Serikali yamchunguza anayedaiwa kujipatia ekari 100 za ardhi Mkuranga

Dar es Salaam. Serikali inaendelea na uchunguzi katika kesi ya kutakatisha Sh8 milioni zilizotokana na kununua eneo lenye ukubwa wa ekari 100 katika Kijiji cha Kibesa Wilaya ya Mkuranga Pwani inayomkabili raia wa Burundi, Kabura Kossan (65).

Kossan anakabiliwa na mashtaka sita katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Baadhi ya mashtaka hayo ni pamoja na kughushi kitambulisho cha Taifa (Nida), kitambulisho cha mpiga kura na kujipatia eneo hilo, huku akijua anaishi nchini Tanzania kinyume cha sheria.

Wakili wa Serikali, Erick Kamala ametoa maelezo hayo, leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa Mwankuga wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa njia ya video na kisha kupangiwa tarehe nyingine.

Kamala amedai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea na kwamba upande wa mashtaka wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mwankuga amekubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 30, 2024 itakapotajwa tena na mshtakiwa yupo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha kutokuwa na dhamana.

Kwa mara ya kwanza mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo Agosti 27, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 24289/2024.

Katika shtaka la kwanza, Kossan anadaiwa kukutwa akiishi nchini bila kibali.

Shtaka la pili anadaiwa kughushi kitambulisho cha mpiga kura chenye jina la Charles Ng’andu kwa lengo la kuonyesha kuwa kimetolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), wakati akijua si kweli.

Pia anadaiwa kuwasilisha kitambulisho hicho kwa maofisa wa Polisi, wakati akijua kitambulisho hicho sio cha kweli.

Kossan pia anadaiwa alighushu kitambulisho cha Taifa chenye jina la Charles Ng’andu akionyesha kuwa kimetolewa na Mamlala ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), wakati akijua si kweli.

Inadaiwa kuwa mshtakiwa huyo alikiwasilisha kwa maofisa wa Polisi, wakati akijua kufanya hivyo ni kinyume cha sheria.

Shtaka la sita ni kutakatisha fedha, tukio analodaiwa kulitenda kosa hilo Septemba 15, 2010 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Inadaiwa siku hiyo ya tukio, mshtakiwa akiwa raia wa Burundi alijipatia eneo lenye ukubwa wa ekari 100 lililopo Kijiji cha Kibesa wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani kwa gharama ya Sh8milioni, huku akitambua kuwa fedha hizo ni mazalia ya kosa tangulizi la kuishi nchini bila kuwa na kibali.

Related Posts