Moscow. Shirika la Ujasusi la Russia (FSB) limedai kumkamata raia wa nchi hiyo akidaiwa kukubaliana na vikosi vya Jeshi la Ukraine kufanya jaribio la mauaji ya mwanablogu na Ofisa wa Juu wa Jeshi la Russia kwa kumlipua na bomu.
Katika taarifa iliyotolewa leo Jumamosi Desemba 28, 2024 na FSB, mtuhumiwa huyo amewaeleza wapelelezi kuwa Ukraine ilimuona kuwa mtu sahihi kutekeleza mashambulizi hayo kupitia maoni yake anayoyatoa kwenye mitandao ya kijamii.
Kwa mujibu wa FSB, walioratibu mpango huo walimtumia ujumbe na kumualika kuwa miongoni mwa maofisa wa akiba wa siri Shirika la Ujasusi la Ukraine (HUR).
Ukraine pia inatuhumiwa kuratibu mpango mzima wa kusafirisha na kuingiza bomu hilo hadi alipo mtuhumiwa kwa kulivalisha vilipuzi maarufu kama IED.
Russia Today imeripoti kuwa mtuhumiwa huyo aliieleza FSB kuwa mpango wa awali ulikuwa kulipandikiza bomu hilo kwenye gari la mwanablogu itakapokuwa imeegeshwa nyumbani kwake.
Mwanablogu huyo ambaye jina lake limehifadhiwa amekuwa akiripoti mwenendo wa vita inayoendelea kati ya Russia na Ukraine.
Hata hivyo, mtuhumiwa huyo aliugua ghafla ndipo maofisa hayo wa Ukraine walipoamua kuharibu mchezo na kutibua mpango huo.
Baadaye, alitakiwa kutumia bomu hilo kutekeleza mauaji dhidi ya Ofisa wa Juu wa Jeshi la Russia (jina limehifadhiwa) ndipo alipokamatwa katika jitihada za kulitega alipokuwa ofisa huyo.
Tayari mtuhumiwa huyo ameshakamatwa na kufikishwa nahakamani nchini Russia kwa tuhuma za kufanya jaribio la kufanya mauaji dhidi ya Ofisa wa Jeshi la Russia na mwanablogu huyo.
Shirika la FSB limeachia kipande cha video kikionyesha bomu hilo lililotengenezwa kwa kutumia sumaku.
Bomu hilo baada ya kuchunguzwa limebainika kuwa na uzito unaokadiriwa kuwa wa vilipuzi vya TNT vyenye kilo 1.5.
Russia imetumia roboti kulipeleka sehemu salama kwa ajili ya kuteguliwa.
Katika kipindi cha wiki moja, FSB imekuwa ikiripoti kudhibiti majaribio ya mauaji dhidi ya maofisa wa juu ya jeshi la nchi hiyo, mauaji ambayo yanatajwa kuratibiwa na majasusi wa Ukraine.
Mapema mwezi huu, Ukraine ilidaiwa kutekeleza mauaji ya aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Silaha za Nyuklia, Biolojia na Kemikali wa Russia, Luteni Jenerali, Igor Kirillov na msaidizi wake.
Igor na msaidizi wake waliuawa nje ya mlango wa nyumba aliyokuwa akiishi jijini Moscow katika bomu ambalo lilitegwa kwenye baiskeli inayotumia umeme maarufu kama Skuta.
Taarifa iliyotolewa na maofisa wa upelelezi nchini Russia ilidai kuwa tayari msako ulifanikisha kukamatwa kwa raia wa Uzbekistan, Akhmad Kurbanov mwenye umri wa miaka 29 akidaiwa kutekeleza shambulizi hilo.
Mauaji ya Luteni Jenerali, Igor Kirillov na msaidizi wake yalitajwa na Russia kuwa ni tukio la kigaidi lililofanywa na Ukraine dhidi ya maofisa wa juu ya Jeshi hilo la Russia.
Tamko la tukio hilo kuwa la kigaidi lilitolewa na Msemaji wa Kamati ya Uchunguzi wa tukio hilo lililotokea eneo Ryazansky, Svetlana Petrenko aliyesema bomu lililowaua maofisa hao wa jeshi lilikuwa na uzito wa Gramu 300 za vilipuzi.
Petrenko pia alisema mauaji ya maofisa hao pia yanachukuliwa kama ya kukusudia, huku akisema kwamba tayari Kamati hiyo imeanzisha uchunguzi dhidi ya uingiaji holela wa silaha zilizotumika kuwalipua viongozi hao.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika