Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linamshikilia dereva wa lori la mafuta, Jackson Kashebo (45), mkazi wa Mbagala, mkoani Dar es Saalam na utingo wake, William Sichone (34), mkazi wa mtaa wa Chapwa wilayani Momba wakituhumiwa kusafirisha vipodozi vyenye viambata vya sumu.
Taarifa ya polisi imesema alikuwa akiendesha lori lenye namba za usajili T 747 DDE na tela namba T 330 CJX aina ya Faw.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga katika taarifa hiyo amesema walikamatwa wakiwa na maboksi 201 ya vipodozi hivyo Desemba 28, 2024 saa 11:15 asubuhi katika Mtaa wa Keseria, Kata ya Chapwa wilayani Momba.
Amesema walikamatwa baada ya Polisi kupata taarifa za siri na kuweka mtego uliowezesha kuwatia mbaroni wakiwa wamepakia na kusafirisha shehena ya vipodozi hivyo kwenye vyumba vya kubebea petroli na dizeli wakitokea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Vipodozi walivyokamatwa navyo ni Extra clair, Betasol tube, Pawpaw cream, Snail white, Prety white, Extra clair lemon, Bronz tone, Clear therapy, Parfect white, Cocopup water, Esapharm movete na Esapharma lemonvate.
Mbali na hilo, polisi wakishirikiana na wataalamu kutoka TFRA na Halmashauri ya Mji wa Tunduma limewakamata watuhumiwa Gosso Mussa (32) na Prisca Shembe (37), wakazi wa Sogea, Tunduma wakiwa na mifuko 125 iliyofungashwa bila kibali na kuuza mbolea kinyume cha bei elekezi.
Wanadaiwa kufanya udanganyifu wa kuuza mbolea ya DAAP Plus ya kampuni ya Minjingu iliyofungashwa kwenye mifuko ya DAP ya kampuni ya Falcon ETG.
Pia wanatuhumiwa kupatikana na mashine ya kushonea mifuko na mifuko tupu mipya 153 ya kampuni mbili tofauti.
Wanadaiwa kukamatwa leo Desemba 28, 2024 saa 2:00 asubuhi katika Mtaa wa Unyamwanga, Kata ya Tunduma wilayani Momba.
Taarifa ya polisi imesema mifuko ilifichwa kwenye ghala la kuhifadhia bidhaa mbalimbali za pembejeo kwa lengo ya kuiuza.
Kamanda Senga amesema upelelezi wa shauri hili unaendelea na kwamba watuhumiwa wote wanne watafikishwa mahakamani, upelelezi utakapokamilika.