Rais Samia kugharamia mazishi ya Kadhi wa Mkoa wa Morogoro

Morogoro. Rais Samia Suluhu Hassan ameaihidi kugharamia shughuli zote za mazishi ya aliyekuwa Kadhi wa Mkoa wa Morogoro Sheikh Mussa Bolingo ambaye amefariki jana Ijumaa Desemba 27,2024 saa moja usiku katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro alikopelekwa kupatiwa matibabu.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Desemba 28,2024 Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Musa Kilakala amesema Rais Samia ametoa ahadi hiyo mapema asubuhi hii kwa njia ya simu baada ya kumpigia na kutoa pole za Serikali kwa ndugu na Waislamu wa Mkoa wa Morogoro na mikoa mingine pamoja na Watanzania kwa ujumla.

Kilakala amesema katika salamu hizo, Rais Samia amewataka Waislamu kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wanachopitia, pia kumuombea kiongozi huyo ambaye alihudumu katika nafasi yake kama kadhi kwa zaidi ya miaka sita.

Mkuu huyo wa wilaya akizumzungumzia marehemu Bolingo, amesema katika uhai wake alikuwa ni kiongozi aliyeshirikiana vizuri na Serikali katika mambo mbalimbali na hata kwenye shughuli za kijamii.

 “Hata kwenye msikiti aliokuwa akiswalisha aliweza kuibua miradi ya kuongeza kipato ikiwemo ujenzi wa Zahanati ya Msikitini. Hata hivyo ujenzi wa zahanati hiyo umefikia hatua ya kupaua. Marehemu Sheikh Bolingo alikuwa ni mtu niliyeshirikiana naye kwenye shughuli mbalimbali za kiserikali, kwa kweli amepotea mtu makini sana,” amesema Kilakala.

Akizungumzia taratibu za kiserikali kwenye kushiriki mazishi mkuu huyo wa wilaya, amesema kwa sasa wanasubiria viongozi wakuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kutoka makao makuu pamoja na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zuber ambaye atafika Morogoro mapema leo kwa ajili ya mazishi.

Awali ofisa habari kutoka ofisi ya Kadhi Mkoa wa Morogoro, Suffy Hashim amesema Sheikh Bolingo alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari kwa muda mrefu ambapo jana Ijumaa asubuhi alipelekwa katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro baada ya hali yake kuwa mbaya.

“Baada ya Sheikh Bolingo kufikishwa hospitali madaktari walianza kumpatia matibabu ya haraka hata hivyo ilipofika saa nane mchana hali yake ilibadilika na kuwa mbaya na hivyo aliingizwa kwenye chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi (ICU) na ilipofika saa moja usiku alifariki dunia,” amesema Hashim.

Amesema baada ya vikao vya familia na viongozi wa Bakwata imeamuliwa kuwa Sheikh Bolingo atazikwa leo Jumamosi saa kumi jioni baada ya swala ya alasiri katika eneo la Msikitini wa Luquman uliopo Kihonda kwa Chambo Manispaa ya Morogoro.

Miongoni mwa watu wa karibu wa marehemu Sheikh Bolingo ni Sheikh Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Sheikh Mwinyiamani Thenei ambaye amesema kuwa kifo cha kiongozi huyo ni pigo kwa Bakwata pia kwa Waislamu wote wa Mkoa wa Morogoro.

 “Sheikh Bolingo alikuwa ni kadhi na kadhi ndiyo mwanasheria mwenye jukumu la kusulushisha na kutatua migogoro ya Waislamu kupitia sheria ya Kiislamu, hivyo katika nafasi yake hiyo ameweza kusulushisha migogoro mingi ya Waislamu ikiwemo ya ndoa, mirathi na mgawanyo wa mali,” amesema Thenei.

 Amesema kupitia marehemu Sheikh Bolingo, viongozi wengi wa Kiislamu akiwemo yeye mwenyewe wameweza kupata elimu na maarifa.

“Mimi nina miaka kama sita tangu nimfahamu lakini kwa muda huo nimeweza kuona uwezo wake kwenye dini, kwa kuwa anaelimu, ana maarifa, anahekima, kwa kweli Waislamu tumeguswa sana na kifo cha kadhi ila ndio hatuna cha kufanya kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndio amekadiria hili litokee na kila nafsi lazima ionje umauti,” amesema Sheikh Thenei.

Related Posts