Watu 11,703 waugua kipindupindu, 145 wafariki dunia tangu Januari

Dar es Salaam. Wizara ya Afya nchini Tanzania imesema kati ya Januari Desemba 22, 2024 watu 11,703 wameugua ugonjwa wa kipindupindu na wengine 145 wamefariki dunia.

Ugonjwa huo umeikumba mikoa 23, ulioathirika zaidi ni Mkoa wa Simiyu wenye jumla ya wagonjwa 4,246 sawa na asilimia 36 ya wagonjwa wa mikoa yote.

Hali hiyo inaripotiwa wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine duniani leo Desemba 27, 2024 kuadhimisha siku ya kimataifa ya kujiandaa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko, ikiainisha namna ilivyojipanga kudhibiti magonjwa hayo.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa Wizara ya Afya, Dk Ntuli Kapologwe amesema kipindupindu kilianza Januari 2023 na kimeikumba mikoa 23.

“Mikoa hiyo ni Mara, Kigoma, Kagera, Singida, Simiyu, Shinyanga, Tabora, Ruvuma, Mwanza, Geita, Rukwa, Dodoma, Manyara, Morogoro, Katavi, Pwani, Mtwara, Tanga, Arusha, Songwe, Lindi, Mbeya na Dar es Salaam.

Mikoa ambayo haijatoa taarifa za ugonjwa katika kipindi tajwa ni Njombe, Iringa na Kilimanjaro,” amesema.

Dk Kapologwe amesema mikoa ambayo tayari imedhibiti ugonjwa huo ni Mtwara, Arusha, Tabora, Geita, Kagera, Ruvuma, Dar es Salaam, Mara, Pwani na Songwe.

Amesema mikoa ambayo bado inatoa taarifa za wagonjwa ni Simiyu, Kigoma, Mwanza, Katavi, Mbeya, Morogoro, Rukwa, Lindi, Tanga, Manyara na Shinyanga.

Akizungumzia namna Wizara ya Afya ilivyojipanga kudhibiti ugonjwa huo, Dk Kapologwe amesema wameongeza uwezo wa timu za ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ngazi ya Taifa, mikoa na halmashauri.

“Hii ni kupitia programu za mafunzo kwa ‘rapid response teams’ programu ya mafunzo ya AVoHC (African Volunteers health Cops), Programu ya mafunzo ya FELTP (wataalmu zaidi ya 1,000 wamepata mafunzo ya muda mrefu na wengine muda mfupi,” amesema.

Hatua nyingine ambazo Wizara ya Afya imechukua ni kuongeza idadi ya wataalamu wa kudibiti afya mipakani kupitia ajira mpya za watumishi 202 katika mwaka 2024.

Amesema wameanzisha vituo 16 vya udhibiti wa magonjwa (PHEOCs) ambavyo wataalamu wake wamejengewe uwezo, ikiwemo kutoa mafunzo ya jinsi ya kujikinga na maambukizi.

Hatua nyingine iliyochukuliwa, amesema ni kujenga uwezo wa maabara kupima aina mbalimbali za vimelea, vikiwemo virusi vipya na vinavyoibuka tena.

Amesema mkoani Kagera imepelekwa maabara inayohama (tembezi) moja na wanahakikisha kunakuwepo vitendanishi na vifaa vingine.

Akizungumzia upatikanaji wa vifaatiba, amesema dawa zinapatikana nchini kwa asilimia 86.

Mtaalamu huyo amesema wanaendelea na kampeni za kutokomomeza ugonjwa huo kupitia wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na kampeni kabambe ya mtu ni afya, ambayo inajumuisha mikakati ya WASH ikiwa ni pamoja na kutibu maji ya visisma vilivyochafuliwa na ugawaji wa vidonge vya kutibu maji.

Pia kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 na kukagua sehemu za kuandalia vyakula.

Akizungumzia changamoto zilizopo katika maeneo yalikoibuka ugonjwa huo, Dk Kapologwe amesema ni kutokupatikana kwa majisafi na salama.

“Hii inachangiwa pia na kuwepo kwa mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababisha kuwepo kwa vipindi vya kubadilishana kati ya ukame na mafuriko,” amesema.

Vilevile uhaba wa miundombinu ya kuhakikisha upatikanaji wa maji salama na imani potofu za jamii juu ya maji yaliyochemshwa.

“Sehemu ya jamii kutokuwa na vyoo bora na kuvitumia, wengine hawana kabisa, wengine vilivyopo vinaharibiwa na mafuriko. Kuna imani potofu kuhusu ugonjwa wa kipindupindu, bado baadhi wanaamini wagonjwa wamelogwa, hivyo kuwapeleka wagonjwa kwa waganga wa kienyeji kwanza, kabla ya vituo vya kutolea huduma za afya,” amesema.

Pia amezungumzia hali duni za usafi, kutokutupa kwa usahihi choo cha mtoto na umwagaji hovyo maji machafu.

Dalili za ugonjwa huo ni kuharisha majimaji yanayofanana na maji ya mchele, kutapika, kujisikia mlegevu, kukosa nguvu, wakati mwingine kusikia maumivu ya misuli, upungufu wa maji mwilini.

Vilevile kuna wakati mgonjwa anakuwa na ngozi iliyosinyaa na mdomo kukauka.

Ili kuepuka kipindupindu hatua zinazopaswa kuchukuliwa ni kuimarisha hatua za upatikanaji wa maji, kunawa mikono kila wakati kwa sababuni na kusaidia jamii kupata majisafi.

Unywaji wa majisafi, maji yaliyochemshwa, kuepuka vyakula vya mtaani vinavyopikwa na kutayarishwa katika mazingira duni ya usafi.

Related Posts