UTAMU wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) unaendelea leo kwa mechi tano za kufungia mwaka, huku macho na masikio ya mashabiki yataelekezwa kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa wakati wenyeji Fountain Gate Princess watakapoialika JKT Queens, huku vinara na watetezi Simba Queens wakiwa ugenini kuikabili Bunda Queens.
Simba inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 19 bila kupoteza baada ya mechi saba, itakaribishwa kwenye Uwanja wa Karume, mjini Musoma Mara, huku watani wao wa jadi, Yanga Princess watakuwa jijini Dar es Salaam kuikaribisha Get Program ya Dodoma kwenye Uwanja wa KMC Complex, uliopo Mwenge.
Mechi nyingine za kufungia mwaka kabla ya kusubiriwa kuingia kwa Mwaka Mpya wa 2025 ni pamoja na Alliance Girls itakayokuwa wenyeji wa Ceasiaa Queens kwenye Uwanja wa Nyamagana na Mashujaa Queens watamalizana na Mlandizi Queens kwenye Uwanja wa TFF Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Hadi sasa ligi ikiingia raundi ya nane, ni mechi tatu za raundi iliyopita ya saba ndizo zilizochezwa, huku mbili zikiahirishwa Ceasiaa dhidi ya Bunda na ile Get Program dhidi ya Fountain zilizokuwa zichezwe Desemba 21 ambapo sasa itapangiwa tarehe nyingine mwakani.
Katika mechi hizo tatu za raundi ya saba zilizochezwa Yanga ilipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya JKT Queens, huku Simba ikishinda 2-0 dhidi ya Mashujaa na Alliance ikitoa kichapo cha 5-1 kwa Mlandizi Queens iliyopo mkiani mwa msimamo.
Hadi sasa mambo yanaonekana kuwa mazuri zaidi kwa watetezi, Simba walioendelea kusalia kileleni huku wakiwa timu pekee ambao haijapoteza katika mechi saba ilizocheza ikivuna pointi 19 kati ya 21 ilizotakiwa kuzipata.