Mwanamke auawa na wanaodaiwa kuwa ‘michepuko’ yake

Bukoba. Jeshi la Polisi linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za mauaji ya Editha Andason, mkazi wa Mtaa wa Kilimahewa, uliopo Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, aliyeuawa kwa kunyongwa kwa mtandio shingoni.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Desemba 28, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda amesema wamefanikiwa kuwakamata watu wawili waliokuwa wakitafutwa kwa tuhuma za mauaji ya mwanamke huyo.

Watuhumiwa hao wanaoshikiliwa Kituo cha Polisi Bukoba ni Mtalewa Answali pamoja na Kennedy Muganyizi, wote ni wakazi wa Mtaa wa Kashenye, kata Kashai na inadaiwa wote walikuwa na uhusiano wa kimapenzi na marehemu Editha.

Chatanda amesema watuhumiwa hao wanadaiwa kufanya tukio hilo Desemba 12, 2024 katika maeneo ya Mtaa wa Kilimahewa baada ya kugundua kuwa wote wapo kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu mmoja.

Taarifa ya Kamanda Chatanda imedai kuwa Editha alikuwa na mume ambaye ni dereva bodaboda, baadaye akaanzisha uhusiano wa kimapenzi na mwenzake waliyekuwa wakifanya kazi sehemu moja, ambaye ni Mtalemwa Answali.

Baada ya muda, Editha alijikuta ameingia kwenye uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine ambaye ni Kennedy Muganyizi na Mtalemwa alipogundua kuwa mpenzi wake, Editha ana mtu mwingine, alishikwa na wivu na kuanza kupanga njama za mauaji.

Kamanda Chatanda, licha ya kutotaja kazi ambayo Editha na mwenzake Mtalemwa walikuwa wakifanya, amesema katika mahojiano na uchunguzi wa awali kwa watuhumiwa, imebainika Mtalemwa alimtafuta Muganyizi na kumueleza ukweli kuhusu uhusiano wake na Editha, kisha wakakubaliana kutekeleza unyama huo.

Amesema walitekeleza unyama huo wa mauaji ya Editha baada ya kumuita sehemu fiche waliyokuwa wakikutana kila siku, kisha mmoja akamkaba kwa mtandio shingoni, wakashirikiana kumhamisha eneo na kumtelekeza mtaroni.

“Kwa ufupi, wote walikuwa ni wezi wa mapenzi lakini kwa kuwa Editha aliamua kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine, mwenziye roho ikamuuma na badala yake Mtalemwa akamuita sehemu ambayo yeye aliona ni rahisi kufanya tukio la unyama ambalo kwa muda mwingi walikuwa wakikutana.

“Imeonekana alikabwa na kunigwa kwa kutumia mtandio, kisha akashirikiana na mwenzake Kennedy kumpeleka sehemu nyingine ili asiweze kutambulika kirahisi, ndiyo maana nikasema ni tukio la ajabu maana katika hali ya kawaida huwezi kulitarajia,” amesema Chatanda.

Katika hatua nyingine kwenye msimu huu wa sikukuu za Krismasi, Jeshi la Polisi limesema limeimarisha ulinzi sehemu zote kuhakikisha matukio ya uhalifu hayajitokezi.

Chatanda ameongeza kuwa katika operesheni ya usalama sikukuu ya Krismasi, Polisi wamefanikiwa kumkamata mtu mmoja mkazi wa Kijiji cha Kakindo kilichopo Wilaya ya Muleba, Japhes Rusolole (52) kwa kukutwa na silaha aina ya gobole aliyokuwa anaimiliki kinyume cha sheria kwa kufanyia uwindaji haramu. Mtuhumiwa huyo alikutwa na vipande tisa vya nyama ya pofu.

Related Posts