Wananchi wa wilaya ya Ludewa mkoani Njombe wameendelea kunufaika na matunda ya serikali ya awamu ya sita kwa kukabidhiwa vyombo vya usafiri ikiwemo piki piki pamoja na magari ya kubeba wagonjwa (AMBULANCE) kwenye vituo vyote vya kutoa huduma za afya wilayani humo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa gari mpya ya kubeba wagonjwa kwa ajili ya hospitali ya wilaya ya Ludewa iliyotolewa na Ofisi ya Rais (TAMISEMI) mganga mfawidhi wa hospitali ya wilaya DKT.ISACK CHUSSI amesema wilaya hiyo ni moja ya wilaya yenye vituo vingi vya afya pamoja na hospitali zinazofikia 81 ambapo mpaka sasa vituo vyote vya afya vimepata gari ya wagonjwa na sasa hospitali yao imeongezewa gari ili kuboresha ufanisi kwenye usafiri.
“Halmashauri yetu ina vituo vya afya vingi sana na tuna jumla ya hospitali na vituo vya afya 81 na vituo vyetu vya serikali vyote tuna huduma za usafiri kwa hiyo tumeongezewa sasa hii Ambulance nyingine ambayo itaongeza ufanisi kwenye usafiri”Amesema Dkt.Isack Chussi
Kwa upande wake Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Ludewa Castory Kibasa amesema licha ya magari waliyotapata lakini serikali imetoa pikipiki huku Kaimu Mganga mkuu wa wilaya hiyo Godlove Katemba akilia na upungufu wa watumishi.
Naye Mbunge wa Ludewa Joseph Kamonga ameahidi kuendelea kushirikiana na wananchi ili kusukuma maendeleo.
“Nimejitahidi sana kutafuta magari tena sio ya halmashauri peke yake hata taasisi zingine,ukienda Polisi,TFS,na TANESCO tunahangaikia gari la kubeba nguzo kwa hiyo ndugu zangu niwahakikishie hamkufanya makosa kunituma niwawakilishe”amesema Kamonga
Nao baadhi ya wananchi wa Ludewa akiwemo Athman Haule pamoja na Merry Mlelwa wameshukuru kuongezewa usafiri huo utakaorahisisha kusafirish wagojwa inapotokea dharula.