Dodoki, nguo za ndani zinapogeuka kuwa hatari

Dar es Salaam. Dodoki, tunda mithili ya tango kubwa linapokauka hutumiwa na wanajamii kujisugua wakati wa kuoga.

Kutokana na maendeleo ya teknolojia, kwa sasa wapo wanaotumia vifaa vilivyotengenezwa viwandani maalumu kwa ajili ya kujisugua wakati wa kuoga. Si hivyo tu, wapo wanaotumia nguo za ndani kwa kazi hiyo.

Swali ni je, wajua matumizi ya dodoki la asili hayapaswi kuzidi wiki tatu, huku yale ya viwandani yaliyotengenezwa kwa plastiki yasizidi miezi miwili kwa afya ya mwili wako?

Wataalamu wa afya waliozungumza na Mwananchi na wengine waliotoa ushahuri kupitia mitandao ya kijamii na tovuti wanabainisha hayo wakieleza, nguo za ndani zinapotumika kujisugua wakati wa kuoga zinahamisha wadudu kutoka eneo moja la mwili kupeleka lingine, hivyo kusababisha maradhi ya ngozi.

Tovuti inayochapisha tafiti mbalimbali za afya nchini Marekani, WebMD inaeleza dodoki la asili linatakiwa kulibadili kila baada ya wiki tatu hadi nne, huku yale ya viwandani yakitakiwa kubadilishwa kila baada ya miezi miwili.

Hata hivyo, jamii haina ufahamu kuhusu kubadilisha dodoki. 

“Sikumbuki nilinunua lini maana ni lile kama la wavu wanauza sokoni, lina muda, na muda wote lipo chooni linaning’inia,” amesema Frank Joram, mkazi wa Tabata.

Linda Mapunda anasema dodoki lake huliweka kwenye kopo la kuogea ili kuepuka kulichanganya na la kuoshea vyombo.

“Yanafanana sasa ukisema ulitoe mtoto anaweza kutafuta la vyombo akilikosa akachukua hili, kuepusha hilo la kuogea hukaa kwenye kopo la chooni muda wote na sabuni yake,” amesema Linda.

Tovuti ya WebMd inashauri dodoki lisafishwe baada ya kutumika na ikishindikana lifuliwe mara moja kwa wiki kwa kuwekwa kwenye mchanganyiko wa maji na dawa ya kuua vijidudu kwa dakika tano.

Taarifa inaeleza hatua hiyo itasaidia kuua vijidudu ambavyo hujificha kwenye mikunjo ya dodoki.

Baada ya usafi wa dodoki linapaswa kuning’inizwa ili likauke haraka na si kuwekwa bafuni.

Kliniki ya Cleveland kupitia tovuti yake inasema dodoki linaweza kuwa na vimelea vya fangasi vinavyoweza kusababisha maambukizi kwenye ngozi.

“Ndiyo maana ni muhimu kuhakikisha unasafisha dodoki, kulibadilisha mara kwa mara na kulitumia polepole unapooga, usisugue ngozi kwa nguvu. Haijalishi aina ya dodoki, kuna nafasi kubwa ya bakteria na vitu vingine visivyopendeza kuishi humo,” inaeleza.

Mtaalamu wa afya ya ngozi, Dk Paul Masua amesema kwa kawaida mwili wa binadamu una bakteria wa kawaida ambao humlinda asishambuliwe na magonjwa.

Hata hivyo, bakteria hao anasema wanaweza kuathiriwa kwa namna tofauti ambazo mtu huzitumia kuoga ikiwemo matumizi ya dodoki ambalo wakati mwingine hubeba bakteria ambao si rafiki.

Bakteria hao anasema wanaweza kutoka kwenye maji yanayotumika ambao wanaweza kusalia katika dodoki ikiwa halitasafishwa vizuri.

Amesema bakteria hao mara nyingi chakula chao ni wale wanaooshwa kutoka mwilini hivyo kuwafanya kuendelea kuzaliana, huku hali ya majimaji inayokuwapo kwenye dodoki lisilokauka ikiweka mazingira mazuri zaidi kwao.

“Kwa bahati mbaya dodoki mtu akimaliza kuoga analiweka bafuni ambako hakuna mwanga wa jua,” amesema.

Dk Masua amesema uwepo wa bakteria humuathiri mtu kwa kumfanya apate magonjwa ya ngozi na ikiwa katika uogaji atachunika wanaweza kuingia mwilini moja kwa moja na kumsababishia maambukizi katika damu.

Tovuti ya Kliniki ya Cleveland inawataka watu kuepuka kutumia dodoki baada ya kunyoa, ikielekeza kusubiri kwa siku chache.

“Kutumia dodoki baada ya kunyoa huweza kufanya bakteria kuingia kwenye ngozi kupitia michubuko au vidonda vidogo,” inaeleza tovuti hiyo.

Inaeleza hakuna sababu ya mtu kutumia dodoki zaidi ya mara mbili kwa wiki, ikielekeza lisitumike usoni au sehemu za siri kwani ni maeneo yasiyopaswa kusuguliwa.

Daktari wa ngozi, Mike Mboneka amesema kwa kawaida ngozi ya mwili haipaswi kusuguliwa kwa kuwa kufanya hivyo ni kuiharibu.

“Dodoki linaleta magonjwa ya ngozi. Ngozi ina wadudu wa kawaida, ukijisugua na kuchubuka unaleta shida kwani watatoka na kuingia ndani, hii itakufanya upate magonjwa ya ngozi,” amesema.

Dk Masua amesema mtu hashauriwi kutumia nguo ya ndani kujisugua wakati wa kuoga, kwani kufanya hivyo ni kuhamisha bakteria kwenda eneo ambalo hawatakiwi, hivyo kuweza kuleta magonjwa.

“Unachukua bakteria wa sehemu za siri kwenda usoni, si sehemu yake wanaweza kuleta mambukizi au unachukua bakteria wa kichwani wanakwenda sehemu za siri si sawa,” amesema.

Anashauri watu kuanika dodoki enei lenye mwanga wa jua liweze kukauka inavyotakiwa na kuua vijidudu.

“Jambo la muhimu dodoki lisitumiwe kwa muda mrefu. Ukitumia kwa muda mrefu usafi wake unakuwa mgumu kutokana na uchakavu na kufanya kuwa makao mazuri ya bakteria,” amesema.

Related Posts