mojawapo ni ile mtoto anazaliwa na wingi wa seli nyekundu ambazo huvunjwavunjwa ili ziwe kwenye namna rahisi ya kutoka mwilini na sehemu pekee ya kuzivunjavunja ni kwenye ini.

Manjano nyingine ni ile inayosababishwa na maziwa ya mama, Dk Massawe anasema ipo homoni ya frojestro ambayo inazuia protini ambayo kazi yake ni kubeba manjano (bilrubin) iliyozalishwa na kuwekwa kwenye ini ili iweze kuvunjwavunjwa na kuwekwa kwenye namna rahisi ya kuondolewa mwilini.

Anasema maziwa ya mama yanapokuwa kwenye hiyo homoni, inazuia kitendo hicho cha kuvunjwavunjwa kisifanyike na matokeo yake mtoto hupata manjano na wakati mwingine ni mama kutonyonyesha kwa wakati.

“Ipo manjano inayosababishwa na bakteria ambazo husababisha seli nyekundu za damu kuvunjwavunjwa kwa wingi na kutengeneza manjano inayoenda kujikusanya kwenye ngozi na macho na mwisho wa siku mtoto anapata manjano,” anasema.

Kwa mujibu wa Dk Massawe, kutowiana kwa kundi la damu kati ya mama na mtoto, inaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa wa seli nyekundu za damu na mkusanyiko wa bilirubini na kusababisha mtoto kupata manjano.

Tatu, anataja upungufu wa baadhi ya Enzaims (vimeng’enyo) vinavyorahisisha shughuli za kikemikali za mwili ziweze kufanya kazi kwa haraka.

Anasema kazi kubwa ya enzaims ni kubeba manjano iliyoko chini ya ngozi na kuipeleka kwenye ini ili ibadilishwe na kwenda kwenye namna rahisi ya kuondolewa na pale unapokuta enzaims hazifanyi kazi vizuri au mtoto hakuzaliwa nazo kusababisha apate manjano.

Aidha sababu nyingine ni magonjwa ya kimaumbile. Dk Massawe anasema mtoto anapozaliwa kwenye ini kuna mfumo wa manjano, inapozalishwa inatolewa kwenye ini inapelekwa kwenye mirija mbalimbali na kufikishwa kwenye kifuko cha nyongo na kutoka kwenye kifuko cha nyongo hadi kwenye utumbo mdogo.

Anasema pale unapokuta mishipa inayotumika ina shida, manjano iliyozalishwa ikikosa pakwenda hurudi kwenye damu na mwisho wa siku inaenda kujificha kwenye ngozi na matokeo yake huonekana kwenye macho na ngozi.

Kwa mujibu wa daktari huyo bingwa wa magonjwa ya watoto, mtoto mwenye hatari ya kupata manjano ni yule anayechelewa kupata maziwa ya mama au yale ya kopo na wale wanaozaliwa au kupata homa pamoja na wale wanaozaliwa kwenye uzazi pingamizi.

Dk Massawe anasema ili kutoa matibabu ya manjano, moja ni kujua sababu zilizosababisha mtoto apate manjano, kama ni maambukizi, ataanzishiwa dawa kama antibiotiki na kama amechelewa kunyonyeshwa mzazi atashauriwa kumnyonyesha mara kwa mara au kumuanzishia maziwa ya kopo kama yeye ana changamoto ya maziwa.

Mwisho kabisa ni tiba mwanga, hii ni tiba ya mwanga maalumu ambao una vigezo maalumu unaotumika kubadilisha manjano iliyoko kwenye namna ngumu kutoka mwilini, inarahisishwa kwenda namna rahisi ambayo mwili unaweza kuiondoa kupitia mkojo au choo.

Tiba hii mtoto atalazwa na kufunikwa sehemu za macho na sehemu za siri na kuwashiwa mwanga wa bluu au mweupe. Hii ni aina fulani ya mionzi inayotumika kuvunjavunja manjano iliyoko kwenye hali ngumu kwenda kwenye hali rahisi.

Akitaja madhara, Dk Massawe anasema Manjano ikiwa nyingi na isipotolewa kwa haraka huenda kwenye kizuizi kilichoko kati ya damu na ubongo na ikivuka inaenda kujirundika kwenye maeneo mbalimbali ya ubongo na mwisho wa siku mtoto anapata ugonjwa kwenye ubongo.

Anasema hali hiyo husababisha ubongo kushindwa kufanya kazi vizuri kutokana na mrundikano wa manjano kwenye ubongo na endapo hatatibiwa mapema, anaweza kupata degedege ya mara kwa mara, kuwa na uwezo mdogo wa kufikiri, ulegevu wa viungo, kushindwa kukua kama watoto wengine, kuchelewa kutembea, kuongea na wakati mwingine wanakuwa na ulemavu wa kudumu.

Dk Massawe anasema kama mtoto hatapatiwa matibabu anaweza kupoteza maisha kutokana na kuwa na manjano kali.

Daktari wa watoto kutoka hospitali ya Mji Geita, Sospiter Marwa anasema pamoja na elimu ya afya kutolewa kwa jamii, bado wapo baadhi wanaoamini dawa za kienyeji, hivyo wakiona tatizo badala ya kuwahi hospitali huanza kutafuta dawa hizo ambazo huathiri figo na ini.

“Wazazi wasitibu manjano kwa dawa asili, mwili wa mtoto hauwezi kuchakata dawa za kienyeji, wanaanza kwa waganga wanapewa dawa, wakija hapa tayari mwili umevimba, ukipima unakuta ini limeharibika, ukihoji anakwambia ameshauriwa kutumia dawa za asili, mwisho wa siku anampoteza mtoto,” anasema Dk Marwa.

Muuguzi kiongozi kitengo cha watoto wachanga hospitali ya Mji Geita anasema kwenye hospitali hiyo hupokea watoto watatu hadi watano kwa mwezi wenye tatizo la manjano, huku wengi wakitokea maeneo ya vijijini.

Related Posts