Ajali ya ndege yaua 85 Korea Kusini

Korea Kusini. Zaidi ya watu 85 wanahofiwa kufariki katika ajali ya ndege ya Kampuni ya Jeju iliyotokea uwanja wa ndege wa Jiji la Muan nchini Korea Kusini. 

Kwa mujibu wa Al Jazeera, ajali ya ndege hiyo iliyokuwa imebeba abiria 175 na wahudumu sita imetokea Saa 6:03 usiku wa kuamkia leo Jumapili, ilipokuwa ikitua katika uwanja wa Kimataifa wa Muan nchini humo.

Mamlaka ya Kupambana na Majanga ya Moto nchini Korea Kusini imesema ndege hiyo imepata ajali baada ya kuacha njia ya kutua na kulipuka ghafla katika uwanja huo.

Mamlaka hiyo imethibitisha kuwa tayari miili ya watu 85 wakiwemo wanawake 46 na wanaume 39 imeshapatikana na tayari moto uliolipuka na kuteketeza ndege hiyo umeshadhibitiwa.

Ikinukuu taarifa ya mamlaka hiyo ya majanga ya moto nchini Korea Kusini, Shirika la Habari la Yonhap nchini humo, limesema matumaini ya kupata manusura katika ajali hiyo yameanza kufifia.

Mwandishi wa Al Jazeera kutokea Seoul Korea Kusini, Rob McBride, amesema idadi kubwa ya waokoaji wamefika eneo uwanja ilipotokea ajali ya ndege hiyo ulioko takriban Kilometa 289 kusini mwa Mji Mkuu wa taifa hilo, Seoul.

“Ndege hii ilikuwa imerejea usiku wa leo kutokea Bangkok, Thailand. Inaonekana kulikuwa na hitilafu kwenye mfumo wa gia ya kurukia na kutua na picha zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha ikitua wa kutumia  sehemu ya chini ya mwili wake kisha mlipuko mkubwa ukafuata,” amesema McBride.

“Mashuhuda wanasema kwamba mlipuko uliotokana na ajali hiyo ni mkubwa kiasi kwamba huenda likawa ni janga kubwa kuwahi kutokea,” amesema.

Katika ndege hiyo aina ya Boeing 737-800, inadaiwa abiria waliokuwemo ni raia wawili wa Thailand na abiria waliosalia ni raia wa Korea Kusini.

Picha zinazosambaa mitandaoni zinaonyesha moshi mweusi ukifuka juu ya anga la ulipo uwanja huo wa Muan nchini Korea kutokea eneo ilipoanguka ndege hiyo. 
Picha nyingine zinaonyesha mabaki ya ndege hiyo hususan ni bawa la injini likiwa linawaka moto huku maofisa wa kuzima moto wakiendelea kupambana nao.

Shirika la Habari la Yonhap nchini humo, limedai huenda ndege hiyo ikawa imepata hitilafu kutokana na kugongana na ndege wawili (wanyama) jambo lililosababisha hitilafu kwenye mfumo wa gia ya kutua wa ndege hiyo.

Shirika la News1 limeripoti kuwa abiria waliokuwemo ndani ya ndege hiyo walikuwa wakiwatumia ndugu zao ujumbe wa simu kuwaeleza kuwa ndege (wanyama) wameingia kwenye injini ya ndege hiyo na hivyo huenda isitue kwenye uwanja wa ndege salama.

Ofisa mmoja kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini Korea (jina limehifadhiwa) amesema kuingiliwa na ndege (wanyama) ni miongoni mwa sababu zinazochangia ndege za abiria kupata ajali japo hlbado uchunguzi wa ajali hiyo unaendelea.

Kaimu Rais wa Korea Kusini, Choi Sang-mok, ameamuru jitihada za kila namna zifanyike ili angalau kunusuru abiria wanaoweza kuwa hai katika ajali ya ndege hiyo ilitokea uwanja wa Muan nchini humo.

“Mamlaka zote zinazohusika katika uokoaji … zishirikiane na kupeleka vifaa vyote vinavyohitajika kunusuru abiria waliosalia katika ajali hiyo,” imesema taarifa ya Ikulu ya Taifa hilo.

Jeju, ni miongoni mwa mashirika la ndege nchini Korea Kusini ambayo gharama zake za usafirishaji ziko nchini humo na lilianzishwa mwaka 2005. Tayari shirika hilo limeshatoa taarifa ya kuomba radhi na kusema: “Litafanya kila liwezekanalo kuwajibika kutokana na ajali hiyo.”

Ajali ya kwanza ya ndege ya Shirika la ndege la Jeju ilitokea Agosti 2007, ikihusisha ndege aina ya Bombardier Q400 iliyokuwa imebeba abiria 74 na kujeruhi wengine kadhaa. Ajali hiyo ilitokea katika uwanja wa ndege wa Busan-Gimhae ulioko Kusini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa wataalam wa anga wanaamini mfumo wa anga wa Korea Kusini ni imara hivyo huenda ikawa rahisi kubaini chanzo cha ajali hiyo na kuongeza usalama katika safari za ndege nchini humo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts