Ajali yaua sita Mbinga, wamo walimu wanne wa shule moja

Nyasa. Watu sita wakiwamo walimu wanne wa Shule ya Msingi Lumalu wilayani Nyasa Mkoa wa Ruvuma, wamefariki dunia kutokana na ajali ya gari lililogonga gema na kuwaka moto katika Kijiji cha Lumala leo Desemba 28, 2024.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 28, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marko Chilya amesema ajali hiyo imetokea katika Kijiji cha Lumalu Kata ya Upolo leo saa 1:10 asubuhi.

Amesema chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva kushindwa kuchukua tahadhari kutokana na kona nyingi na mteremko katika Wilaya ya Mbinga.

Amewataja waliofariki katika ajali hiyo kuwa ni pamoja na dereva ambaye pia ni mmiliki wa gari aina ya Toyota Land Cruiser Prado.

Wengine ni Damas Namkombe, Dominic Ndau, Judith Nyoni, John Mtui wote wakiwa ni walimu wa Shule ya Msingi Lumala na Boniface Mapunda aliyekuwa mhitimu wa kidato cha sita.

“Wote walikuwa wakienda kuhudhuria mafunzo ya BVR (Uandikishaji wa wapigakura kielektroniki) wilayani Nyasa mkoani Ruvuma.

“Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva kushindwa kuchukua tahadhari kutokana na kona kali zilizopo katika barabara hiyo,” amesema.

Akifafanua zaidi, amesema dereva huyo alishindwa kulimudu gari na hivyo likaacha njia na kwenda kugonga gema na kuwaka moto.

“Aliweza kukata kona ya kwanza alipokwenda kona ya pili kwa sababu ile njia ina kona nyingi na imechongwa, gari liliacha njia na kwenda kugonga gema na kuwaka moto.

“Mle ndani hakuna aliyetoka, bali wote waliungua,” amesema.

Amesema miili ya marehemu imepelekwa kuhifadhiwa katika hospitali ya Wilaya ya Mbinga. 

Akizungumza katika eneo la ajali kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyasa, Salumu Ismail amesema watumishi hao walikuwa wakienda Nyasa katika Shule ya Sekondari Limbo kufanya usaili ya watendaji, pamoja na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Amewashukuru wananchi kwa kujitokeza katika eneo la ajali na amewaomba ajali ikitokea wakimbilie na kutoa msaada.

Amewaomba ndugu za marehemu kuja kupima vinasaba (DNA) kwa ajili ya utambuzi.

Kwa upande wao Mashuhuda wa ajali hiyo, Logatus Venant amesema aliona gari hiyo ikikosa mwelekeo ambapo watu waliokuwemo kwenye gari waliumia na kupoteza maisha.

Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, Khalid Khalif amesema ajali hiyo ni pigo kubwa kwa halmashauri na familia za watumishi hao na Taifa.

“Halmashauri itafanya msawazo kwa shule ya msingi Lumulu ambayo ndio imeathirika kwa kupoteza walimu wanne na wamebakia watatu,” amesema.
Amesema watashugulikia vibali vya ajira mbadala na kudumu ili kupata walimu wengine.

Ameongeza kuwa halmashauri inaendelea na taratibu za kuandaa mazishi na kuwashika mkono wafiwa.

Ajali hiyo imetokea baada ya mfululizo wa ajali zilizoondoa uhai wa watu, huku wengine wakijeruhiwa.

Desemba 3, 2024 watu saba walifariki dunia katika ajali iliyohusisha magari matatu, wilayani Karagwe mkoani Kagera.

Desemba 6, 2024 wabunge 16, maofisa wawili wa Bunge na dereva wa basi la kampuni ya Shabiby, walijeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea eneo la Mbande, wilayani Kongwa mkoani Dodoma, baada ya basi walilokuwa wakisafiri kwenda kwenye michezo ya Afrika Mashariki, Mombasa nchini Kenya, baada ya basi lao kugongana na lori lililokuwa likitoka Morogoro kuelekea Dodoma.

Desemba 18, 2024 watu 15 walifariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali iliyotokea Mikese mkoani Morogoro. Katika Ajali hiyo, gari aina Toyota Coaster liligongana na lori.

Desemba 20, 2024 abiria 44 wa basi la kampuni ya usafirishaji ya Kisire walijeruhiwa baada ya basi hilo kupata ajali iliyosababishwa na dereva alipojaribu kulipita gari la kampuni ya George Town bila kuchukua tahadhari katika eneo la Magu, mkoani Mwanza.

Pia, Desemba 20, 2024 watu sita wa familia moja waliokuwa wakisafiri na gari aina ya Toyota Harrier walinusurika kifo baada ya gari hilo kupinduka kwa kuacha njia na kuingia kwenye mtaro eneo la Kizumbi, katika Manispaa ya Shinyanga.

Ajali nyingine ni ile iliyokatisha uhai wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko na binti yake, Maureen Nnko na kujeruhi wanafamilia wanne, akiwemo mke na watoto watatu wa Nnko. Ajali hiyo illitokea Desemba 22, 2024.

Wiki hii takribani watu 20 wamepoteza maisha Handeni mkoani Tanga baada ya kutokea ajali mbili tofauti.

Mkoani Kilimanjaro watu 10 walipoteza maisha kwenye ajali ya Noah iliyogongana na basi la Ngasere.

Related Posts