Kursk. Mwanajeshi wa Korea Kaskazini anadaiwa kukamatwa na vikosi vya Jeshi la Ukraine katika eneo la mapigano la Kursk nchini Russia, lakini mwanajeshi huyo aliyekuwa na majeraha alifariki muda mfupi baada ya kutiwa mbaroni na vikosi hivyo.
Mwanajeshi huyo ni miongoni mwa zaidi ya askari 11,000 wa Korea Kaskazini waliopelekwa nchini Russia kuongeza nguvu, wakati vita hiyvyo zikiwa vimetimiza siku 1,038.
Tovuti ya The Guardian na Al-Jazeera zimeripoti kuwa kifo cha mwanajeshi huyo kimeripotiwa na Shirika la Habari la Yonhap la nchini Korea Kusini likinukuu chanzo kutoka Shirika la Ujasusi la Korea Kusini.
Mwanajeshi huyo ambaye picha zake zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha akiwa na majeraha mwilini anadhaniwa kuwa mfumo wa kivita wa kwanza wa Korea Kaskazini kukamatwa nchini Ukraine tangu Pyongyang itangaze kuiunga mkono Russia katika vita hiyo.
Kwa nyakati tofauti, Marekani nayo imetoa taarifa ikidai kwamba vikosi vya Korea Kaskazini vilivyopelekwa eneo la Kursk kupigana upande wa Russia vinapitia wakati mgumu katika vita hiyo na kudai hadi kufikia Desemba 25, 2024, takriban wanajeshi 1,000 wa Korea Kaskazini walikuwa ama wameuawa ama kujeruhiwa katika mapigano hayo.
Msemaji wa Ikulu ya Marekani, John Kirby amesema utawala wa Russia na Korea Kaskazini unawachukulia wanajeshi hao kama wapiganaji wa kukodiwa maarufu kama Expendable.
“Wanaamriwa kufanya mauaji yasiyo na tija dhidi ya vikosi vya Ukraine na wanatumika kutekeleza mauaji ya watu wasio na hatia,” amesema Kirby.
Shirika la Ujasusi la Korea Kusini, limedai kuthibitisha taarifa za uwepo wa wanajeshi wa Korea Kaskazini eneo la Kursk nchini Russia kutokea kwa washirika wao nchini Ukraine na kwamba mwanajeshi huyo aliyekamatwa alifariki kutokana na majeraha aliyokuwa nayo.
“Huu ni ukamataji wa kwanza kuwahi kutokea,” amesema Yang Uk ambaye ni Mtafiti wa Sera za Kimataifa kutoka Taasisi ya Asan nchini Korea Kusini.
Uk amedokeza kuwa hatua hiyo ni faida kwa Ukraine ambayo inataka kuwatumia mateka hao kufanya mabadilishano dhidi ya wanajeshi wake wanaoshikiliwa kama wafunga wa kivita nchini Russia.
“Picha zinazozunguka mitandaoni zinaonyesha kwamba mzozo wa Russia na Ukraine unavyoendelea inaonekana Korea Kaskazini itapeleka idadi kubwa zaidi ya wanajeshi wake katika kambi za Russia,” amesema.
Kwa mujibu wa Jeshi la Ukraine, wanajeshi hao wa Korea Kaskazini wametengenezewa utambulisho feki wa Russia, huku Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy akituma kipande cha video wiki iliyopita kikionyesha wanajeshi wa Russia wakichoma moto nyuso za wanaodhaniwa ni maiti za wanajeshi hao kutoka Korea Kaskazini waliouawa vitani.
Ukraine na Korea Kusini zimedai kuwa wanajeshi waliopelekwa vitani eneo la Kursk nchini Russia ni wanajeshi bora na wenye uwezo wa juu nchini Korea Kaskazini wanaofahamika kama wanajeshi wanaopigana kwenye mazingira yaliyoshindikana maarufu kama ‘Storm Corps.”
Wanajeshi hao wanadaiwa kupitia mazingira ya mateso, hujuma, hata kuuliwa wanapokuwa kwenye mafunzo ili kuwajengea uwezo wa kuhimili mikiki mikiki wanapokuwa vitani.
Kwa upande wake, Jumatatu Desemba 23, Rais Zelenskyy alisema zaidi ya wanajeshi 3,000 wa Korea Kaskazini wamekufa ama kujeruhiwa wakipigana upande wa Russia katika vita hiyo.
Russia ilianzisha ilichokiita Operesheni ya Kijeshi nchini Ukraine Februari 2022 na kupelekwa kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini nchini Russia ni ishara ya kuimarika kwa uhusiano kati ya Russia na Korea Kaskazini.
Muunganiko na ushirikiano kati ya mataifa hayo siyo tu umeibua hofu kwa Korea Kusini, pia umeibua hali ya sintofahamu ndani ya mataifa ya magharibi huku faida ikionekana kwenda kwa China ambayo inaushirikiano na pande zote za mzozo huo.
Kwa mujibu wa Oleg Chaus, ambaye ni Sajenti katika Kikosi cha 17 cha Silaha nzito cha Ukraine kilichopo eneo la Kursk ameieleza Aljazeera, kuwa Disemba 24,mwaka huu, askari wa Russia waliuawa kwa kashtukizwa kwa kutumia mashambulizi kutoka angani.
“Askari wote waliouawa kwenye makundi hayo matatu kila mmoja alikuwa na makombora ya kurusha, walikuwa na vifaa vya kuwawezesha kuona wakati wa giza na silaha ndogo ndogo za kufanyia mauaji.
“Makundi hayo yasingeuawa basi huenda Russia ingeendeleza uvamizi wake kwa kasi nchini Ukraine,” amesisitiza.
Desemba 24, 2025, hiyo Russia ilitekeleza mashambulizi 248 vilipo vikosi vya Ukraine kwa mujibu wa Ofisa Mkuu wa Jeshi la Ukraine, yakifuatiwa na mashambulizi 200 yaliyotekelezwa na Russia siku ya Krismas.
Wakati huo zilisambaa picha zikionyesha vikosi vya Russia vikisonga mbele kutokea Mashariki kwenda Magharibi mwa taifa hilo hadi Jiji la Kurakhove, nchini Ukraine na kukamilisha utekwaji wa Mji wa Donetsk nchini humo.
Msemaji wa Chuo Kikuu cha Luhansk Anastasia Bobovnikova, amesema mapigano hayo pia yalikuwa yameshika kasi eneo la mgodi katika Mji wa Toretsk nchini humo.
Mapigano makali zaidi pia yanatajwa kutokea katika Mji wa Pokrovsk nchini humo.
“Pokrovsk ni eneo la msingi na lenye reli inayounganisha maeneo mbalimbali sambamba na kuvirahisishia vikosi vya Russia kutokea mashariki kwenda magharibi mwa Ukraine,” amesema Mwanadiplomasia na Mwana Anga Mstaafu wa Marekani, Demetries Andrew Grimes alipozungumza na Aljazeera.
“Kuikamata Pokrovsk itakwamisha Ukraine kusafirisha vikosi na silaha zake na kutoa unafuu kwa Russia kusafirisha mahitaji ya wanajeshi wake wanaoendelea kusonga mbele katika eneo la vita,” alisema mwana anga huyo.
Kwa mujibu wa Bobovnikova, uvamizi na kutwaa maeneo hayo ya Ukraine kuna gharama zake ambazo Russia imeziingia ikiwemo kupoteza wanajeshi wake wabaofikia 17,400 katika kipindi cha wiki moja kuanzia Desemba 17 mwaka huu sawa na wanajeshi 52,200 kwa mwezi mmoja.
Hata hivyo uwezo wa Russia kuajiri wanajeshi wapya kwa mwezi unatajwa kuwa ni wanajeshi wapya 30,000 pekee kwa mwezi.
Wakati kukiwa na taarifa hiyo, Rais Vladimir Putin katika mkutano wake wiki hii amesikika akijibu kuwa Russia inapozungumzia kutwaa maeneo ya Ukraine hainaanishi mita 100, 200, 300 bali kilometa kadhaa za mraba.
Taasisi ya Utafiti wa Vita kutoka Washington Marekani inakadiria kwamba hadi sasa Russia inadhaniwa kuyateka maeneo ya Ukraine yanayokadiriwa kufikia Kilometa za Mraba 3,306 katika kipindi cha mwaka 2024 pekee.
Kuteuliwa kwa Trump na Naibu wake, JD Vance huenda kukawa ni ushindi kwa Vladimir Putin ambaye anaendelea kuyatwaa maeneo ya Ukraine hususan ni kipindi hiki ambacho anaenda kuapishwa kuingia Ikulu ya Washington huku kipaumbele chake kikiwa ni kukomesha vita hiyo ndani ya Saa 24 tangu kuapishwa kwake.
Russia ilionyesha uwezo wake Desemba 25 baada ya kufanya mashambulizi mazito nchini Ukraine kwa kurusha makombora zaidi ya 78 kutokea angani na makombora ya droni za Kamikaze 106 hata hivyo Ukraine ilidai kudungua makombora 113 kati ya 184 yaliyorushwa na Russia nchini humo.
Makombora mengine yalitua na kuharibu miundombinu ya nishati nchini humo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika