Marekani. Rais mteule wa Marekani, Donald Trump ametoa wito kwa Mahakama ya Juu nchini humo kuchelewesha uamuzi wa kuufungia mtandao wa Tiktok hadi atakapoingia madarakani.
Tovuti ya The Guardian imeripoti kuwa Trump, anayetarajiwa kuapishwa Januari 20, 2025, amesema anaamini atapata suluhu la kisiasa la changamoto zilizoibuka kwenye matumizi ya mtandao huo unaomilikiwa na kampuni ya ByteDance ya China, jambo linalouweka katika hatari ya kufungiwa kutumika nchini humo.
Tiktok ambayo inakadiriwa kuwa na watumiaji takriban milioni 170 nchini Marekani, inakabiliwa na tishio la kufungiwa ifikapo Januari 19, 2025 endapo haitauza umiliki wake kwa kampuni za Marekani, ikiwa ni siku moja tu kabla ya Trump kurejea Ikulu ya White House iliyoko Washington nchini humo.
Awali, Mahakama ya Juu ilikataa ombi la TikTok la zuio la dharura dhidi ya kufungiwa, lakini ilikubali kusikiliza tena hoja za pande zote kwenye kesi hiyo Januari 10, 2025.
Tiktok inatuhumiwa kutumika na Serikali ya China kuingilia taarifa binafsi za raia wa Marekani.
Tuhuma hizo ziliibuliwa na Bung la Congress nchini humo Aprili 2024, na kuamuru mtandao huo kufungiwa kutumika nchini humo ama uuzwe kwa kampuni inayomilikiwa na Mmarekani kabla ya Januari 19, 2024.
Uamuzi huo wa Trump kuikingia kifua TikTok ni kinyume na aliowahi kutoa mwaka 2020, alipoonyesha nia ya kuifungia kutumika nchini humo kwa sababu tu ya umiliki wake kuwa mikononi mwa raia wa China.
Pia, mchango wa TikTok kwenye kampeni za Trump dhidi ya mpinzani wake Kamala Harris wa chama cha Democrats, unatajwa kuwa sababu ya Rais huyo mteule kuomba kucheleweshwa kwa uamuzi huo.
“Rais Trump hayuko upande wowote kwenye sakata hili la TikTok,” amesema D John Sauer, ambaye ni mwanasheria na mteule wa nafasi ya Wakili Mkuu wa Serikali katika uongozi ujao wa Trump.
“Badala yake anaiomba Mahakama kuchelewesha kidogo uamuzi wa shauri hilo usitolewe kabla ya Januari 19, 2025, lengo ni kutoa mwanya kwa uongozi ujao madarakani kutafuta mwarobaini wa suala hilo,” amesema Sauer.
Awali, Trump alikutana na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa TikTok, Shou Zi Chew, Desemba 2024 muda mfupi baada ya kutangazwa kuwa mshindi wa nafasi ya urais wa nchi hiyo na kudai kwamba jukwaa hilo ni miongoni mwa maeneo yalivyochangia ushindi wake na angetamani ikiendelea kutumika nchini humo.
Pia, Trump alionekana akijikusanyia mabilioni ya ufuatiliaji ‘views’ kila alipochapisha maudhui kwenye mtandao huo wakati wa kampeni za urais wa nchi hiyo.
TikTok haijatoa kauli yoyote kuhusiana na ombi hilo la Trump kuhusu shauri linaloikabili mahakamani.
Hata hivyo, kampuni hiyo iliwahi kusema kuwa bunge hilo la Congress limeshindwa kutofautisha ushirikiano wake na China kwa kile ilichodai mfumo wa uhifadhi wa taarifa za watumiaji uko nchini Marekani na kusema miongozo yote ya matumizi yake imetengenezwa nchini humo.
Kitengo cha sheria nchini Marekani kimekuwa kikidai kwamba umiliki wa Tiktok kuwa nchini China unahatarisha usalama wa Marekani na taarifa za raia wa nchi hiyo, jambo lililoungwa na wabunge hao.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika