Daniel Chapo, ambaye ameahidi kuwa “rais wa wote” baada ya kuapishwa katikati ya Januari, alielezea masikitiko yake juu ya vurugu zilizotokea baada ya Baraza la Katiba kuthibitisha ushindi wa chama chake tawala, Frelimo, kwa asilimia 65.17 ya kura.
Kiongozi wa upinzani, Venancio Mondlane, aliyepata asilimia 24, anaendelea kukataa matokeo hayo na kuwataka wafuasi wake waandamane kwa amani.
Machafuko hayo yamesababisha vifo vya watu wasiopungua 261, huku 134 wakiripotiwa kufariki wiki hii pekee, kwa mujibu wa shirika la Plataforma Decide. Miji iliyoathirika zaidi ni pamoja na Maputo, Matola, Beira, na Nampula.
Chapo alikiri changamoto zinazolikabili taifa hilo maskini, akaahidi kujenga upya uchumi, na kupongeza juhudi za raia na vikosi vya usalama kurejesha utulivu, ingawa maafisa wa polisi kadhaa walipoteza maisha katika machafuko hayo.
Rais wa Msumbiji wakimbilia Malawi
Zaidi ya familia 2,000 za Msumbiji zimekimbilia Malawi wiki hii kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi.
Soma pia: Viongozi wa Afrika Kusini, Zimbabwe na Tanzania kuijadili Msumbiji
Wilaya ya Nsanje nchini Malawi imepokea kaya 2,182 zinazotafuta hifadhi, huku kamishna wa wilaya- hiyo, Dominic Mwandira, akiielezea hali hiyo kuwa mbaya na inahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.
Vurugu hizo zimejumuisha uporaji, uchomaji moto, na maandamano yenye vurugu, na kusababisha kufungwa kwa biashara katika mji mkuu wa Maputo na maeneo mengine.
Utata wa uchaguzi na wasiwasi wa kimataifa
Waangalizi wa kimataifa wamebaini dosari katika uchaguzi wa Oktoba 9. Wakati tume ya uchaguzi ilitangaza ushindi wa asilimia 71 kwa Frelimo, Baraza la Katiba lilipunguza takwimu hiyo hadi asilimia 65.17.
Waangalizi wa Magharibi wamekosoa uchaguzi huo wakisema haukuwa huru wala wa haki.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amewahimiza viongozi wa kisiasa kupunguza mvutano kupitia mazungumzo na hatua za kisheria, akitoa wito wa suluhisho la amani kwa mzozo huo.
Uvunjaji gereza na kuongezeka kwa ghasia
Machafuko yalifikia kiwango cha juu Siku ya Krismasi baada ya vurugu kubwa katika gereza la usalama wa juu jijini Maputo, ambapo wafungwa 6,000 walitoroka, wakiwemo magaidi 29 waliokuwa wamehukumiwa.
Uasi huo ulisababisha vifo vya wafungwa 33 na majeruhi 15, huku wafungwa wakichukua silaha na kubomoa kuta za gereza.
Mkuu wa polisi wa Msumbiji, Bernardino Rafael, ametoa wito kwa waliotoroka kujisalimisha na kwa wananchi kuwa waangalifu.
Video zinazosambaa mtandaoni zinaonyesha wafungwa wakitoroka, huku baadhi yao wakikamatwa tena walipojaribu kujificha.
Athari kwa uchumi na kampuni za kigeni
Ghasia hizo zimevuruga shughuli za kampuni za kigeni, zikiwemo kampuni za madini kama Gemfields na South32, pamoja na kampuni ya petroli, Sasol.
Soma pia: Zaidi ya wafungwa 1,500 watoroka Msumbiji katika machafuko ya uchaguzi
Gemfields ilisitisha kwa muda operesheni zake kwenye mgodi wake wa madini ya zumaridi kufuatia vurugu karibu na eneo hilo, ikiwa ni pamoja na jaribio la watu 200 kuvamia makazi ya wafanyakazi na kuchoma moto majengo.
Vikosi vya usalama vya Msumbiji vilipiga risasi na kuua watu wawili waliokuwa wakihusika.
Muktadha wa kihistoria na mtazamo wa baadaye
Chama cha Frelimo, ambacho kimeiongoza Msumbiji tangu uhuru mwaka 1975, kinakosolewa kwa namna kilivyoshughulikia mgogoro huo na madai ya udanganyifu wa uchaguzi.
Uthibitisho wa Baraza la Katiba wa ushindi wa Chapo umechochea maandamano na migomo inayoendelea.
Serikali ya Chapo sasa inakabiliwa na jukumu kubwa la kushughulikia ukosefu wa usawa, kujenga upya uchumi, na kuunganisha taifa lililogawanyika sana.