Walilia uraia pacha, kisa kudhulumiwa na ndugu zao

Dar es Salaam. Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) wamesisitiza haja ya kuwa na uraia pacha ili kuepuka usumbufu, ikiwa ni pamoja na uhalifu wanaofanyiwa na ndugu na jamaa zao wanapowatumia fedha kwa ajili ya kuwekeza kwenye vitega uchumi.

Mara kadhaa Serikali imetoa msimamo suala la uraia pacha, ikisema linasimamiwa na Sheria ya Uraia ya Tanzania sura ya 357, rejeo la mwaka 2002 inayotoa uraia pacha kwa watoto pekee na si kwa watu wazima.

Msimamo huo wa Serikali ulitolewa bungeni na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo Aprili mwaka huu, akijibu swali la mbunge wa viti maalumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Suma Fyandomo aliyehoji sababu za Tanzanaia kutoruhusu uraia pacha.

Aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk akijibu swali hilo alisema kama Serikali itaoa haja ya uwepo wa uraia pacha mchakato wake utafanyika.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Michael Mlowe, diaspora wa Tanzania aliyeko Uingereza, amesema mkasa ambao hatausahau katika maisha yake ni kudhulumiwa mali zake na mtu anayemtaja kuwa mpenzi wake.

Mlowe anadai kuwa mtu huyo amemtapeli nyumba na viwanja baada ya kuwa anatuma fedha kwa nyakati tofauti kwa ajili ya kuvinunua.

“Ilikuwa mwaka jana tulitofautiana kidogo tu akaenda kukata RB polisi nikamatwe nitakapofika nchini, wakati sifahamu lolote. Nilirudi Tanzania nikakamatwa kwa kile kilichoelezwa nimekuja kumfanyia fujo,” amesema.

Mlowe anasema mtu wake huyo, alitoa maelezo yeye ni raia wa kigeni na anapofika nchini humsababishia fujo.

“Ninachoomba Serikali iangalie suala la uraia pacha ni muhimu sana, sisi tunaonekana sio raia na watu wanaiba mali zetu, hatuwezi kuwafanya lolote kwa sababu ya uongo wanaoutengeneza,” amesema.

Diaspora mwingine, Hamidu Mwasanyage anayeishi Marekani amesema wengi wanadhulumiwa na ndugu na marafiki wanapowatumia fedha za kununua mali nchini.

Amesema diaspora wanawaamini ndugu zao kwa uwekezaji kwenye mashamba na ujenzi wa nyumba, wanapodhulumiana wengine wana shtakiana na kifikishana mahakamani au kusamehe.

“Mimi rafiki yangu ninayeishi naye huku ndugu yake tumbo moja yupo Dar es Salaam alimsomesha hadi akamaliza chuo kikuu akaajiriwa, wakashauriana wanunue mashamba Morogoro.

“Basi akawa anamtumia fedha za kununulia, lakini ikawa kinyume mdogo wake akachukua fedha akaenda kuoa wake wawili kwa wakati mmoja,” amesema.

Tukio la pili, Mwasanyage amesimulia mke wake alikubaliana na marafiki zake kuchanga Sh10 milioni kununua viwanja Kigamboni na mwisho alidhulumiwa kiwanja.

Akisimulia tukio hilo Mwasanyage anasema kuna mtu alimtumia fedha mdogo wake baada ya kumwambia shamba ekari 10 linauzwa Sh25 milioni wilayani Kibaha (Pwani), alitumiwa Sh27 milioni, shamba lililonuliwa lilikuwa ekari tano.

Naye Mars Lyimo diaspora wa Tanzania nchini Norway amesema changamoto iliyomkumba nayo ni kudhulumiwa fedha zake hapa nchini.

“Rafiki yangu yupo Tanzania kanitafuta akaniomba nimsaidie fedha atanirejeshea, tangu nilipompa hadi sasa nikimtafuta simpati, uaminifu ni mdogo sana hata kwenye mashamba, tatizo ndio kubwa watu kudhulumiwa,” amesema.

Kwa upande wake, Adinani Milanzi diaspora wa Tanzania Afrika kusini, amesema alinunua shamba la ekari tano Kata ya Vianzi wilayani Mkuranga (Pwani) akimshirikisha kaka yake na mdogo wake.

“Niliamua kwenye hati ya shamba niweke jina la kaka yangu na langu ili iwe rahisi kufuatiia, kila nikirudi nchini kwenda kuangalia hilo shamba hakuna kinachofanyika, nikajaribu kuuza ikashindikana, nilivyoondoka na kurudi tena shamba tayari limeuzwa,” amesema.

 Milanzi amesema baada ya kufuatilia aliambiwa aliyeliuza shamba lile ameshafariki dunia na mwenyekiti wa Serikali za Mitaa alishakimbia ofisi.

Amesema hata alipouliza kwa kaka yake, alijibiwa atafuatilia bila utekelezaji, kitendo alichodai kilimfedhehesha hivyo kuamua kunyamaza ili kutoibua ugomvi na ndugu zake.

Akizungumzia jinsi ya kuondokana na changamoto hiyo kwa diaspora, Oscar Mkude mchambuzi wa masuala ya uchumi amesema malalamiko hayo pia wanayapata watu wengi wanoishi mbali na sehemu zao za asili.

“Tatizo hasa ni hali duni za kipato za hao wanaoombwa kusimamia fedha zinazotumwa, wanajikuta wanakosa uaminifu na kuanza kutumia fedha vibaya na hivyo kuathiri utekelezaji wa lengo kusudiwa,” amesema. 

Mkude amesema diaspora wanapaswa kutambua ni hatari kutumia mfumo wa kufahamiana kwenye utekelezaji wa miradi.

 “Nashauri watu, pamoja na diaspora, waanze kutumia taasisi zilizosajiliwa zinazofanya kazi kama hizo za usimamizi wa miradi na kulipwa ada ya huduma. Hii itawapa uwezo wa kuwawajibisha kisheria wanapofanya kinyume na makubaliano ya kimkataba,”

“Lazima kuanza kuchukulia uwekezaji wowote tunaoufanya kibiashara na kisheria zaidi, tuingie mikataba ya usimamizi ili tuwe na nguvu ya kuwawajibisha wale tuliowapa kazi na tunaowalipa fedha kwa kazi hizo, wanaposhindwa kutekeleza kwa mujibu wa mkataba,”amesema.

Mchango wa diaspora nchini

Ripoti ya mifumo kitaifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwaka 2022 inaonyesha mwaka 2023 diaspora waliichangia Tanzania Sh829 bilioni.

Related Posts