Arumeru. Ni majonzi, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Ofisi ya Hazina, Amos Nnko na binti yake Maureen wakizikwa.
Nnko na Maureen (16) walifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea Same mkoani Kilimanjaro Desemba 22, 2024.
Katika ajali hiyo, Agnes mke wa Nnko, watoto wao wawili Merilyne na Melvine na msaidizi wa nyumbani, Sylvana Lugwalu walijeruhiwa.
Maziko yamefanyika leo nyumbani kwa Nnko katika Kijiji cha Seela, Kata ya Seela Sing’isi, wilayani Arumeru Mkoa wa Arusha.
Kabla ya maziko kulifanyika ibada katika uwanja wa Shule ya Sekondari Seela iliyoongozwa na Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Meru, Mchungaji Ndelekwa Pallangyo.
Licha ya kuwa mtumishi wa umma, Nnko tangu mwaka 2018 hadi anafikwa na mauti alikuwa mzee wa kanisa katika Kanisa la KKKT, Usharika wa Mbezi Beach, jijini Dar es Salaam.
Waombolezaji waliangua vilio miili ilipowasili uwanjani kwa ajili ya kuagwa. Ilikuwa imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru.
Miili ya marehemu iliingizwa uwanjani ikisindikizwa na wazee wa kanisa kutoka Usharika wa Mbezi Beach.
Maureen alikuwa amemaliza kidato cha nne mwaka huu 2024 akisubiri matokeo. Alikuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Mt. Monica ya jijini Arusha.
Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu akitoa salamu amesema Nnko alikuwa mtumishi mwema wa umma na mahiri katika utendaji kazi.
“Alikuwa mtumishi mwema wa umma, inajieleza katika wasifu wake. Kuzunguka nafasi zote hizo inaonyesha umahiri na utendaji wake ulivyokuwa mzuri. Tunamshukuru Mungu kwa maisha yake ya miaka 48 aliyompa.
“Shemeji yangu (Agnes) Mungu atakuinua, sote tumeshuhudia picha ya lile gari, sote hatuamini kama mtu alitoka kwenye lile gari. Kukutoa mzima ana jambo na wewe na watoto aliokuachia,” amesema.
“Amos kazi yake ya kiroho pia na nafasi zake zote wamemshuhudia tangu alivyomaliza shule, kabla hajaajiriwa alijitolea kuja kufundisha wengine, ni mtu wa watu,” amesema.
Akitoa salamu za Serikali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo, amesema kifo ni fumbo na kinaacha alama ya simanzi na maumivu yasiyofutika.
“Tumepokea taarifa za msiba kwa mshtuko mkubwa, hakika analofikiria mwanadamu ni tofauti na analofikiria Mungu. Tujiandae kwa kifo wakati wote kwani hatujui muda.
“Watumishi tufanye kazi kwa bidii. Ukisoma wasifu wa Nnko alifanya kazi kwa bidii. Tuna wajibu wa mara zote kutimiza majukumu yetu tuliyojipangia kwa wakati kwani hatujui wakati wetu. Tunaloweza kufanya leo tufanye, ukiahirisha huwezi kujua kesho utaamka kutekeleza,” amesema.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema katika maisha ya mwanadamu yapo mambo unaweza kuzoea isipokuwa kifo.
“Nimesimama hapa kuungana na waombolezaji wote kuipa pole familia, najua shemeji una huzuni kubwa moyoni, unajiuliza mume ambaye mlikuwa mnamtegemea, msaada mtapata wapi ila msaada u- katika bwana aliyeziumba mbingu na nchi. Tusihuzunike kama watu waliokosa imani,” amesema.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Daniel Pallangyo amesema alipata taarifa za msiba kwa mshtuko kwa kuwa alifanya kazi na Nnko aliyekuwa mpole na mahiri katika kazi.
“Meru tumepigwa na kitu kizito, ni msiba mkubwa kwa Meru hatuna la kufanya. Kifo ni amri ya Mungu, kuna vifo vingine ni vigumu kuvumilia unatoka kituo A unaendesha gari lako umejipanga vizuri, ndugu zako waliokuwa wanakusubiri wanapokea mwili baridi, ni jambo gumu tuombe Mungu atuwezeshe kupokea,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amir Mkalipa amesema wilaya imepoteza mzalendo na kielelezo cha wasomi katika eneo hilo.
“Tumepoteza ndugu aliyekuwa anatusaidia kwa hali, fikra, mipango na mikakati. Tumepata pengo kubwa,” amesema.
Katibu Baraza la wazee Usharika wa Mbezi Beach, wa kanisa la KKKT, Elizabeth Mangesho amesema wamepokea kwa mshtuko taarifa za vifo hivyo.
“Kama familia ya usharika, Amos tumetumika naye tangu 2018 akiwa mzee wa kanisa. Pengo lake ni kubwa hatujapata dira huko mbele tunaendaje,” amesema.