Waziri Ulega akagua ujenzi wa barabara usiku

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amewataka makandarasi wanaotekeleza miradi ya barabara zikiwemo za mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), kuhakikisha wanakamilisha kazi kwa sehemu kubwa kabla ya mvua za masika hazijaanza.

Ametoa agizo hilo jana Ijumaa Desemba 27, 2024 alipofanya ziara kukagua maeneo ya Kimara Bucha, Mwenge na Lugalo kukagua ujenzi wa barabara za BRT na upanuzi wa ile ya Morogoro kuanzia eneo la Ubungo hadi Kimara.

Ziara hiyo aliyofanya usiku pia ililenga kuangalia utekelezaji wa agizo  alililotoa Desemba 15, 2024 alipotembelea miradi ya barabara jijini Dar es Salaam, alipoagiza kazi zifanyike usiku na mchana ili kukamilika kwa wakati.

Waziri Ulega amesema makandarasi wapo nyuma ya muda katika utekelezaji wa miradi hivyo wafanye juu chini kuhakikisha wanakamilisha ujenzi kwa muda waliokubaliana kwa kufanya kazi usiku na mchana.

Amesema agizo hilo halihusu barabara za jijini Dar es Salaam pekee bali hata za mikoani zinazotekelezwa.

“Wakimaliza mapema na kwa ubora kwetu ni faida ndiyo maana nimesisitiza kabla ya mvua za masika hazijaanza basi sehemu kubwa ya miradi iwe imekamilika. Mvua za masika zikianza vurugu yake itakuwa kubwa, tusingependa kuona watu wakitaabika.

“Waamsheni na wengine (makandarasi) waliolala ili kazi ziendelee, tuinaijenga nchi yetu na tutaendelea kuijenga Tanzania,” amesema.

Ulega amesema amefanya ziara ya kushtukiza ili kuona kazi inafanyika usiku na mchana kama alivyoagiza Desemba 15, 2024.

“Nimefurahi kuona watendaji hawa wanafanya kazi kama nilivyoagiza, lakini haya mambo sitaki yawe zimamoto, bali nataka yawe endelevu. Mtendaji Mkuu Tanroads na timu yako muwe na fikra ya kuwakagua wakati wote,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mohamed Besta amemuhakikishia waziri kwamba watasimamia maelekezo aliyoyatoa yakiwemo ya kazi zifanyike usiku na mchana.

“Mara ya mwisho ulipofanya ziara yako ulisema kazi zifanyike kwa saa 24, hivi leo (jana) katika Barabara ya BRT kutoka Mwenge hadi Tegeta mkandarasi anafanya kazi hadi usiku na sasa hivi ni saa tano usiku.

“Tutaendelea kufanya hivi hata pale wewe usipofanya ziara, sisi tutaendelea kusimamia maelekezo yako usiku na mchana ili tufikie malengo,” amesema.

Related Posts