Mamlaka za Korea Kusini zimedai kwamba watu 179 wamefariki dunia katika ajali ya ndege ya Shirika la Jeju iliyokuwa imebeba jumla ya abiria na wahudumu 181, hivyo ni abiria wawili pekee ndiyo waliotoka wakiwa hai.
Ndege hiyo aina ya Boeing 737-800 imepata ajali saa 6:03 usiku wa kuamkia leo Jumapili Desemba 29, 2024, katika Uwanja wa Kimataifa wa Muan nchini Korea Kusini, muda mfupi baada ya kushindwa kutua kwa kutumia tairi zake.
Picha na video zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha ndege hiyo ikitua kwa kasi kwa kutumia sehemu ya mwili wake badala ya kuanza kutua kwa tairi zake, jambo ambalo lilisababisha ilipuke na kusababisha madhara hayo.
Kwa mujibu wa Tovuti ya The Guardian, ndege hiyo iliyokuwa ikitokea Bangkok, Thailand kwenda Korea Kusini, abiria wawili waliokuwemo ni raia Thailand na waliosalia ni raia wa Korea Kusini.
Hadi kufikia saa 3:30 asubuhi, mabaki ya miili 120 ya abiria waliokuwemo ndani ya ndege hiyo yalikuwa yamepatikana na jitihada za maofisa wa Mamlaka ya Kupambana na Majanga ya Moto nchini humo wanaendelea kutafuta miili iliyosalia.
Majeruhi wawili walionusurika kifo, ambao ni abiria na mhudumu, wamepelekwa katika hospitali iliyoko karibu na uwanja huo wa ndege huku taarifa zikidai kwamba tayari Kaimu Rais wa Korea Kusini, Choi Sang-mok amefika eneo ilipotokea ajali hiyo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika