Waliovamia ‘gesti’, kupora wapangaji kwa bunduki wakwama

Musoma. Siku ya kufa nyani miti yote huteleza, ni usemi unaoleza namna washtakiwa wa ujambazi wanaodaiwa kuvamia nyumba ya kulala na kuwapora wateja kwa mtutu wa bunduki, walivyokwaa kisiki kupangua kifungo cha miaka 30 jela.

Tukio lililowatia matatani lilitokea usiku wa manani Desemba 2, 2016 katika Kijiji cha Magunga wilayani Butiama, Mkoa wa Mara.

Siku hiyo, majambazi wenye silaya walifika katika nyumba kulala wageni ya Mjaja wakijifanya ni askari polisi wanaohitaji kuwachunguza wateja waliolala humo.

Kwenye tukio hilo, washtakiwa walichakaza mlango wa chumba kimojawapo cha nyumba hiyo ya kulala wageni, baada ya mteja aliyekuwa na mpenzi wake kugoma kufungua, alipobaini hawakuwa polisi, bali majambazi.

Awali, walitiwa hatiani na Mahakama ya Wilaya Butiama kwa makosa 12 ya uporaji wa fedha, simu na vitu mbalimbali vya wateja kwa kutumia silaha, wakakata rufaa Mahakama Kuu ambako walikwama na sasa wamekwaa kisiki tena kwenye Mahakama ya Rufani.

Katika hukumu iliyotolewa Desemba 27, 2024 jopo la majaji Shaban Lila, Pantrine Kente na Leila Mgonya lilibatilisha kutiwa kwao hatiani katika makosa 10, lakini likabariki hatia kwenye makosa mawili.

Kwa sheria za Tanzania, Mahakama ya Rufani Tanzania ndiyo chombo cha juu cha mahakama katika masuala ya rufaa kwenye makosa ya jinai, hivyo kwa hukumu hiyo, washtakiwa hao watatu wamefika mwisho katika kutetea haki yao.

Warufani ni Saimon Samson au Mwita, Chacha Gisinda au Mahairi na Zephania Mabura wameshindwa kujinasua katika makosa mawili kati ya 12 waliyokuwa wametiwa nayo hatiani.

Siku ya tukio, nyumba hiyo ya kulala iliyo na baa ikiwa imefungwa mageti na wateja kwakiwa vyumbani, majambazi waliokuwa na silaha za moto, mapanga, nondo na silaha nyingine waliivamia.

Kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani, majambazi hao walifika na kujitambulisha ni polisi na wanatekeleza jukumu lao la kuwatafuta watu wanaojihusisha na uhalifu.

Mrufani wa kwanza, Samson ndiye aliyetambuliwa kuwa alijitambulisha polisi.

Hivyo wakamweleza mlinzi aliyekuwa getini wanataka kuingia ndani kukagua kitabu cha wageni ili kuona kama kuna washukiwa wa uhalifu waliolala humo, lakini walipoingia walibadilika na kuwa majambazi.

Kwanza walikwenda kwa mtunza fedha na kupora simu na fedha taslimu zikiwamo za mauzo ya vinywaji ya siku hiyo, kabla ya kwenda chumba kimoja baada ya kingine kuwaamuru wapangaji kutoka vyumbani.

Wapangaji hao waliamriwa kukabidhi kila kitu cha thamani walichokuwa nacho, huku wakiwafanyia mateso na ukatili wa kisaikolojia ikiwamo kuwapekua waliokuwa na jinsia ya kike kwa kuingiza vidole sehemu zao za siri.

Mmoja wa wapangaji aliyekuwa na mpenzi wake wakati huo wakiwa hawajafungua mlango, alishuku watu waliokuwa nje ya chumba chao hawakuwa polisi kutokana na namna walivyokuwa wakiongea na amri walizotoa.

Mpangaji huyo akampigia simu Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya (OC-CID) ya Butiama na kumuuliza kama kuna polisi wametumwa katika nyumba hiyo ya kulala, akamweleza hajatuma watu wa aina hiyo katika eneo hilo.

OC-CID akamwahidi anatuma kikosi cha askari mara moja katika eneo hilo ili kukabiliana na majambazi hao. Wapenzi hao waliendelea kugoma kufungua mlango, kitendo ambacho kiliwaudhi majambazi hao.

Ilionekana kiongozi wa genge hilo na washirika wake walikuwa wakimfahamu mtu aliyekuwamo ndani ya chumba hicho, kwani walimwita kwa jina lake la Danny, ili afungue mlango, naye aligoma akiwa na matumaini polisi watafika kwa wakati.

Kiongozi wa genge hilo alimtaka Danny na mpenzi wake kufungua mlango vinginevyo wangewaua lakini waligoma, ndipo mrufani wa kwanza ambaye alikuwa akimfahamu, alijaribu kuvunja mlango wa chumba bila mafanikio.

Inadaiwa mrufani wa kwanza alimwamuru wa tatu, Mabura aliyekuwa na silaha, kuwashambulia kwa risasi kupitia nyufa zilizotokana na jaribio lake la kuvunja mlango kushindwa, ndipo risasi zisizo na idadi zilifyatuliwa kuelekea chumbani humo.

Kutokana na mfululizo wa risasi hizo, chumba kilijaa moshi mzito kiasi cha waliokuwamo kushindwa kupumua vizuri na kusababisha wakohoe, huku mpenzi wa Danny akiwa amepigwa risasi ya paja, ndipo wakaamua kufungua mlango.

Kama ilivyotokea kwa wapangaji wengine, nao waliporwa na majambazi hao. Polisi walipowasili eneo hilo, tayari majambazi hao walikuwa wametoweka na kutokomea kusikojulikana.

Polisi walianzisha msako na kuwakamata majambazo hao watatu ambao inaelezwa walipofikishwa polisi, waliandika maelezo ya onyo wakikiri kufanya tukio hilo, mmoja akiandika maelezo ya ungamo kwa mlinzi wa amani.

Hata hivyo, katika utetezi wao kortini, wote walikana mashtaka wakiegemea ushahidi wa alibi, wakieleza hawakuwepo eneo la tukio kwa muda na siku inayotajwa na mashahidi, hivyo wakataka waachiliwe huru na mahakama.

Hata hivyo, ushahidi huo haukuwasaidia, Mahakama ya Wilaya ya Butiama iliwatia hatiani kwa makosa yote 12 na kuwahukumu kifongo cha miaka 30 jela.

Baada ya hukumu hiyo, walikata rufaa Mahakama Kuu ambako waligonga mwamba na hukumu hiyo ikasalia vilevile, kisha wakapiga hodi Mahakama ya Rufani Tanzania iliyoketi Musoma.

Katika rufaa hiyo walitoa sababu mbili kupinga hukumu na adhabu wakipinga ushahidi wa utambuzi ambao Mahakama ya Wilaya ya Butiama iliuegemea, wakisema hakutosha kuwatia hatiani, hasa ikizingatiwa tukio lilitokea usiku wa manani.

Hoja ya pili ilikuwa ni kwamba maelezo yao ya kukiri kosa hilo ambayo walichukuliwa polisi na kupokewa mahakamani kama kielelezo, yalipokewa kwa kukiuka sheria na mahakama haikujiridhisha kama yalitolewa kwa hiyari.

Wakati wa usikilizwaji wa rufaa, warufani walijiwakilisha wenyewe kortini huku upande wa Jamhuri ukiwakilishwa na mawakili wawili wa Serikali, Isihaka Mohamed na Beatrice Mgumba kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka (NPS) Musoma.

Baada ya kuchambua ushahidi na hoja za rufaa, majaji waliridhika kuwa mashahidi wanne pekee ndio utambuzi wao kwa warufani ulikuwa sahihi na kuwa hawakutambuliwa kwa bahati mbaya, bali ushiriki wao ulielezwa.

Hata hivyo, majaji walikubaliana na Wakili Isihaka kuwa upande wa Jamhuri ulithibitisha pasipo kuacha shaka mashtaka mawili, na mengine 10 yaliyobaki hayakuthibitika kwa kuwa waathirika hawakuitwa kutoa ushahidi.

Majaji wakasema kifungu cha 34 cha Sheria ya Ushahidi kinaruhusu maelezo ya waathirika hao waliyoyatoa polisi kama ushahidi yapokewe na mahakama kama kielelezo, lakini upande wa Jamhuri haukufanya hivyo.

“Ni muhimu kueleza hapa kwamba kesi ya Jamhuri iliyofanikiwa katika kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha kama hili tulilonalo, ilikuwa ni muhimu sana Jamhuri kuleta ushahidi unaoelezea hatua kwa hatua namna uporaji ulivyokuwa,” inasema sehemu ya hukumu ya majaji.

Majaji hao wakaongeza kuwa kukosekana kwa ushahidi wa namna warufani walivyowapora fedha na simu waathirika ambao hawakutoa ushahidi, upande wa mashitaka hauwezi kusema kuthibitisha mashitaka ya aina hiyo.

Ni kutokana na msimamo huo, majaji walibatilisha kutiwa kwao hatiani na kuhukumiwa katika kosa la 1 hadi la 12, isipokuwa ikabariki kutiwa kwao hatiani na hukumu ya kifungo cha miaka 30, kwa kosa la tatu na la saba pekee.

Related Posts