Wachaga wanavyokula maisha mwisho wa mwaka

Moshi. “Wachaga hatuna shughuli ndogo.” Hayo ni baadhi ya maneno yanayozungumzwa na wenyeji wa Mkoa wa Kilimanjaro,  ambao wameendelea kusherekea sikukuu za mwisho wa mwaka, wakifanya sherehe kwa kuchoma na kunywa.

Baadhi yao ni wale waliotoka mikoa mbalimbali kuja mkoani hapa kusherekea sikukuu za mwisho wa mwaka pamoja na ndugu jamaa na marafiki.

Hata hivyo, asubuhi kunapokucha ni kama vile mji haupoi na watu hawalali, kwani unapopita kwenye maeneo ya kumbi za starehe, ni mwendo wa foleni za magari kwenye maeneo hayo.

Mwananchi limepita katika kumbi mbalimbali za starehe zilizopo katikati ya mji wa Moshi na kushuhudia wingi wa magari yakiwa yameegeshwa katika maeneo hayo na baadhi ya watu wakikosa mahali.

Wakizungumza na  Mwananchi leo, Desemba 28, 2024, wamesema kwao sikukuu za mwisho wa mwaka ni muhimu kwani wanakutana ndugu, jamaa na marafiki na kuweka vizuri mipango yao kama familia au kijiji.

Joshua Mtui, mmoja wa wananchi wa mkoa huo, amesema sikukuu za mwisho wa mwaka kwao ni kama hija na ni lazima warudi nyumbani na kuchinja, akisema ni kama shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa kuwalinda mwaka mzima katika mihangaiko ya hapa na pale ya utafutaji.

Hivyo, amesema kwa kipindi chote wanapokuwa nyumbani hadi Januari ni kipindi kifupi ambacho hutumia fedha zao na kwamba haijalishi ni asubuhi au jioni kwao muda wowote ni sawa.

“Wachaga hatuna shughuli ndogo, tunapokutana, tunakula bata usiku na mchana bila kuchoka, mwaka mzima mtu uko porini ukirudi ni lazima usherehekee na wenzako na kile ambacho unakipata kwenye shughuli zako ukirudi nyumbani lazima ukae na ndugu zako mfurahi,” amesema.

Furaha Eusebi, mkazi wa Moshi, amesema utamaduni wa Wachaga kurejea nyumbani kusherehekea kila sikukuu za mwisho wa mwaka, unatoa fursa kwa baadhi ya familia kukaa kwa pamoja na kujadiliana mambo mbalimbali huku wakisherekea.

“Asikwambie mtu, yaani sisi Wachaga tuna utaratibu wetu, yaani tunapenda vitu vizuri hasa tunaporudi nyumbani sikukuu za mwisho wa mwaka, yaana kama ni ndafu tunazimenya hasa ndiyo furaha yetu,” amesema mmoja wa wananchi hao.

Naye, mmoja wa wamiliki wa kumbi ya starehe mjini hapa, amesema ujio wa wageni kwao ni neema kwa kuwa wanauza vinywaji na nyama choma na kwamba ni kipindi ambacho hutengeneza faida.

“Tangu Desemba 20, 2024 sisi huwa hatulali tunauza kuanzia asubuhi hadi asubuhi inayofuata, kwa kweli kwetu hii ni neema, hakuna kulala ni mwendo wa kuuza tuu,” amesema mfanyabiashara huyo.

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa huo, Nurdin Babu aliwatakia sikukuu njema wananchi wote wa mkoa huo na kuwataka kusherekea sikukuu hizo kwa amani, utulivu na kheri katika kuumaliza mwaka 2024.

“Niwatakie kheri na maandalizi mema ya sikukuu za mwisho wa mwaka 2024 na mwaka mpya 2025. Mwenyezi Mungu atajujalie tuweze kusherekea sikukuu zote kwa amani na utulivu na atujalie kila la kheri katika kuumaliza mwaka 2024,” amesema Babu.

Related Posts