Bado tatu tu, Matampi anaswe

KIPA namba moja wa Simba, Moussa Camara ‘Spider’, ameendelea kung’ara katika Ligi Kuu Bara, kwa sasa akisaliwa na clean sheet tatu tu aifikie rekodi iliyowekwa msimu uliopita na kipa aliyekuwa Coastal Union, Ley Matampi aliyeachana na klabu hiyo hivi karibuni.

Matampi aliyetwaa tuzo ya Kipa Bora wa msimu akimzidi ujanja aliyekuwa mtetezi wa tuzo hiyo aliyekuwa akiishikilia kwa misimu miwili mfululizo, Diarra Djigui, kwa kupata clean sheet 15 kwa msimu mzima, wakati kwa sasa Camara amefikisha 12 katika mechi 15, ikiwa na maana akifanya hivyo michezo mitatu anaifikia.

Mapema juzi akizungumza na Mwanaspoti, Matampi alikiri mtu anayeweza kutwaa tuzo hiyo kwa msimu huu ni Camara kwa namna alivyoizoea haraka Ligi Kuu na pia kuwa na ukuta mgumu, ulioruhusu mabao matano tu hadi sasa na yenyewe ikifunga mabao 31 na kuongoza msimamo kwa pointi 40 kupitia mechi 15.

Kipa huyo kutoka Guinea, alifikisha clean sheet ya 12 juzi wakati Simba ikiichapa Singida Black Stars kwa bao 1-0 ikiwa ugenini ukiwa ni ushindi wa 13 kwa timu hiyo na wa tisa mfululizo sasa tangu ilipopasuka kwa Yanga katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Oktoba 19. Katika mchezo huo, kipa huyo alipangua mashuti mawili yaliyolenga lango kati ya manne na kumfanya aendelee kuwaburuza makipa wengine wanaomfuata kwa nyuma akiwamo Patrick Munthali wa Mashujaa mwenye clean sheet nane, wakati Diarra na Metacha Mnata wa Singida kila mmoja akiwa na saba.

Kulingana na idadi ya michezo iliyopo mbele (15) na kiwango alichoonyesha katika duru la kwanza, Camara anapewa nafasi ya kuvunja rekodi ya Matampi ambaye alikusanya clean sheets 15, akisaidia Coastal Union kurejea kwenye michuano ya kimataifa baada ya zaidi ya miaka 20.

Katika hatua nyingine, Simba inajiandaa kwa changamoto za kimataifa, ambapo itakutana na timu za CS Sfaxien ya Tunisia, Bravos do Maquis ya Angola na Constantine ya Algeria. Mchezo dhidi ya CS Sfaxien na Bravos do Maquis ugenini, pamoja na Constantine nyumbani, ni mitihani mikubwa kwa timu ya Simba, ambayo itakuwa ikisaka robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika michuano hii, Camara atakuwa na jukumu kubwa zaidi la kuhakikisha kuwa lango la Simba linabaki salama, ili kuendelea kutimiza malengo ya klabu hiyo katika mashindano ya kimataifa.

Related Posts