Nyongo kuongoza maziko ya kigogo wa Hazina, mwanaye

Arumeru. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo anatarajiwa kuongoza waombolezaji katika ibada ya maziko ya aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Amos Nnko na binti yake, Maureen Nnko.

Nnko na binti yake,  walifariki katika ajali ya gari iliyotokea maeneo ya Same mkoani Kilimanjaro, Jumapili Desemba 22, 2024.

Katika ajali hiyo, Nnko alikuwa na familia yake, ambapo waliojeruhiwa ni pamoja na mke wake, Agnes Nnko, watoto wao wawili; Marilyn na Melvin na mwanafamilia mwingine, Sylvana.

Maziko hayo yanafanyika leo Jumamosi Desemba 28, 2024 ambapo miili hiyo inatarajiwa kuwasili katika viwanja vya shule ya sekondari Seela, vilivyopo kata ya Seela Sing’isi, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Mbali na Naibu Waziri huyo, hadi sasa viongozi wengine ambao wamefika ni pamoja na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, Balozi Thobias Makoba, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amir Mkalipa, watumishi wa hazina na waombolezaji kutoka maeneo mengine.

Maureen (16), alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Mt. Monica iliyopo Moshono mkoani Arusha ambapo mwaka huu wa 2024, amehitimu kidato cha nne shuleni hapo na alikuwa akisubiri matokeo.

Miili hiyo imeingizwa viwanjani hapo ikiwa imebebwa na wazee wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam ambapo pia Nnko alikuwa akisali na pia alikuwa mzee wa kanisa.

Awali, akizungumza na Mwananchi kijijini hapo nyumbani kwa marehemu, mmoja wa ndugu za marehemu, Obilio Mbise alieleza kuwa waliwasiliana na ndugu yao ambaye alikuwa anaelekea kijijini humo kwa ajili ya kusheherekea sikukuu za Krismasi.

“Amos (Nnko) alinipigia simu Desemba 21, 2024 kwamba atakuja hapa Arusha kwa ajili ya kula sikukuu pamoja nasi na tarehe 22, asubuhi alitoka Dar es Salaam na saa 6 mchana tuliwasiliana naye akasema amefika Bwiko, lakini baada ya hapo hatukuwasiliana naye tena hadi tulipoambiwa amepata ajali,” ameeleza.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa awali na Mchechu, ilieleza mipango ya maziko inaendelea kuratibiwa na familia ya marehemu kwa kushirikiana na ofisi hiyo.

Related Posts