TASHICO YAFAFANUA MELI MV SERENGETI KUZAMA ZIWA VICTORIA

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

KAMPUNI ya Meli Tanzania (TASHICO) imefafanua tukio la kuzama kwa meli ya MV Serengeti katika Bandari ya Mwanza Kusini,Ziwa Victoria, baadaa ya kukumbwa na tatizo la kuegemea upande wa nyuma na kutitia chini ndani ya maji.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO, Wakili Alphonce Paul Sebukoto, ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Disemba 26, majira ya saa 8:00 usiku, ambapo meli ilionekana kulalia upande wa nyuma na kuzama majini.

Amesema kuwa walipokea taarifa ya meli hiyo kuingiza maji na hivyo kuzama upande wa nyuma baada ya kuelemewa na maji , ikiwa imeegeshwa katika ghati eneo la Bandari ya Mwanza Kusini, wilayani Nyamagana.

“Meli haijafanya biashara muda mrefu ilikuwa imeegeshwa tangu mwaka 2016, ikisubiri kufanyiwa ukarabati mkubwa. Hii ni meli ambayo ilisitisha kutoa huduma ya usafirishaji wa mizigo na abiria,” amesema Wakili Sebukoto.

Amesema MV Serengeti, imetengewa fedha za ukarabati ni moja ya meli nne zilizokuwa zimesimamishwa na serikali ili kufanyiwa ukarabati mkubwa,zingine ni MT Ukerewe, MV Nyangumi na ML Wimba na zinakaguliwa kila mwaka na wataalamu wa kiusalama ili kuhakikisha usalama wa meli hizo.

“MV Serengeti haikuwa na matatizo yoyote ya kiusalama,iko katika mpango wa matengenezo mwaka huu wa fedha 2024/25.Meli hii inakaguliwa kila mwaka na wataalamu wa usalama na siku chache kabla ilikaguliwa na kuonekana iko salama.”

Wakili Sebukoto ameongeza kuwa chanzo cha meli hiyo kujaa maji bado hakijajulikana, na kuna uwezekano wa kuchakaa kwa baadhi ya vyuma vya meli, au kupigwa mawimbi makali ambayo yanaweza kuleta tatizo hilo.

Amesema bado ni mapema kusema nini kimesababisha meli ilemewe na maji hadi kuzama upande wa nyuma, hivyo baada ya kunyayuliwa utafanyika uchuguzi wa kitaalamu kuibaini tatizo.

“Meli hii iliyojengwa mwaka 1988 ina uwezo wa kubeba abiria 500 na tani 250 za mizigo. Ni meli muhimu yenye faida kwa TASHICO na serikali, hasa katika maeneo yasiyo na miundombinu ya bandari, ikiwemo visiwani,” amesema Wakili Sebukoto, akisisitiza umuhimu wa ukarabati wa meli hiyo.

Akijibu maswali kuhusu tukio lingine la meli ya MV Clarias, Wakili Sebukoto amefafanua kuwa, hilo halihusiani na la MV Serengeti na kubainisha wazi kuwa MV Clarias ililalia upande mmoja ikiwa ghatini baada ya kutoka safari katika visiwa vya Gana na Goziba.

Amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini ikiwa kulikuwa na uzembe au hujuma katika matukio yote mawili,endapo uchunguzi utaonesha uzembe au makosa ya watu, hatua kali zitachukuliwa ikiwemo watu kufikishwa mahakamani.

“MV Clarias ilikuwa na tatizo la matundu (Stain tube) yaliyo na upana usio wa kawaida, ya kuruhusu maji kuingia ndani ya meli na kupumua kwa kiwango kinachotakiwa.Uchunguzi unaendelea na hatua zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kuhusika,” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo wa TASHICO.

Naye, Said Sekiboto wa Kitengo cha Uokoaji Ndani ya Maji cha Jeshi la Zimamoto ya Uokoaji, Mkoa wa Mwanza, ameeleza kuwa hatua za dharura zinaendelea kuchukuliwa ili kuinyanyua meli ya MV Serengeti.

Amesema kuwa walifika katika tukio majira ya saa 8:00 usiku (Disemba 26,) baada ya kupata taarifa za meli hiyo kuzama, lakini walishindwa kufanya operesheni ya kuinyanyua mara moja kutokana na changamoto za vifaa.

“Vifaa tulivyokuwa navyo havikuwa na uwezo wa kuinyanyua meli kwa haraka, lakini sasa tumeimarisha vifaa hivyo na tunaendelea na operesheni ya kuinyanyua.Tutatumia vifaa vya ziada kuendelea na kazi ya kuinyanyua meli na kufyonza maji yaliyokuwa yamejaa ndani pamoja na kwenye Chelezo,”alisema.

Sekiboto ameongeza kuwa, licha ya meli hiyo upande wa nyuma kuzama hakuna madhara, sehemu ya mbele inaendelea kuelea juu ya maji, kazi ya kuondoa maji ndani ya meli itafanyika kwa siku nzima ili kuhakikisha usalama wa meli na kuirejesha hali yake.
Hivyo, TASHICO na vyombo vingine vya usalama, likiwemo Jeshi la Zimamoto, vinaendelea na operesheni hiyo kwa umakini mkubwa kuhakikisha meli inarejeshwa kwa usalama na kuondoa hatari yoyote inayoweza kutokea kwa umma na mali za serikali ili kusubiri uchunguzi zaidi wa kitaalamu.

Related Posts