Mama wa pacha waliotenganishwa apewa makazi ya muda, atoa ombi kwa Samia-2

Dar es Salaam. Hadija Shaban (24), mama wa pacha waliotenganishwa nchini Saudi Arabia, Oktoba 23, 2023 anasimulia furaha aliyokuwa nayo alipopewa taarifa za kurudi nyumbani Tanzania baada ya wanawe kuendelea vyema kiafya.

“Nilihisi furaha ya ajabu nikiwaza kwamba watoto wangu wanarudi kwao wakamuone ndugu yao, mama na ndugu zangu wengine. Nilikumbuka sana nyumbani kwetu, nchini kwetu, nilijisikia furaha sana,” anasema.

Anasema furaha ilikamilika alipotua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

“Niliona furaha watoto wangu wamerudi nchini, wametenganishwa ni wazima, bila Serikali nisingewapata watoto hawa,” anasema.

Alipozungumza na Mwananchi Desemba 13, 2024 Hadija alisema hakuwa ameonana na ndugu yake hata mmoja, ingawa alizungumza na mama yake mzazi.

“Sijamuona ndugu hata mmoja. Mama niliongea naye, anasema hana nauli kuja huku (Dar), sasa hivi kijijini mvua inanyesha hawana kusema labda tumevuna tuuze kitu, hawana kitu, kwa hiyo ameshindwa kusafiri,” anasema.

Anasema anatamani kuonana na mwanaye mkubwa ambaye wametengana kwa muda mrefu, anayeishi na bibi yake.

Baada ya kurejea nchini, Hadija amepewa nyumba ya kuishi na MNH kutokana na kuendelea ufuatiliaji wa watoto hao.

Nyumbani hapo, Hassan na Hussein wanaonekana kuwa wachangamfu na wanacheza kama walivyo watoto wengine.

Hadija anasema wapo imara kiafya na wanatambaa, lakini ana wasiwasi kwa kuwa kila anakokwenda humfuata na akiwaacha sebuleni hupanda juu ya vitu, hivyo wanaweza kuuamia.

“Niko peke yangu. Nina wasaidizi wanakuja kunisaidia wanaondoka, wakati mwingine nakuwa jikoni, wanatembea kwa kutambaa wanapanda mpaka juu ya makochi na viti, nina wasiwasi wanaweza kuumia.

“Natamani kuwa na msaidizi ninapokuwa na shughuli awaangalie. Wanapigana, wakianza kupigana umtoe mmoja, unamwacha mwingine hapo Analia. Ukienda mbali, baadaye unamrudisha mwenzake ugomvi umeshaisha, unawaweka pamoja wanaendelea kucheza,” anasema.

Anasema fikra zake kwa sasa ni kuhusu namna atakavyomudu maisha katika safari ndefu ya kuwalea wanawe hao wenye miaka mitatu sasa.

Hadija anasema ametoka familia duni inayoishi Kijiji cha Kifulumo, Kata ya Sungwizi, Igunga mkoani Tabora.

“Maisha ya nyumbani kwetu ni magumu sana, hatuna kituo cha afya. Mazingira ya nyumbani kwetu ni magumu, kuna mito ambayo hata ukiwa na pikipiki lazima uivuke kwenda ng’ambo. Umeme hakuna na hata pikipiki kupata pia ni shida,” anasimulia.

Hadija anasema akipata fursa ya kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan, anaamini maisha ya watoto wake yatakuwa mikono salama katika ukuaji wao, kwa kuwa misaada ina ukomo.

Anasema hana elimu, alikuwa akijishughulisha na kilimo pamoja na mumewe, hivyo anahitaji kufanya biashara ambayo pia atahitaji kujifunza ili ajitegemee.

“Nawashukuru Watanzania kwa maombi, namshukuru Rais Samia, namuomba aje awaone wajukuu zake Hassan na Hussein, naamini ataona watoto hawa walivyo kwa macho yake na kuona namna anavyoweza kusaidia makuzi yao,” anasema.

Anasema kutokana na uduni wa maisha, hatamani watoto hao warudi Tabora kwani hakuna wataalamu wanaojua historia zao, hivyo inaweza kuwa vigumu katika matibabu.

“Hali ya nyumbani ngumu, ningeshukuru nikibaki mazingira ya huku, watoto wangu wawe wanahudhuria Muhimbili ambako wanajua wana changamoto gani, daktari wao mkuu ni Dk Zaituni na wasaidizi wake, ambao wanajua zaidi ikitokea shida yoyote wanawasiliana na madaktari kule Saudi Arabia.

“Hawa watoto wamewekewa njia mbadala ya kutoa haja, hivyo wanatumia mfuko mbadala wa kubebea choo, mfuko huu unauzwa Sh18,000 hadi Sh20,000. Pia wanatumia ‘pampasi’ na wana mguu mmoja kila mmoja, natamani wapate mguu bandia kama inawezekana,” anasema.

Anasema kwa sasa wanagharimiwa na Muhimbili, hajui hatima ya maisha ya watoto hao baadaye.

Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Zaituni Bokhari aliyewahudumia watoto hao tangu wakiwa na siku 12, anasema kutokana na maumbile yao baada ya upasuaji, kumetengenezeka kama kibiongo, hali inayowalazimu kuhitaji tiba mazoezi ya muda mrefu.

Anasema kwa mujibu wa maelekezo ya madaktari wa Saudi Arabia, wanahitaji kila baada ya siku tatu mpaka nne tiba ya viungo vya uti wa mgongo na mguu ili kuunyoosha uwe imara kabla hawajarejea Saudia mwakani kuendelea na matibabu.

“Wakienda mwakani kuna uwezekano wa kuwatengenezea mguu wa pili. Wanahitaji kuonwa na madaktari bingwa wa watoto wa mifupa kwa ajili ya kuangalia ukuaji wa mifupa unavyoendelea, pia kuangaliwa na madaktari bingwa wa kibofu cha mkojo, kwani cha mmojawapio kilikuwa na hitilafu, kinafunguka kwa nje, na kuleta shida.

“Mwingine alitengenezewa njia ya zamani ileile, ili mkojo uwe unatoka kwa nje, hivyo anatakiwa kuonwa na daktari bingwa wa mfumo wa mkojo mara kwa mara,” amesema.

Anasema Hassan ana sehemu haijaziba vizuri, hivyo anatakiwa kuangaliwa kwa umakini asipate maambukizi.

Anasema watoto hao wanatumia dawa za vitamini, madini ya chumvi kutokana na maumbile yao na pia wanahitaji kuonwa kwa ukaribu zaidi na madakati bingwa wa watoto, kwani kila mmoja amewekewa njia ya haja kubwa eneo la tumboni, hivyo wanahitaji uangalizi.

Anasema kila baada ya wiki mbili wanapaswa kuonwa na idara ya upasuaji wa watoto. Dk Zaituni anasema mama huyo anahitaji usaidizi, akieleza kuwa mume wake alimkimbia.

“Awali tulikuwa tunawasiliana naye kuhusu watoto wake na tunampa maelekezo, baadaye akakata mawasiliano kwetu hata kwa mkewe. Anahitaji kusaidiwa kwa kila kitu, watoto wanavaa pampasi zile kubwa, mmoja anabadilisha mara tatu mpaka nne, mfuko wa kuwekea choo mmoja Sh18,000 mpaka Sh20,000, hayo yote Muhimbili inagharamia kwa sasa.

“Wanatembea kwa kutambaa mikono inashika chini, huyu mwingine kidonda chake bado kuna sehemu ndogo inahitaji uangalizi. Wakiruhusiwa mapema watapata maambukizi, tunataka waondoke wakiwa kamili na hatutawaruhusu mpaka twende Tabora,” anasema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi anasisitiza kwa sasa watoto hao wapo chini ya uangalizi wa taasisi hiyo.

Anasema upasuaji ulifanikiwa kutokana na mahusiano mazuri kati ya Serikali ya Saudi Arabia na Tanzania.

“Bahati mbaya mzazi wao wa kiume yaani baba yao alikimbia, kwa hiyo sisi ambao tunakaa naye hapa tukaona kuliko kuwapeleka Tabora, ngoja tuwaweke sawa kwanza Muhimbili, tuna nyumba kadhaa ambazo tunazitumia kwa wageni wetu wanaotoka nje.

“Hivyo, mmoja wa madaktari wetu anawaona pale kila siku, Dk Zaituni na wenzake huwaangalia. Kwa hiyo tunafuatilia hali yao inavyokwenda,” amesema.

Amesema wanawasiliana na Tabora wakiwemo watu wa ustawi wa jamii kuona namna gani watakavyorejea huko.

Profesa Janabi anatoa rai kwa Watanzania wenye uwezo kumsaidia mama huyo kutokana na hali ilivyo.

“Watanzania wenye uwezo wanaweza kuja kututafuta, Tunachohitaji siyo hela pekee, tunaweza kumpata mtu akaja kumjengea nyumba Tabora na kuangalia yeye atapewa kitu gani, siyo siku ameenda kule sababu ya maisha duni mtoto ana homa au nimonia. Binafsi ukiacha mimi ni daktari, nalifikiria hili sana, akipata mtaji wowote wa kuanzia si mbaya,” anasema

Related Posts