Kapama, Gustavo watua Fountain Gate

KLABU ya Fountain Gate iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa viungo Nassor Kapama kutoka Kagera Sugar na Daniel Joram ‘Gustavo’ kutokea Pamba, ili kuongezea nguvu katika timu hiyo yenye makazi yake Wilaya ya Babati mkoani Manyara.

Kapama aliyewahi kutamba na timu mbalimbali zikiwemo za Mtibwa Sugar na Simba, tayari amekuwa na mazungumzo chanya na mabosi wa Fountain Gate ambao wameonyesha nia ya kumuhitaji, sambamba na ‘Gustavo’ anayetolewa kwa mkopo na Pamba Jiji.

“Kapama na Gustavo wameshawasili jijini Dar es Salaam na walikuwa na mazungumzo na mabosi wa Fountain Gate, kwa taarifa zilizopo wamekubaliana maslahi binafsi na huenda muda wowote kuanzia leo (jana) wakawatangaza,” kilisema chanzo hicho.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua mastaa hao juzi walikutana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Fountain Gate, Kidawawa Tabitha katika ofisi zake zilizopo jengo la Mwanga, Makumbusho jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kukamilisha taratibu zote.

Mwanaspoti lilipomtafuta Kidawawa alieleza nisubiri kwanza taratibu zote zitakapokamilika, kwani kwa sasa mawazo yao yote wameyaelekeza katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga, utakaopigwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex Mwenge.

Nyota wengine wapya waliojiunga na kikosi hicho ni Said Mbatty na Faria Ondongo waliotokea Tabora United, Jackson Shiga (Coastal Union), Mtenje Albano (Dodoma Jiji), Jimmyson Mwanuke (Singida Black Stars) na winga, Kassim Haruna ‘Tiote’.

Related Posts