Musoma watenga Sh580 milioni mikopo kwa makundi maalumu

Musoma. Wilaya ya Musoma mkoani Mara imetenga zaidi ya Sh580 milioni kwa ajili ya mikopo isiyokuwa na riba inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa mwaka wa fedha 2024/25.

Takwimu hizo zimetolewa leo Desemba 28, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka alipokuwa akifungua tamasha maalumu lililopewa jina la Mama Samia Musoma Festival,  huku akiwataka wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa hiyo.

Chikoka amesema mikopo hiyo ni moja ya fursa ambayo Serikali imeweka kwa ajili ya kuwainua kiuchumi wananchi kila mmoja kwa nafasi yake lengo likiwa ni kuboresha maisha ya Watanzania kupitia nyanja tofauti tofauti.

“Serikali inahakikisha kila mtu anawezeshwa kwa nafasi yake ili sote kwa pamoja tuwe sehemu ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii na katika kipindi hiki cha miaka mitatu na nusu ya Serikali ya awamu ya sita, mengi yamefanyika na bado yanaendelea kufanyika, tunachotakiwa kufanya ni kuiunga mkono Serikali,” amesema Chikoka.

Amefafanua kuwa mbali na mikopo hiyo, Serikali pia imeanza kutenga zaidi mikopo kwa wavuvi mikopo ambayo itawawezesha wavuvi hao kuanza ufugaji wa vizimba pamoja na kununua boti kwa ajili ya shughuli zao ili waweze kufanya kazi zao kwa tija zaidi.

Katika tamasha hilo la siku tano, mambo mbalimbali yamepangwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kongamano lenye lengo la kueleza fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya Wilaya ya Musoma, mashindano ya mbio za mitumbwi kwa wanawake na wanaume, maonyesho ya bidhaa mbalimbali za biashara kutoka kwa wajasiriamali, burudani na mkesha wa mwaka mpya.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma vijijini, Msongela Palela amewaomba wawekezaji kufika katika halmashauri hiyo ili kuwekeza katika sekta ya uvuvi hasa wa vizimba kwa maelezo kuwa tayari ofisi yake imebainisha na kutenga maeneo kwa ajili ya uvuvi huo.

“Tunayo maeneo 18 ambayo tayari yamebainishwa na kutengwa kwa ajili ya shughuli hii ya uvuvi wa vizimba, nitoe wito kwa wale wanaotaka kufanya uvuvi waje katika halmashauri yetu, fursa ipo,” amesema Palela.

Related Posts