Askari 13, muuguzi wadaiwa kuua mfungwa kwa kipigo

Marekani. Askari 13 na muuguzi mmoja wako hatarini kufukuzwa kazi katika Gereza la Marcy jijini New York, Marekani baada ya kuhusika katika shambulizi lililosababisha kifo cha mfungwa katika gereza hilo.

Kipande cha video kilichotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali nchini humo, kinaonyesha askari hao wakimshushia kipigo mfungwa huyo, Robert Brooks (43) muda mfupi baada ya kufikishwa katika chumba cha matibabu kuangaliwa tatizo la kiafya linalomkabili.

Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali nchini humo, Letitia James, askari na muuguzi huyo walimshushia kipigo mfungwa huyo aliyekuwa anatumikia adhabu ya kifungo cha miaka 12 gerezani tangu mwaka 2017 na kusababisha kifo chake. 

Tukio hilo linatajwa kutokea Desemba 9, 2024 ndani ya gereza hilo.

“Ninalazimika kutoa kipande hiki cha video kinachoonyesha tukio zima la mauaji ya Brooks akiwa gerezani siyo kwa lengo la kuiumiza familia bali kuonyesha uwajibikaji na kuionyesha familia ya marehemu ukweli wa tukio hilo,” amesema Letitia.

Letitia amesema tayari uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo umeanza na wahusika wamesimamishwa kazi. Amesema wakikutwa na hatia watafukuzwa kazi na kushtakiwa kwa mauaji ya mfungwa huyo.

Gavana wa New York, Kathy Hochul amelaani tukio hilo aliloliita mauaji ya kutisha dhidi ya Brooks ambaye ni mfungwa katika gereza hilo.

Kipande hicho cha video kinawaonyesha askari wa Gereza la Marcy maarufu kama ‘New York State Department of Corrections and Community Supervision (DOCCS) wakimshushia kipigo, kumpiga ngumi na makofi huku wakiwa wamemfunga mikono nyuma kwa kutumia pingu kisha kumny’onga hadi kupoteza maisha

Brooks alianza kutumikia kifungo chake cha miaka 12 gerezani baada ya kutiwa hatiani kwa mauaji ya kukusudia mwaka 2017. Alihamishiwa katika gereza hilo siku chache kabla ya kifo chake akitokea katika gereza la Oneida Kaskazini mwa nchi hiyo.

Taarifa ya kifo chake ilitangazwa Desemba 10, mwaka huu katika Hospitali iliyoko eneo hilo ambako alipelekwa muda mfupi baada ya kufanyiwa unyama huo. 

Taarifa ya awali ya uchunguzi wa mwili wake imebaini kuwa mfungwa huyo alinyongwa na askari hao hadi kufariki.

Mwanasheria wa familia ya Brooks, Elizabeth Mazur amesema video hiyo inaonyesha; “akishambuliwa vibaya na askari ambao kiuhalisia kazi yao ilikuwa ni kumlinda na kumfanya awe salama,”

Mwanasheria huyo ameongeza kuwa: “Kila mfungwa anayeishi na kutumikia kifungo chake ndani ya gereza la Marcy hapaswi kuishi kwa hofu kutokana na matendo ya wafanyakazi waliopo ndani ya gereza hilo,” 

Umoja wa Vikosi vinavyosimamia magereza nchini Marekani vimetoa taarifa kwa Umma kuwa “Kitendo hicho hakikubaliki na hakiakisi kazi kubwa na nzuri inayofanywa na watumishi wa magereza yaliyoko nchini Marekani, tunalaani na hatuungi mkono unyama huu,”

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika

Related Posts