Dodoma. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima ametoa pole kwa wazazi wa mtoto Graison Kenyenye aliyeuawa na watu wasiojulikana, huku akiwataka wazazi au walezi kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto.
Tukio hilo lilitokea Ilazo Extension jijini Dodoma Desemba 25, 2024, wakati mfanyabiashara Zainab Shaban maarufu Jojo alipomuacha mtoto huyo nyumbani kwa rafiki yake wa kiume ambaye ni Ofisa Uvuvi Mtera, Hamis Mpeta.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi, tukio hilo lilitokea Desemba 25,2024 saa 1.00 asubuhi ambapo Mpeta akiwa na mama wa mtoto Zainab walibaini mtoto huyo kuuawa baada ya kurejea kutoka matembezini.
“Walimkuta mtoto huyo akiwa ameuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na shingoni amekatwa na kitu chenje nja kali. Katika tukio hilo ni kwamba mama wa mtoto alimwacha chini ya uangalizi dereva bodaboda anayejulikana kwa jina la Kelvin Gilbert,” alisema.
Katika taarifa yake kwenye vyombo vya habari leo Ijumaa Desemba 27, 2024, Dk Gwajima amesema wizara yake imepokea kwa taarifa hizo za masikitiko kwa simanzi kubwa kutokana na mtoto huyo kukatishwa uhai wakati ndiyo kwanza alikuwa anaanza safari ya ndoto za maisha yake.
“Natoa pole nyingi kwa wazazi wa mtoto, ndugu na jamaa kwa msiba huu mkubwa uliogusa hisia za wengi,” amesema.
Ametoa wito kwa wazazi au walezi kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto na kukumbuka kuwa, tafiti zinaonyesha ndugu jamaa wa karibu ndio wanaoongoza kuwafanyia watoto ukatili ikiwa ni pamoja na ubakaji, ulawiti na hata mauaji.
“Ninaimani vyombo vya kusimamia sheria vinafuatilia jambo hilo kwa kadiri iwezekanavyo ili wahusika waweze kubainika na haki ya mtoto iweze kupatikana na kuwa funzo kwa wengine wanaofanya ukatili kwa watoto.
“Kwa mara nyingine, natoa pole kwa wafiwa, Mwenyezi Mungu awape moyo wa uvumilivu katika kipindi hiki kigumu, mtoto Graison apumzike kwa amani,” amesema.
Tayari Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, linawashikilia watu wawili ambao ni pamoja na dereva bodaboda, Kelvin Gilbert na mtu mwingine ambaye jina lake halijatajwa kwa sababu za kiuchunguzi.
Mtoto huyo alizikwa jana (Desemba 26, 2024), katika makaburi ya Kilimo Kwanza jijini Dodoma.